Wanasiasa watumia mitandao ya kijamii kutoa salamu za mwaka mpya

Muktasari:

Wakati Watanzania wakiungana na wananchi duniani kote kusherehekea Mwaka Mpya, wanasiasa nchini Tanzania wameitumia mitandao ya kijamii kutoa salamu za mwaka mpya 2019.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba amesema waliomkosoa 2018 wamemkomaza na kumuelimisha.

Ametoa kauli hiyo leo Januari Mosi, 2019 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter ikiwa ni sehemu ya salamu za sikukuu ya mwaka mpya wa 2019.

 “Naomba tusameheane tulipokosea 2018 na ninashukuru Mwenyezi Mungu atujalie baraka zake sote tutimize malengo yetu mema katika 2019,” amesema Makamba.

Mbunge wa Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema  aliandika kuwa wakati nchi inapita katika wakati mgumu katika demokrasia na haki mwaka 2019 ni wa kuonyesha tofauti kati ya busara na uoga.

 “Tofauti ya mwaka na siku katika maisha haisababishwi na kalenda yake bali wanapaswa kuwa na fikra tofauti kwa mambo ya msingi yaliyoshindikana mwaka 2018,” amesema Lema.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema, “mimi na familia yangu, tunawatakia watanzania wote heri ya mwaka mpya 2019, ukawe mwaka wa baraka, upendo na furaha, mwaka wa mafanikio kadri Mungu atakavyokujalia,.”

Aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amewataka Watanzania wanapoanza mwaka 2019  kuwaombea watu wote waliotiwa nguvuni na walio mashakani.

“Mengi yametokea 2018 na miaka lukuki iliyotangulia, walio vizuizini mashauri yao yasikilizwe kwa haki na wakati na kutendewa haki ikiwa ni pamoja na kuwa huru,”  amesema Nyalandu.

“Walio wapole wa kunena wasije kunyamaza endapo macho na dhamira zao zitashuhudia uonevu miongoni mwa jamii wanayoishi. Wenye mamlaka wakaone fahari kwa kutenda haki na mashuhuda wa nyakati tuishio tusimame kama mashujaa.”