Monday, July 17, 2017

Kona za Chongoleani zapunguzwa kwa ajili ya marais Museveni, JPM

 

By Burhani Yakub,Mwananchi; byakub@mwananchi.co.tz.

Tanga. Wakala wa Barabara (Tanroads) imelazimika kupunguza kona za barabara ya kuelekea Kata ya Chongoleani ili kurahisisha msafara wa marais John Magufuli na Yoweri Museveni watakaowasili hivi karibuni kuzindua mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Tanga, Alfred Ndumbaro alitoa taarifa hiyo leo Jumatatu Julai 17 alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa mradi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,403 kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga.

Marais hao wawili wa Tanzania na Uganda wanatarajiwa kufika Chongoleani mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Agosti.
Alisema Tanroads imelazimika kupunguza kona za barabara hiyo ambayo ilikuwa na urefu wa kilomita nane na sasa imefikia kilomita saba ili kurahisisha magari yatakayokuwa kwenye msafara wa marais hao.
“Tayari tushapunguza kona na kuipanua barabara na kuweka changarawe tumefanya hivyo ili kurahisisha msafara wa marais wetu lakini pia kuweka mazingira rahisi kwa wataalamu watakaoendesha mradi wa bomba la mafuta,”alisema Ndumbaro.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alisema  maandalizi ya kuwapokea marais hao kwa ajili ya uzinduzi wa mradi huo yameshakamilika .
“Maandalizi yote ya kuwapokea marais yashakamilika, wananchi wa Tanga wanawasubiri kwa shauku kubwa  kwani ni heshima kubwa mradi huo kuzinduliwa Chongoleani kwa sababu mradi huu ungeweza hata kuzinduliwa Uganda au sehemu yoyote litakakopita bomba hilo,” alisema Shigela.
Alisema kwa sasa timu ya wataalamu wa bomba hilo ipo katika mchakato wa kuainisha njia litakapopita kutoka  Hoima hadi Tanga ikiwa ni pamoja na kupima udongo utakahimili bomba hilo liwapo ardhini.
Hata hivyo wakazi wa Kata ya Chongoleani ambako bomba la mafutaghafi kutoka Uganda litaishia kabla kusafirishwa kwa njia ya meli, wamesema wamepokea mradi huo lakini watakuwa na furaha zaidi iwapo watalipwa  kwa haraka fidia ya mali na ardhi
iliyochukuliwa, kuhakikishiwa ulinzi pamoja na kuwekewa mazingira bora ya uvuvi wa kisasa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga alipozungumza na wakazi wa Chongoleani wiki iliyopita aliwahakikishia kuwa kila atakayeguswa na mradi huo, Serikali itahakikisha analipwa bila kupunjwa na kuwataka kufanya subira wakati mchakato wa kutathmini ukiendelea.
Ujenzi wa bomba hilo utagharimu Dola 4 Bilioni huku uwekezaji huo ukitarajiwa kutoa fursa za ajira kwa watu zaidi ya 10,000 wakati wa ujenzi na wengine wapatao 1,000 hadi 5,000 wakati wa kuendesha mradi.
Faida za mradi huo ni pamoja na fursa mbalimbali zikiwemo kuongeza wigo wa uwekezaji mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla ikiwamo ajira kwa Watanzania pamoja na ushiriki wa kampuni za Kitanzania.

-->