Wanafunzi 599,000 wachaguliwa kidato cha kwanza, 133,000 utata

Muktasari:

Mikoa ili-yofanikiwa kuchukua wanafunzi wake wote waliofaulu ni Dar es Salaam, Geita, Kili-manjaro, Mtwara, Morogoro, Mwanza, Ruvuma, Singida na Songwe.

Dar es Salaam. Asilimia 18.7 ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari, hawataweza kufanya hivyo mapema kutokana na uhaba wa madarasa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi)Selemani Jafo alisema jana.

Jafo alisema wakati wa kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari kuwa jumla ya wanafunzi 733, 103 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.

Lakini akasema ni wanafunzi 599,356 (asilimia 81.76) watakaoanza masomo mwezi Januari wakati wengine 133,747 (asilimia 18.7) waliofaulu wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Aliitaja mikoa yenye uhaba wa madarasa kuwa ni Arusha inayohitaji madarasa 18,719, Dodoma (5,991), Iringa (2,774), Kagera (14,046) na Kigoma (12,178).

Mingine ni Lindi (1,294), Mara (16,365), Mbeya (6,395), Pwani (4,731), Rukwa (49,300), Tabora (11,209), Tanga (5,400), Manyara (5,392), Shinyanga (6,271), Katavi (1,249), Njombe (3,172) na Simiyu (12,684).

Jafo ameiagiza mikoa hiyo kukamilisha ujenzi wa madarasa na kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga kidato cha kwanza kabla ya mwishoni mwa Februari.

Wakati huohuo, waziri huyo ametoa siku saba kwa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kumpa taarifa kuhusu mwenendo wa mradi wa stendi ya mabasi ya Mbezi Luis, kinyume na hapo, fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo zitaondolewa.

Jafo alisema fedha hizo Sh50.9 bilioni zitatumika kwa miradi kwenye halmashauri nyingine baada ya Serikali kutoridhishwa na mwenendo wa mradi huo.

Agizo hilo pia limeelekezwa kwa wilaya zilizopewa fedha za ujenzi wa hospitali za wilaya, lakini hazijaanza ujenzi, nazo amezipa kabla ya Desemba 19, vinginevyo zikishindwa fedha zitachukuliwa.

“Itakapofika Jumatano wiki ijayo wilaya yoyote itakayokuwa haijaanza mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na tayari imepewa fedha, zitachukuliwa na kupelekwa wilaya nyingine ambazo hazikupata fedha,” alisema.

Jafo alisema ujenzi katika hospitali hizo unatakiwa uwe umekamilika kwa asilimia 100 ifikapo Juni 30, mwakani.