Wakulima kahawa watupia lawama wasimamizi

Muktasari:

Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI), Aloyce Mdalavuma alisema kwa simu jana kuwa ili kupata bei nzuri ya kahawa ubora ni jambo la muhimu lakini ubora haupatikani bila kuimarisha utafiti.

Mbozi. Wakulima wa kahawa wilayani hapa mkoani Songwe wameeleza sababu za kushuka kwa bei ya zao hilo kutoka Sh4,000 mwaka jana hadi Sh2,800 kwa kilo mwaka huu, kuwa imetokana na kukosekana kwa ubora unaosababishwa na mamlaka zinazosimamia kutotimiza wajibu wake.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI), Aloyce Mdalavuma alisema kwa simu jana kuwa ili kupata bei nzuri ya kahawa ubora ni jambo la muhimu lakini ubora haupatikani bila kuimarisha utafiti.

Mdalavuma alisema kama ilivyo kwa mazao mengine, Serikali haina budi kuingiza nguvu zake katika utafiti ili iweze kubadilisha aina ya miche na kuachana na ya zamani.

Mkulima wa kijiji cha Itaka, Kenneth Rainford alisema kahawa imekosa usimamizi wa kutosha na wakulima wengi wana miche ya zamani inayoshambuliwa na magonjwa.

“Lengo la Serikali kuanzisha soko huria katika ununuzi ilikuwa kuleta ushindani wa bei lakini ajabu siku hizi wanunuzi wote wanakuja na bei moja,” alisema Rainford.

Naye Yangson Mwilenga alisema tatizo lingine ni ukosefu wa maji ya kumwagilia kahawa inapofika muda wa kuchanua hivyo husubiri mvua za vuli ambazo mara nyingi zimekuwa zikichelewa, hali ambayo inasababisha wakulima kushindwa kuboresha zao.