Serikali kumiliki asimilia 49 ya hisa kampuni ya Airtel Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisoma taarifa ya majadiliano kutoka kwa mgeni wake Bw. Sunil Mittal Mwenyekiti wa Bharti Airtel ( kampuni ya Simu ya Airtel ) mara baada ya Mazungumzo yao . Ikulu Jijini Dar es Salaam. Januari 11,2019.


Muktasari:

Kampuni ya Bharti Airtel imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi 49


Dar es Salaam. Kampuni ya Bharti Airtel imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi 49.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Januari 11, 2019 katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa baada ya mazungumzo kati ya Rais John Magufuli na mwenyekiti wa kampuni ya Bharti Airtel Sunil Mittal, waliokutaka Ikulu Dar es Salaam.

Wawili hao wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya mazungumzo hayo Mittal amesema kampuni yake imekubali kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika kampuni ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49.

Kwa uamuzi huo umepunguza  hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Bharti Airtel kutoka asilimia 60 hadi asilimia 51.

Mittal amesema mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.

Kwa upande Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo pamoja na kuongeza hisa za Serikali katika umiliki wa Airtel Tanzania.

Kampuni hiyo imekubali kutoa gawio kwa Serikali ya Tanzania mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika hivi karibuni.

“Masuala mengine ya kumalizia mazungumzo haya yataendelea leo ili kumalizia, lakini jambo zuri ni kuwa sasa wamekubali kutoa gawio kwa Serikali ambapo kwa muda wa miaka minane hadi kumi tulikuwa hatujapata gawio,” amesema Magufuli.

“Kiasi cha asilimia za gawio nacho watajadili leo, kwa hiyo mimi naona huu ni mwanga mzuri wa kwenda mbele kati ya kampuni ya Bharti Airtel na Serikali ya Tanzania pamoja na kampuni zingine.”

Timu ya majadiliano na kampuni ya Bharti Airtel inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa  Palamagamba Kabudi.