Upelelezi kesi ya Zitto wakamilika, kusomewa maelezo Desemba 13

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Desemba 13, 2018, kumsomea maelezo ya awali (PH), Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe anayekabiliwa na kesi ya uchochezi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imepanga Desemba 13, 2018, kumsomea maelezo ya awali (PH), Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  Zitto Kabwe anayekabiliwa na kesi ya uchochezi.

Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327 ya mwaka 2018, iliyopo mahakamani hapo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Novemba 26, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi, baada ya upande ya mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Mutalemwa Kishenyi amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekwisha kamilika.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tunaomba kuiarifu Mahakama hii tukufu kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya awali (PH)," amedai Kishenyi.

Kishenyi baada ya kueleza hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na Peter Kibatala umedai hauna pingamizi juu ya tarehe hiyo.

Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya Zitto kusomewa maelezo ya awali na mshtakiwa yupo nje ya kwa dhamana.

Zitto alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Novemba 2, Mwaka huu na kujibu mashtaka yanayomkabili.

Katika kesi ya msingi,  Zito anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za  makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Alitoa maneno ya uchochezi kuwa "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua"

Inadaiwa  maneno hayo yalikuwa ni maneno ya uchochezi na yenye kuleta hisia za hofu na chuki.

Katika shtaka la pili, Zitto anadaiwa  kuwa oktoba 28, 2018 huko Kijitonyama wilaya ya Kinondoni  katika mkutano huo na wanahabari, mshtakiwa alitoa maneno ya uchochezi yafuatayo "lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa, na jeshi la polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro wamekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi...kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua na si kuwaua, wananchi wengine wamekufa"

Wakili huyo alida maneno hayo pia ni ya uchochezi na yenye kuleta hofu.

Katika shtaka la tatu, mshtakiwa huyo siku hiyo katika mkutano huohuo alitoa waraka kwa umma ukiwa na maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya polisi.

Zitto alitoa waraka huo wenye maneno yafuatayo "Tumekuwa  tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza...tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupingwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi..:"

Upande wa mashtaka uliendelea kudai kuwa maneno hayo ni ya  kichochezi yenye kujenga chuki kwa Watanzania dhidi ya jeshi la polisi.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Zitto alikana kutenda makosa hayo.

Soma zaidi: