Uuzaji hisa za Bharti Airtel soko la London njiapanda

Muktasari:

Serikali imepinga uwekezaji wowote utakaofanywa ndani ya Airtel Tanzania kutokana na mpango wa Airtel Africa kuuza hisa zake za awali (IPO) katika Soko la Hisa London (LSE) hadi mazungumzo yanayoendelea yatakapokamilika

Dodoma. Kufuatia kampuni ya Bharti Airtel kukaribisha wanahisa wapya kwa kuuza hisa zake za awali (IPO) kwenye Soko la Hisa la London (LSE) nchini Uingereza, Serikali imesema haiutambui mpango huo.

Wiki iliyopita, kampuni hiyo ilitoa taarifa yake kuhusu kuwakaribisha wawekezaji wa kimataifa walionunua hisa za Dola 1.25 bilioni za Marekani katika mpango wa Airtel Africa, ili kutafuta Dola 4.4 bilioni zitakazosaidia kuimarisha uendeshaji wake kwenye nchi 14 za Afrika na kulipa deni lake linalofika Dola 5 bilioni.

Akizungumza na wanahabari jana, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema kilichofanywa na kampuni hiyo ni batili nchini Tanzania. “Tunaamini kampuni ya Bharti Airtel itafuata utaratibu wa kumshirikisha mbia mwenza ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mchakato mzima wa kuwakaribisha wanahisa wapya,” alisema Mbuttuka.

Bharti Airtel, kampuni kubwa ya mawasiliano inayoshika nafasi ya sita duniani yenye makao makuu nchini India, ndiye mmiliki wa Airtel Tanzania inayotoa huduma nchini.

Kwa siku za karibuni, Airtel Tanzania imekuwa na mgogoro wa umiliki wa hisa zake kati ya wabia wawili wakubwa; Tanzania na Bharti Airtel.

Mbuttuka alisema kwa kuwa Airtel Tanzania inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Bharti Airtel, uamuzi wowote wa uuzaji na uhamishaji hisa au ukaribishaji wanahisa wapya unapaswa kuishirikisha Serikali.

Serikali na Airtel Tanzania zinaendelea na mazungumzo kupata mwafaka wa umiliki wa kampuni hiyo na uendeshaji wake.

Katika hatua za awali za kukamilisha IPO inayotarajiwa kufanyika Septemba mwakani, tayari Airtel Africa imewapata wawekezaji sita wa kimataifa wakiwamo Warburg Pincus, Temasek, Singtel, Soft Bank Group International na wengine.