Upinzani: Mswada wa vyama umejaa makosa ya jinai

Muktasari:

  • Vyama tisa vya upinzani nchini vimekutana na kutoa tamko kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa. Viongozi wa vyama hivyo wamesaini makubaliano wakipinga muswada huo wakidai unalenga kuvikandamiza vyama vyao.

Dar es Salaam. Vyama vya upinzani nchini vimetoa tamko kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa uliowasilishwa bungeni Novemba 16, vikidai kwamba muswada huo una lengo la kuua upinzani nchini.

Vyama tisa vya upinzani vimekutana leo Disemba 9 jijini Dar es Salaam na kutoa msimamo wa pamoja. Vyama hivyo ni ACT Wazalendo, ADC, CUF, UPDP, DP, CCK, Chaumma, Chadema na NCCR Mageuzi.

Akisoma tamko la vyama hivyo, mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe amesema wanapinga sheria hiyo kwa sababu inakiuka haki ya kikatiba ya uhuru wa watu kukusanyika kwenye shughuli za kisiasa.

Amesema muswada huo umejaa makosa ya jinai ambayo yanatishia uwepo wa vyama hivyo na Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa mamlaka makubwa ikiwemo kumvua uanachama mtu yoyote kwenye chama cha siasa.

"Kwenye muswada huu,  msajili wa vyama vya siasa amejipa mamlaka makubwa ambayo yanaingilia uhuru wa vyama, kwa Msajili anaweza kumfukuza mwanachama wa chama chochote cha siasa. Msajili sasa amekuwa mdhibiti wa vyama vya siasa na siyo mlezi," amesema Rungwe.

Rungwe amesema maoni yaliyotolewa na vyama vya siasa kuhusu muswada huo hayajaingizwa kwenye muswada huo, jambo linalowafanya wadhani kwamba hizo ni njama za serikali kutaka kuua vyama vya upinzani.

Akifafanua yaliyomo kwenye muswada huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kifungu cha 5 (a) kwenye muswada huo unaeleza kwamba Msajili wa vyama anatakiwa kupata taarifa na kutoa kibali cha mafunzo kwa viongozi wa chama.

Amesema kifungu kingine cha 5 (d) nacho kinasema msajili anaweza kuhitaji taarifa zozote za chama cha siasa kutoka kwa mwanachama yoyote.

"Huu ni utaratibu gani jamani, si bora wangesema apate taarifa kutoka kwa viongozi. Watapandikiza watu wao kwenye vyama na kutumia taarifa zao kuviadhibu vyama vya siasa," amesema Mwalimu.

Amesema sura ya 18 inaeleza kwamba chama cha siasa kikipata hati chafu kwenye ukaguzi wa hesabu zake basi ruzuku yake itazuiliwa kwa kipindi cha miezi sita. Amesema kifungu hicho kina lengo la kuviadhibu vyama vya siasa kwa kuvinyima fedha kwa ajili ya kujiendesha.