Wafanyakazi Dar waandamana kumpongeza Rais Magufuli

Muktasari:

  • Wafanyakazi jijini Dar es Salaam wameandamana leo Alhamisi kupongeza uamuzi wa Rais John Magufuli wa kusitisha kikokotoo kipya na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.

Dar es Salaam. Wafanyakazi jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Januari 03,2019 wameandamana kwa lengo la kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta kikokotoo kipya cha mifuko ya hifadhi za jamii na kurejesha cha zamani.

Maandamano hayo ambayo yameanzia ofisi za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Mnazi Mmoja jijini humo hadi viwanja vya Mnazi Mmoja wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kumpongeza Rais Magufuli, yamepokewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva.

Akizungumza na waandamanaji hao, Lyaviva ametoa rai kwa wafanyakazi wa umma nchini kufanya kazi kwa uadilifu na kuwahudumia wananchi bila upendeleo.

Aidha amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Amesema wapo baadhi ya watumishi wa Serikali wanaochelewesha huduma kwa wananchi kwa makusudi hali inayosababisha malalamiko.

“Zingatieni nidhamu ya utumishi na utendaji, bahati nzuri kila taasisi ina mfumo wake wa utendaji kazi zingatieni hiyo mifumo, furaha hii ya kikokotoo haimanishi mjisahau katika kuwahudumia wananchi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu tamko la Rais Magufuli la kusitisha kikokotoo walichokiita kandamizi amesema uamuzi huo uwe chachu ndani ya mioyo ya wafanyakazi hao kwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma zaidi.

Akisoma risala iliyoandaliwa na wafanyakazi hao, Katibu wa kamati za wanawake wa Tucta, Jenijely James amesema kikokotoo hicho kilichorejeshwa kina mafao bora katika sekta ya umma.

“Ni wazi kutokana na malipo duni ya mishahara kwa watumishi wa umma, wengi wao hawakuweza kujenga makazi bora wakati wa utumishi wao hivyo matarajio yao yote yalikuwa kwenye malipo ya mkupuo kwa kanuni bora za waliyojiunga  na hatukujiandaa kisaikolojia kuhusu kikokotoo kipya,” ameongeza.

Desema 28, 2018, Rais Magufuli alikutana na Tucta, viongozi wa Mamlaka  ya Usimamizi  wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii  (SSRA) na wadau wengine Ikulu jijini Dar es Salaam na kusitisha kikokotoo kipya na kurudisha cha zamani ambacho kitatumika hadi 2023.