Korti ya Ufisadi kuamua hatima ya majalada 106 ya makontena

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayotokana na utoroshaji wa makontena hayo, uliomba kuwasilisha mahakamani majadala hayo kupitia kwa shahidi wake wa kwanza, Ashrafu Khan, yapokewe kama vielelezo ya ushahidi.

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Ufisadi, leo inatarajia kutoa uamuzi wa kuyapokea au kutoyapokea majalada 106 yanayohusu makontena 329 yaliyotoroshwa katika Bandari Kavu ya Azam (AICD), bila kulipiwa kodi.

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayotokana na utoroshaji wa makontena hayo, uliomba kuwasilisha mahakamani majadala hayo kupitia kwa shahidi wake wa kwanza, Ashrafu Khan, yapokewe kama vielelezo ya ushahidi.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi Kung’e Wabeya na Nehemia Nkoko waliweka pingamizi dhidi ya shahidi huyo kuwa si mtu sahihi, hivyo hana mamlaka kisheria kuyawasilisha mahakamani majalada hayo kama vilelezo kwa kuwa si yeye aliyeyaandaa wala hayakuwa mikononi mwake.

Nkoko alipinga kuwa majalada hayo si sehemu ya nyaraka au vielelezo vilivyotajwa na upande wa mashtaka katika hatua ya ufungaji wa kesi hiyo katika mahakama ya chini.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Vitalis Peter aliiomba mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo akidai kuwa shahidi huyo ni sahihi kuwasilisha vielelezo hivyo, kwani hakuna kifungu cha sheria kinachoeleza kuwa kama shahidi si mtunzaji wa vielelezo hawezi kuviwasilisha maakamani.

Kuhusu hoja kwamba vielelezo hivyo havikutajwa katika hatua ya ufungaji na uhamishaji shauri hilo katika mahakama ya chini, Vitalis alidai yalitajwa kwa jina la jumla kama Azam custom clearence files na nakala zake mawakili hao walipewa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Winfrida Korosso anayesikiliza kesi hiyo aliahirisha kwa ajili ya kuandika uamuzi ambao alipanga kuutoa leo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Raymond Louis (39) ambaye ni meneja wa operesheni za ulinzi na usalama, AICD; Hamis Omary (48), mchambuzi mwandamizi wa masuala ya biashara TRA, Haroun Mpande (28) wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta (ICT), Khalid Yusuph Hassan na Benson Vitalis Malembo.