Ujenzi makazi ya Balozi Idd kuwekewa jiwe 2019

Muktasari:

  • Wahandisi wa ujenzi huo kutoka vitengo tofauti vya KMKM wako makini

Pemba. Uongozi wa Wakala wa Majengo umeieleza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwa mradi wa ujenzi wa makazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar utawekewa jiwe la msingi Januari 12 mwakani.

Uwekeji wa jiwe hilo, umo kwenye ratiba ya maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi Zanzibar yatayofanyika Januari 12 mwakani.

Mshauri mwelekezi wa ujenzi huo, Mansour Mohamed Kassim alieleza hayo katika ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika Kijiji cha Pagali Chake Chake Pemba.

Mansour alisema mradi huo uko kwenye hatua nzuri ya ujenzi wa majengo yote yaliyokusudiwa kujengwa awamu ya kwanza.

Kamanda wa kitengo cha ufundi wa Kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar (KMKM), Hamad Masoud Khamis alisema awamu ya pili ya mradi huo itazingatia ujenzi wa uzio utakaozunguka kijiji hicho pamoja na mfumo wa huduma za kijamii.

Alisema wahandisi wa ujenzi huo kutoka vitengo tofauti vya KMKM wako makini katika kutekeleza kazi hiyo.

Balozi Idd aliwapongeza wajenzi wa mradi huo kwa jitihada zao akisema hatua hiyo inaleta faraja kwa Serikali.

Pia, Balozi Idd alitembelea uwanja wa michezo wa Gombani kuangalia ujenzi unavyoendelea.

Uwanja huo unatarajiwa kutumika katika kilele cha sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.