VITA YA KAGERA: JWTZ yazingira miji ya Kampala na Entebbe, yasubiri amri ya kushambulia-17

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi alivyompa Rais Julius Nyerere uhalali wa kuingiza jeshi lake mjini Kampala baada ya Majeshi ya Libya kupigana kumsaidia Iddi Amin. Hata hivyo, baada ya askari wa Tanzania kuizingira miji ya Entebbe na Kampala—hususan katika eneo la Mpigi, Nyerere alitoa amri kwa JWTZ kusubiri kwanza mpaka hapo watakapopewa amri ya kufanya hivyo.

BAADA ya mapigano ya Lukaya, eneo la katikati ya Lukaya na Kampala lilikuwa na wapiganaji wengi wa Iddi Amin na Libya waliokuwa wakikimbia. Ndege tatu zilizobeba askari wa Libya waliojeruhiwa ziliondoka mjini Entebbe kwenda Tripoli, Libya.

Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wanasonga mbele kuelekea mji wa Kampala walipofika eneo la Buwama walikuta basi la abiria lililokwama njiani na walipochunguza, wakagundua kuwa ‘abiria’ hao ni askari wa Iddi Amin waliokuwa wanakimbia. JWTZ hawakulipua basi hilo, lakini waliwaua askari 20 wa Amin waliojaribu kuwatoroka.

Katika eneo la Mtola Maria, kwa mujibu wa ‘War in Uganda’, askari wa Tanzania walikuta kanisa na shule, wakaona ni heri wapumzike. Ndani ya kanisa hilo mlikuwa na kinanda. Askari mmoja wa JWTZ aliyekuwa amechoka na kuchafuka sana matope alikitumia kinanda hicho kupiga Wimbo wa Taifa, “Mungu Ibariki Afrika.”

Kituo kilichofuata kilikuwa ni Mpigi, kiasi cha kilomita 32 kufika mji wa Kampala. Taarifa za kiintelijesia ziliifikia JWTZ kwamba askari wa Amin waliokuwa wamejiimarisha sana walikuwa wamejichimbia katika eneo hilo.

Kwa kuweka mikakati sawa, Jenerali Msuguri aliamua kuwa brigedi mbili—207 na 208—ziende moja kwa moja Mpigi. Msuguri alipanga Brigedi ya 201 ifagie njia kuelekea upande wa Magharibi kudhibiti barabara na reli inayotoka Kampala kuelekea mji wa Fort Port ulioko Magharibi mwa Uganda.

Brigedi ya 201 ilipoanza kufagia njia, ilikutana na shamba la kahawa karibu na Mityana ambako askari wengine wa Libya walikuwa wameweka kambi yao. Kabla askari wa Libya hawajajua kinachotokea, askari wa JTWZ wakawashambulia kama radi. Ndani ya dakika chache askari zaidi ya 30 wa Libya wakawa wameuawa.

Baada ya hapo askari wa JWTZ wakaendelea kusonga mbele. Lakini wakakabiliwa na changamoto nyingine. Kwa sehemu kubwa ya barabara, askari wa Tanzania walikuwa wakitembea kwenye matope kiasi cha mabuti yao kuzama kabisa na walikuwa wamelowa chapachapa kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha mfululizo.

Kadiri walivyokuwa wakisonga mbele, ndivyo walivyokuwa wakikutana na vikundi vya askari wa Iddi Amin. Sasa kwao ilikuwa ni kuua tu askari wa Amin kadiri walivyokutana nao. Waliendelea pia kuteka vifaru, mizinga midogo na mikubwa, magari mbalimbali ya kijeshi, hususan Land Rover na mabasi ya jeshi, ilimradi walinyakua chochote cha Majeshi ya Amin walichokitia machoni.

Kupitia darubini za kijeshi, JWTZ waliona gari aina ya Mercedes Benz ikiingia Mpigi na baadaye kusimama eneo hilo. Askari wa Tanzania wakajua huyo alikuwa Iddi Amin amefika eneo hilo akiwa katika gari hilo.

Baadaye askari wa Tanzania wakawa na hakika kuwa huyo alikuwa ni Iddi Amin kwa sababu baadaye siku hiyo, Redio Uganda ilitangaza kuwa Rais wa Uganda alikuwa anahutubia mkutano wa hadhara eneo la Mpigi.

Hata baada ya kujua kuwa aliyefika eneo hilo ni Iddi Amin na kwamba wangeweza kumtia mikononi, askari wa Tanzania waliamua wasimfanye chochote. Walimwacha hadi alipomaliza kuhutubia akajiondokea zake.

Makamanda wa JWTZ waliokuwa mstari wa mbele walikubaliana kuwa wasimuue hata kama fursa ya kufanya hivyo ingepatikana.

Sababu ya uamuzi huo ni kwamba ikiwa Amin angeuawa, huenda nafasi yake ingechukuliwa na mtu mwingine na hivyo kuwanyima askari wa Tanzania fursa ya kuishuhudia Kampala ikiangukia mikononi mwa Tanzania.

Hatimaye askari wa Tanzania walipoingia Mpigi, walikuta mji huo mdogo ukiwa tayari umekimbiwa na watu na uporaji ulikuwa wa kiwango cha juu. Askari wa Amin walichukua chochote walichoweza kubeba na kisha kukimbilia Kampala.

Sasa Iddi Amin alikuwa katika hali ngumu kuliko wakati mwingine wowote tangu alipoipindua Serikali ya Dk Milton Obote miaka minane iliyopita.

Mawasiliano ya barabara na reli kutoka Kampala kwenda Fort Port sasa yakawa tayari yameshakatwa. Njia pekee ya kutoka Kampala kwenda Fort Port ikabaki kuwa ni helikopta, lakini marubani wengi wa jeshi la anga la Uganda nao tayari walikuwa wameshakimbia kazini.

Kutoka sehemu zilizoinuka za Mpigi, sasa askari wa Tanzania wangeweza kuishambulia kwa urahisi Entebbe na Kampala.

Jeshi la Uganda sasa lilikuwa limeshachanganyikiwa huku wapiganaji na maofisa wake wakiwa katika hali ya hofu kubwa iliyowasababisha kukimbia ovyo huku na huko.

Kama ni mchezo wa karata, basi Iddi Amin alitumia vibaya karata alizopewa na rafiki yake, Muammar Gaddafi wa Libya.

Rais Nyerere, akizungumzia tishio la Gaddafi la kumuondoa Uganda, alisema“…Pamoja na kwamba (Libya) wanaongeza uzito katika vita, hawawezi kubadilisha msimamo wa Tanzania. Amin atabaki yuleyule mshenzi, muuaji, haaminiki... Ila sasa najua atavimba kichwa zaidi kwa kujua kwamba ana nguvu na nchi tajiri nyuma yake. Na nguvu hiyo sasa imetamkwa rasmi. Si ya kifichoficho tena. Amin atavimba kichwa zaidi.”

Miji mikubwa ya Uganda ambayo sasa ilikuwa imewekwa kwenye shabaha ya kutekwa ilikuwa ni Entebbe na Kampala.

Kwa wakati huo, Iddi Amin alikuwa mjini Kampala akiwahimiza makamanda wa jeshi lake waendelee kupigana vita ambayo wao walijua walielekea kabisa kushindwa.

Ingawa askari wa Libya na wale wa Amin walikuwa wanakimbia vita, bado aliamini tofauti, kwamba atafaulu kuwarudisha nyuma wapiganaji wa Tanzania na kisha kuirudisha ardhi yote ya Uganda kwenye himaya yake.

Sasa askari wa Tanzania walikuwa wameizingira miji ya Kampala na Entebbe, hususan eneo la juu la Mpigi, wakisubiri amri ya kushambulia. Lakini wakiwa wamejiandaa kufanya hivyo, Rais Nyerere alituma neno la kuwaambia wasishambulie kwanza miji hiyo hadi watakapoelekezwa vinginevyo.

Je, kwa nini Mwalimu Nyerere aliwazuia kwanza askari wake kuishambulia na kuiteka miji ya Kampala na Entebbe wakati tayari walikuwa wameshaizingira?

Soma zaidi: VITA VYA KAGERA : Utekaji wa kwanza wa ndege kielektroniki duniani wafanywa na Jeshi la Wananchi-16

Itaendelea kesho