Waziri aagiza wanaopotosha takwimu kushughulikiwa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ametaka watu wanaotoa takwimu wa lengo la kupotosha jamii kuchukuliwa hatua kwa kuwa ni kosa kisheria

Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameitaka ofisi ya takwimu kuwashughulikia watu wanaotoa takwimu za kupotosha jamii.

Amesema wapo watu wenye nia ovu ambao  kwa maslahi yao au kwa kutumiwa wamekuwa wakitoa takwimu za uongo jambo ambalo ni kosa kisheria.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 22, 2018 wakati akifungua kongamano la takwimu Afrika mwaka 2018, huku akizigusia halmashauri kwamba zina kasoro katika utoaji wa takwimu  na kusababisha miradi kutekelezwa chini ya kiwango.

Amesema  miradi imetekelezwa lakini kutokana na kukosekana kwa takwimu sahihi imekuwa haikidhi mahitaji hivyo kuonesha upungufu haraka na hivyo kuitia hasara Serikali.

“Mradi unatekelezwa haijulikani umelenga watu wangapi na utakaa kwa muda gani. Hili tatizo ni changamoto kwenye Halmashauri zetu hasa kwenye miradi ya maendeleo,” amesema Dk Kijaji

Ameagiza ofisi ya takwimu kushirikiana na halmashauri kuwa na takwimu sahihi kwa ngazi zote ili mipango ya maendeleo iakisi hali halisi.

Amesema kumekuwa na upotoshaji wa takwimu unaofanywa na watu licha ya kuwa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na kanuni zake imeweka mwongozo.

Amesema kukosekana kwa kada ya takwimu kwenye muundo wa Serikali ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili kada hiyo hasa ngazi ya halmashauri.

Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amesema uamuzi wa kuridhia mkataba wa takwimu Afrika umekuja katika kipindi muhimu ambacho Tanzania inaongoza kamisheni ya takwimu Afrika.

Dk Chuwa amesema ofisi hiyo itaendelea na utaratibu wake wa kutoa miongozo mbalimbali ya ukusanyaji na usambazaji wa takwimu katika halmashauri ili kujenga mfumo imara wa ukusanyaji taarifa na kuwa na takwimu sahihi.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Takwimu rasmi zenye ubora kuimarisha uwazi, utawala bora na maendeleo jumuishi’.