Upinzani wakwama kusoma hotuba yao bungeni

Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshindwa kusoma maoni yake kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Fedha Ndogo ya mwaka 2018 baada ya kushindwa kuiwasilisha mezani asubuhi.

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshindwa kusoma maoni yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma ya Fedha Ndogo baada ya kushindwa kuweka mezani asubuhi wakati Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango alipowasilisha.

Asubuhi leo wabunge wa upinzani walitoka bungeni wakati walipokuwa wakiapishwa, Pauline Gekul (Babati Mjini), James Ole Millya (Simanjiro), Chacha Marwa (Serengeti) na Joseph Makundi (Ukerewe).

Wabunge hao walichelewa kuingia bungeni wakati, Dk Mpango na Kamati ya Bunge ya Bajeti walipoitwa na Spika Job Ndugai kwa ajili ya kuweka hotuba zao mezani.

Hata hivyo, baada ya hotuba ya kamati ya Bunge ya bajeti, Spika Ndugai alimuita mchangiaji wa kwanza badala ya msemaji wa kambi hiyo hali iliyosababisha Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kumuomba Spika kutumia busara zake wasome hotuba yao kwa sababu wakati wanaitwa walikuwa katika kikao kidogo.

Ombi hilo lilikataliwa na Spika Ndugai ambaye alisema wanafuata kanuni za Bunge zinavyosema.