Kocha Ubelgiji alizwa na Ufaransa

Muktasari:

Akiwa na huzuni Martinez alisema inauma sana kuona Ubelgiji iliyotawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa iking’oka huku Ufaransa iliyocheza kujilinda zaidi ikitinga fainali.

St. Petersburg, Russia. Hatimaye mabingwa wa Dunia 1998 Ufaransa jana walitinga fainali ya mwaka huu ya Kombe la Dunia kwa kuilaza Ubelgiji bao 1-0 katika nusu fainali iliyopigwa dimba la St. Petersburg, mjini Moscow.

Akizungumzia kipigo hicho Kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez, ameeleza masikitiko yake akisema kilichoiangusha timu hiyo iliyotawala mchezo kwa kipindi kirefu ni kutotumia nafasi.

Akiwa na huzuni Martinez alisema inauma sana kuona Ubelgiji iliyotawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa iking’oka huku Ufaransa iliyocheza kujilinda zaidi ikitinga fainali.

“Nadhani wachezaji wa Ubelgiji itabidi wajilaumu wenyewe kwa kuzichezea nafasi kadhaa walizozipata katika mchezo huu, bila shaka tulikua na nafasi nzuri zaidi ya ushindi lakini hatukuzitumia nafasi tulizozipata na siku zote unapochezea nafasi unaweza kuzijutia,” alisema.  

Alisema kila mara aliwakumbusha vijana wake kutofurahia kutawala mchezo bali walazimishe kupata mabao lakini hawakuzingatia wakiamini mabao yatapatikana kirahisi kama ilivyotokea katika mechi zilizopita.

Katika hatua nyingine ushindi huo umeifanya Ufaransa kuvunja rekodi waliyokuwa nayo Ubelgiji chini ya Kocha Roberto Martinez, ambao hawajapoteza mchezo hata mmoja kati ya michezo 24 mfululizo waliyocheza ikiwa ni rekodi ya juu mno kwa Taifa hilo.

Kocha Didier Deschamps, mmoja wa wachezaji walioipa Ufaransa ubingwa wa Dunia mwaka 1998, aliwapongeza vijana wake kwa kuing’oa timu ngumu ya Ubelgiji akisema walitekeleza maelekezo yake kwa kiwango kikubwa.

Bao lililowazamisha Ubelgiji hapo jana lilifungwa kwa kichwa na mlinzi Samuel Umtiti katika dakika ya 51, akiunganisha kona iliyochongwa na Antoine Griezmann.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo, wamefanya kazi kubwa kuizuia Ubelgiji, kwani ni timu imara sana inayocheza soka la kasi na wamekua wabunifu katika kufunga mabao,” alisema Deschamps.

Alijisifia kuwa hajali kulaumiwa kwa kuwaelekeza viungo wake N'golo Kante na Paul Pogba kurudi nyuma kuwasaidia walinzi kuimarisha ngome yao tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo.

Alidai kufurahia pia namna walivyowasaidia walinzi wao kumdhibiti nahodha wa Ubelgiji, Eden Hazard, ambaye katika fainali za mwaka huu ameonekana kuwa mchezaji hatari zaidi kwa wapinzani.

Hadi inafika fainali Ufaransa imeruhusu kufungwa mabao manne tu yakiwemo matatu kutoka kwa Argentina na moja dhidi ya Australia.

Alisema mbinu zao za kucheza kwa kujilinda zilikua na manufaa na kama sio umahiri wa kipa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois wangeweza kupata mabao mawili au matatu kutokana na mashambulizi machache ya kushtukiza waliyoyafanya kipindi cha kwanza.