VIDEO: Kupata hati ya kiwanja sasa kwa Sh150,000 tu

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, William Lukuvi ameshusha tozo ya upatikanaji wa hati ya ardhi kutosha Sh250,000 hadi Sh150,000  huku akizindua utoaji leseni za makazi zinazotolewa kwa Sh5,000.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameshusha tozo ya kupima na kurasimisha makazi na hatimaye kupata hati ya kiwanja kutoka Sh250,000 hadi 150,000 ili kuwawezesha wananchi wengi kupata hati hizo ili walipe kodi ya ardhi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 17, 2019 jijini Dar es Salaam, Waziri Lukuvi amesema wali bei hiyo ilikuwa Sh500,000 ikashushwa hadi Sh250,000 na sasa imeshushwa tena hadi Sh150,000 ambayo itahusisha mchakato wa kupima na kurasimisha makazi.

“Zoezi la urasimishaji gharama zake ni kubwa mno, wananchi wanashindwa kulipa Sh250,000. Zilikuwa Sh500,000 nikashusha lakini bado. Kuanzia leo gharama za kupanga, kupima mpaka kutayarisha jedwali akalipie hati ifikie Sh150,000,” amesema Waziri Lukuvi.

Amesema lengo la Serikali ni kutoa hati 500,000 ndani ya miezi mitatu ambao watalipa kodi ya Sh24 bilioni.

Mbali na utoaji wa hati, Waziri Lukuvi amesema kuna utoaji  leseni za makazi ambazo zinalipiwa Sh5,000 ambazo hudumu kwa miaka mitano.

“Nimezindua programu ya kutoa leseni kwa Dar es Salaam. Tangu nimezindua mwezi mmoja wamefikia watu 60,000. Tunataka mwenye leseni awe anajua mipaka yake na mamlaka za serikali za mitaa zitambue nani anaishi wapi.

“Tumejipambanua Serikali ya awamu ya tano kuwa ni Serikali ya wanyonge. Hawa squatters (makazi holela) hawakuwa na uwezo wa kununua viwanja mlivyopima,” amesema.

Amezitaka kampuni za urasimishaji na upimaji viwanja kufuata mwongozo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha data wanazokusanya zinafanana na za wizara.

Amewapa muda baadhi ya watumishi wa wizara hiyo wenye kampuni za upimaji na urasimishaji makazi kujitafakari kama wanataka kuendelea na kazi pamoja Serikali au la.