Korea Kaskazini, Kusini waandika historia

Muktasari:

  • Inaaminika kwamba hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kim kuzungumza ana kwa ana na maofisa kutoka Kusini tangu alipoingia madarakani mwaka 2011. 

Seoul, South Korea. Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameuambia ujumbe wa ngazi ya juu wa Serikali ya Korea Kusini kwamba, “anataka kuandika historia mpya ya kuunganisha taifa” katika kikao cha kihistoria cha pande mbili hizo kilichofanyika Jumatatu Pyongyang.

Shirika la habari la Korea Kaskazini lilitoa picha na maoni kutoka kwa Kim kwenye hafla ya chakula cha jioni na maofisa wa Korea Kusini akiwemo mkuu wa usalama wa taifa, Chung Eui-yong. 

Korea Kusini ilithibitisha kikao hicho, ambacho ilisema kilidumu kwa saa nne kuanzia saa 12:00 jioni Jumatatu na kilihudhuriwa pia na mkewe Kim Ri Sol Ju na dada yake Kim Yo Jong.

Inaaminika kwamba hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kim kuzungumza ana kwa ana na maofisa kutoka Kusini tangu alipoingia madarakani mwaka 2011.

Ilikuwa mara ya kwanza pia kwa msafara wa Korea Kusini kuingia kwenye jengo la Chama cha Wafanyakazi Korea, maofisa wa Korea Kusini wamesema.

Shirika la habari la Korea Kaskazini la KCNA lilielezea mkutano huo ulikuwa wa “mazungumzo ya moyo mkunjufu” juu ya masuala kadhaa yaliyolenga "kuboresha uhusiano na Korea Kusini na kuhakikisha utulivu katika rasi ya Korea.”

Ujumbe huo kutoka Korea Kusini uliwasilisha barua binafsi kutoka kwa Rais Moon Jae-in kwenda kwa Kim, KCNA lilisema.