Wenye baa waeleza machungu, furaha

Moja ya baa ambayo itafaidika na tangazo la kutofunga saa 6 usiku na kukesha iliyopo kinondoni jijini Dar es Salaam.Picha na Omari Fungo

Dar es salaam. Siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kueleza nia ya kurejesha utaratibu wa kufanya biashara kwa saa 24, mameneja wa baa mbalimbali katika jiji hilo wamepongeza, wakisema itasaidia kuongeza mapato na kurejesha kazini waliowapunguza kazi.

Makonda alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa wilaya, makatibu tawala na maofisa wa TRA wa mkoa huo kuhusu mkakati wa ukusanyaji mapato bila kuwabugudhi wafanyabiashara, akisema anaandaa utaratibu ili wafanye biashara kwa saa 24 wakiwamo wamiliki wa baa.

Jana katika maeneo mbalimbali ya starehe, Mwananchi ilizungumza na mameneja wenye vibali vya ukomo unaoishia saa 6:00 usiku na kueleza namna walivyoathirika tangu Makonda alipotangaza kuzuia kufanya biashara kwa saa 24.

Meneja Mkuu wa Rombo Green View Bar iliyopo Sinza Shekilango, John Masawe alisema baada ya zuio hilo alipunguza wafanyakazi kutoka 36 hadi 10 alionao sasa kutokana na mapato kupungua.

“Kama anataka kuruhusu naomba iwe kweli, isiwe maneno ya siasa tu kwa sababu mapato yalishuka kwa zaidi ya asilimia 60. Wakiruhusu kukesha itaongeza hata uzalishaji wa vilevi kwenye viwanda hata wao wameathirika, wakirejesha saa 24 nitawarudisha wahudumu niliowapunguza,” alisema.

Meneja Mkuu wa baa ya Uhuru Peak iliyopo Kinondoni Vijana, Deogratius Mtei alisema baada ya Makonda kuzuia kukesha mapato yake yalishuka kwa asilimia 60 huku akipunguza wahudumu 10 kati ya 22.

“Athari za zuio hilo hazikuangaliwa kwa umakini, kwa sababu kwanza ajira wanazotaka kuzitoa kwa wananchi zilipungua, mapato kwa Serikali yameshuka sana, mie niko tayari hata kulipia ulinzi wa polisi katika eneo langu la biashara ili nifanye biashara kwa saa 24,” alisema.

Meneja Mkuu wa Freeland Pub iliyopo Mabibo, Kichabe Miyenzi alisema kutokana na zuio hilo ameathirika kibiashara kwa zaidi ya asilimia 50 hatua iliyopelekea wahudumu wake wanane kuanza kuwalipa nusu siku ili kulinda ajira zao.

Meneja msaidizi wa Hongera baa iliyopo Bamaga ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake alisema suala hilo lisichukuliwe kisiasa na Serikali badala yake iruhusu ili kunusuru ajira.