Vilio vilivyotawala wakulima wa mazao wakililia bei nzuri sokoni

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akitazama ubanguaji wa korosho unavyofanyika wakati alipotembelea kiwanda cha Terra Cashew cha Kibaha kwa Mathias mkoa wa Pwani.Picha na Maktaba

Muktasari:

Wakati kukiwa na ahadi ya Serikali kuwa muhongo ungeuzwa kwa bei nzuri, zao hilo halikufanya vizuri sokoni, ingawa kwa sasa kuna juhudi za ujenzi wa kiwanda cha muhogo wilayani Handeni mkoani Tanga.

Dar es Salaam. Mwaka 2018 utakumbukwa na wakulima pamoja na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo kufuatia kuporomoka kwa bei ya mazao ya chakula na biashara katika masoko ya ndani na nje.

Kuporomoka kwa bei za mazao kuliziathiri pia serikali za vijiji, wilaya na mikoa kwa kukosa fursa ya kukusanya ushuru wa mazao, hivyo kuvuruga mipango na bajeti zao za maendeleo.

Pigo la kwanza lilianza kuwapata wakulima wa mbaazi ambao walianza kujitayarisha tangu mwaka 2017 baada ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kuitembelea Tanzania, Julai 2016 na kuahidi kununua zao hilo kwa bei nzuri.

Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla baada ya India ambayo hununua zaidi ya asilimia 90 ya mbaazi kutoka Tanzania kuweka zuio la kununua zao hilo kwa sababu za kimkataba.

Kutokana na katazo hilo, bei ya mbaazi ilishuka ghafla kutoka kati ya Sh2,500 na 4,000 kwa kilo hadi Sh100 na 200 na kuibua vilio kutoka kwa wakulima.

Zuio hilo lilisababisha tani zaidi ya 200,000 zenye thamani ya zaidi ya Sh27 bilioni kudoda. Hilo lilitokea wakati mavuno yakiongezeka na kufikia karibu tani 300,000.

Kilimo cha mbaazi nchini huingiza kwenye mzunguko wa biashara zaidi ya Sh500 bilioni kwa mwaka na huajiri moja kwa moja maelfu ya wakulima.

Wakulima wa mahindi walia

Kuporomoka kwa bei za mazao kumekuwa pigo kubwa kwa wakulima wa mahindi mwaka huu baada ya bei kushuka kutoka Sh100,000 kwa gunia la kilo 100 hadi kati ya Sh40,000 na Sh20,000.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), Tanzania huzalisha tani milioni 5.36 za mahindi kila mwaka. Ni zao la pili kuzalishwa kwa wingi baada ya muhogo.

Sababu zilizotajwa za anguko la bei ni pamoja na Serikali kufunga mipaka yake na kuzuia kupeleka mahindi nje ya nchi.

Sababu nyingine ilitajwa kuwa hatua ya Kenya ambayo ndio mteja mkubwa wa mahindi ya Tanzania kususa kununua baada ya kukataliwa mwaka jana kununua mahindi hayo wakati nchi hiyo ikiwa na ukame mkali.

Serikali ilikataa kuuza mahindi hayo kwa kwa kigezo cha upungufu wa chakula. Baada ya hapo Kenya waliamua kuagiza mahindi kutoka Zambia na Mexico.

Kuporomoka kwa bei ya mahindi kulihusishwa pia na madai ya kuingizwa kwa wingi nchini kwa mahindi kutoka Zambia.

Hivi karibuni kumekuwapo na matumaini ya kupatikana kwa soko la mahindi baada ya Ubalozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kusema kuna mahitaji ya zao hilo katika majimbo ya Haut, Katanga na Tanganyika nchini humo.

Mwakilishi Mkazi wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki (EACG), Ikunda Terry ameliambia Mwananchi kwa simu kuwa walishapeleka wafanyabiashara nchini DRC na Rwanda na kusaini mikataba ya ununuzi wa mahindi.

Sakata la korosho

Tofauti na mwaka jana ambapo wakulima wa korosho kilo moja waliuza hadi Sh4,000 wakati bei elekezi ilikuwa Sh1,500, mwaka huu mambo yamekuwa magumu baada ya bei ya soko la dunia kuporomoka kiasi cha wafanyabiashara kununua kwa bei za kati ya Sh2,700 na Sh3,000 kwa kilo.

Wakulima wengi walizigomea bei hizo. Wakati huo Serikali ilikwishafanya mabadiliko makubwa ikiwa pamoja na mabadiliko ya Sheria ya Korosho ya 2009 inayoipa nguvu ya kuchukua fedha za ushuru wa kusafirisha nje ya nchi zao hilo kwa asilimia 100.

Baada ya mambo kuendelea kusuasua na wakulima kususia minada ya korosho, Rais John Magufuli aliingilia kati na kutangaza kuwaunga mkono.

Ghafla alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri kwa kumtimua aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na kumteua Japheth Hasunga, huku pia akimtoa aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na kumteua Joseph Kakunda.

Rais Magufuli akatangaza Serikali itanunua korosho yote mwaka huu kwa bei ya Sh3,300, na akalielekeza Jeshi la Wananchi (JWTZ) kusimamia na kusafirisha korosho kutoka vyama vya ushirika kwenda kwenye ubanguaji.

Hata hivyo, kumekuwapo na maoni tofauti kutoka kwa wadau kwa hatua hizo, ikiwa pamoja na agizo la Serikali kuwataka wauzaji wa korosho kuonyesha mashamba yao kabla ya kulipwa.

Kahawa yaondoka na mawaziri

Bei ya kahawa na urasimu wa kuipeleka kwenye mnada Moshi mkoani Kilimanjaro navyo viliongeza kero ya wakulima wa zao hilo.

Wakulima mkoani Kagera waliamua kusafirisha kahawa yao ghafi kwenda nchini Uganda kwa magendo walikodai kuiuza kwa Sh2,000 tofauti na bei ya Sh1,000 nchini.

Kuna wakati waliokuwa mawaziri; Dk Tizeba (Kilimo) na Mwijage (Viwanda na Biashara) ilibidi wakutane na Waziri wa Biashara na Ushirika wa Uganda, Fredrick Ngobi Gume kujadili suala hilo.

Oktoba 8, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa viongozi wa polisi mkoani Kagera ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya zao hilo wilayani Kyerwa pamoja na tuhuma nyingine.

Akizungumza wakati wa kuwaapisha mawaziri wapya wa Kilimo na Viwanda Novemba 12, Ikulu ya Dar es Salaam, Rais alibainisha sababu ya kuwatumbua kuwa ni kushindwa kusimamia vyema soko la kahawa hadi alipomtuma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani humo.

“Kulipokuwa na shida ya bei ya kahawa mkoani Kagera ilibidi Waziri Mkuu aende akalimaliza ndani ya muda mfupi. Sasa najiuliza Mwijage hakuliona hili na yupo karibu,” alisema Rais Magufuli.

Tumbaku moto

Zao la tumbaku lililotamba kwa muda mrefu kwa kushika nafasi ya pili kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni nalo halikuachwa salama na mporomoko wa bei kwenye soko la dunia.

Mkoa wa Tabora ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa zaidi ya asilimia 50 ya tumbaku yote inayozalishwa nchini ukifuatiwa na Shinyanga, Kagera, Geita, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Mara.

Kwa mujibu wa Bodi ya Tumbaku, mapato ya fedha za kigeni yanayotokana na kuuzwa tumbaku nje yaliongezeka kutoka Dola 302.8 milioni (zaidi ya Sh694 bilioni) mwaka 2011 hadi Dola 343.9 milioni (zaidi ya Sh791 bilioni) mwaka 2016/2017.

Makusanyo ya ushuru wa halmashauri za wilaya yaliongezeka kutoka Sh10.8 bilioni 2011/12 hadi Sh14.8 bilioni mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 37.

Hivi karibuni Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora limemuomba Rais Magufuli kuingilia kati kuporomoka kwa zao hilo kulikosababisha kampuni zinazonunua tumbaku kupunguza makisio ya uzalishaji kila mwaka.

Waliolima muhogo walia

Mamia ya wakazi katika mikoa ya Tanga na Pwani waliwekeza katika kilimo cha maelfu ya eka za muhogo baada ya kuahidiwa soko la uhakika hasa nchini China.

Kwa mfano, wakulima karibu kila kijiji kilichopo mkoani Tanga isipokuwa maeneo ya milima ya Usambara iliyopo wilaya za Korogwe, Lushoto na Mkinga waliamua kulima muhogo kwa wingi wakitarajia kunufaika kufuatia hamasa kubwa ya ahadi ya bei na soko la uhakika.

Viongozi wa Serikali na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali walihamasisha wakulima kulima muhogo kwa sababu wanunuzi kutoka nchini humo wanayo mahitaji mengi, lakini hamasa hiyo imegeuka msiba.

Awali, wakulima waliahidiwa kuuza kilo moja kwa Sh250 ambyo ni wastani wa Sh4 milioni kwa eka moja, lakini hadi sasa hakuna wanunuzi isipokuwa wachache wanaotaka kununua kwa Sh100 kwa kilo.