Umeme wang’oa vigogo wawili

Muktasari:

Wastani wa dakika 30 ambazo umeme umekuwa ukikatika kwa mujibu wa Waziri Merdard Kalemani

Dodoma. Kukatikakatika kwa umeme katika siku za karibuni kumeondoka na vigogo wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao Serikali imeagiza wasimamishwe mara moja.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amefikia uamuzi huo akiiagiza bodi ya shirika hilo kuchukua hatua hiyo mara moja dhidi ya naibu mkurugenzi wa uzalishaji umeme na naibu mkurugenzi wa usambazaji kutokana na tatizo la gridi ya Taifa na kuisababishia hasara Serikali.

Dk Kalemani alitoa agizo hilo mjini hapa jana alipokutana na bodi hiyo kwenye kikao cha dharura kujadili tatizo la kukatika umeme mara kwa mara kunakosababishwa na gridi ya Taifa. Alisema kwa miezi miwili sasa gridi hiyo imetoka mara nne kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 14 na kulisababisha Taifa kuwa gizani kwa muda wa nusu saa, kitendo ambacho ni hatari kwa usalama wa nchi ikizingatiwa kuwa kuna ziada ya umeme wa megawati 252.

Kutoka kwa gridi ya Taifa, kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya umeme, Ernest Anord ni kukatika kwa umeme katika mfumo huo na kusababisha mikoa yote iliyounganishwa kukosa nishati hiyo.

Dk Kalemani alisema gridi ya Taifa ilitoka Novemba 28 na 30, Desemba 4 na 14, na mara zote umeme ulikatika kwa wastani wa dakika 30.

Alisema nchi inapokuwa gizani hata kwa sekunde moja maana yake ni kuwa hakuna usalama na akatoa maelekezo kwa bodi hiyo kuchukua hatua kuanzia jana ili kuhakikisha kinachosemwa gridi kutoka hakitokei na kusababisha Taifa zima au sehemu ya nchi kukosa umeme.

“Lazima kuchukua hatua mahsusi kuhakikisha hilo halijitokezi, mwenyekiti unda timu mahsusi kuanzia leo (jana) ya kuchunguza na kufuatilia jambo hilo kwa kushirikisha tasnia na taasisi mbalimbali siyo Tanesco pekee, ndani ya siku saba nipate matokeo ya nini chanzo cha tatizo hilo ili lisijirudie,” alisema.

Waziri huyo alisema, “Jambo hili linapotokea ina maana kuwa kuna uzembe katika usimamizi ama kutofuatilia maagizo ya Serikali au kunaweza kuwa na hujuma katika baadhi ya watumishi wasiokuwa wazalendo, kwa hiyo kuanzia sasa bodi ichukue hatua dhidi ya naibu mkurugenzi wa generation (uzalishaji) na naibu mkurugenzi wa transmission (usambazaji), ichukue hatua za kiutawala ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa zao kuanzia leo.”

Alisema hatua hiyo inatokana na uzembe au kutochukua hatua ama kutowawajibisha watu walio chini yao kwa kuwa jambo hilo limejitokeza mara nyingi.

Pia, Dk Kalemani aliagiza wateja wote wa Tanesco waliolipia fedha za kuunganishiwa umeme miezi miwili hadi mitatu iliyopita wawe wameunganishwa ifikapo Desemba 31. “Na matengenezo (ya umeme) yanapofanyika wananchi wapewe taarifa wa muda umeme unaporudi,” alisema.