VIDEO:Kuichukua Airtel ni vita kubwa

Kuichukua Airtel ni vita kubwa

Muktasari:

Mgogoro wa umiliki wa kampuni ya Airtel unatokana na uamuzi wa wakurugenzi sita waliohudhuria kikao cha bodi ya TTCL kilichoketi Agosti 5, 2005 pamoja na wawakilishi wawili wa menejimenti ya kampuni hiyo.

Dar es Salaam. Wakati TTCL ikisema mchakato wa kuirudisha Airtel mikononi mwake utakuwa ni vita kubwa, kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa nyingi za kampuni hiyo ya simu za mkononi, imejitokeza na kusema, “Uwekezaji wetu ulifuata na kuzingatia sheria na taratibu kabla haujapata baraka zote za Serikali ya Tanzania.”

Jana, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Omary Nundu akiwa ameambatana na menejimenti ya shirika hilo alizungumza na vyombo vya habari na kusema: “Tunaenda vitani na tunajua hii ni vita kubwa.”

Mbali ya taasisi hizo mbili, mwandishi wetu alizungumza na aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya Airtel Tanzania, Jaji Joseph Warioba kuhusu mzozo huo wa hisa na kusema Serikali ndiyo inayopaswa kuulizwa juu ya suala hilo kwani ndiyo yenye mkataba.

Juzi, Rais John Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kufuatilia utata uliopo kwenye umiliki wa Airtel akisema kampuni hiyo ni mali ya Serikali.

Jaji Warioba aliyeiongoza bodi iliyovunja uhusiano uliokuwapo kati ya TTCL na kampuni ya Celtel na kuunda kampuni mbili tofauti alisema: “Hayo mambo iulizwe Serikali kwa sababu ndiyo ilikuwa na mkataba. Bodi haikutengeneza mkataba, ilichofanya ni kutekeleza makubaliano kati ya Serikali na Airtel.”

Mgogoro wa umiliki wa kampuni ya Airtel unatokana na uamuzi wa wakurugenzi sita waliohudhuria kikao cha bodi ya TTCL kilichoketi Agosti 5, 2005 pamoja na wawakilishi wawili wa menejimenti ya kampuni hiyo.

Akimwakilisha Jaji Warioba, kumbukumbu zilizopo ambazo Mwananchi imezithibitisha, zinaonyesha kiliongozwa na Omari Issa aliyekuwa mwenyekiti. Wajumbe wawili wa bodi hiyo walihudhuria ambao ni Yona Killagane na Agnes Bukuku huku Werner Ruessel akishiriki kwa njia ya masafa ya mtandao (teleconferencing).

Licha ya Jaji Warioba, wajumbe wengine wawili wa bodi hiyo walituma wawakilishi wao. Tito Alai aliwakilishwa na Moez Daya huku Edward Mwakyembe akizungumza kwa niaba ya Felix Mrema. Pamoja nao, alikuwapo aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TTCL, George Mbowe na mwanasheria wa kampuni, Gilder Kibola.

Nusu ya wajumbe wa bodi hiyo walioteuliwa kwa mujibu wa sheria wakishirikiana na wawakilishi wakurugenzi waliokuwa dharura, siku hiyo walipitisha uamuzi ambao miaka 12 baadaye umeishtua Serikali.

Kwa mujibu wa wajumbe hao, mustakabali wa TTCL uliandaliwa, na Jaji Warioba anasema mkataba uliojadiliwa ulikuwa kati ya Serikali na kampuni ya Airtel.

Kumbukumbu

Kikao hicho kilikuwa ni matunda ya uwekezaji uliofanywa mwaka 1998, TTCL ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya TTCL kwa asilimia zote.

Mtaji wa Dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Sh11 bilioni za sasa) uliwekezwa. Lakini, January 31, 2002 ikiendelea kuwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa Dola za Marekani 82 milioni (zaidi ya Sh180.4 bilioni) ili kukuza mtaji.

Wakati mkopo huo unachukuliwa, TTCL ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na kampuni ya Mobile System International Celluler Investments Tanzania (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa na asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.

Miaka mitatu baadaye, mwaka 2005 mabadiliko yalifanywa kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel na kuunda kampuni mbili tofauti, Celtel ikitenganishwa na TTCL.

Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba, 2007 iliuza hisa zake kwa Zain ambayo nayo baada ya miaka mitatu, iliziuza kwa Bharti Airtel, June 8, 2010.

Bodi mpya

Kukamilika kwa kikao hicho kulimaanisha kuvunjwa kwa bodi ya wakurugenzi na kuundwa kwa uongozi mpya utakaosimamia shughuli za Celtel.

Makubaliano yaliyoafikiwa yanaeleza kuwa wajumbe wapya walitangazwa na kuchukua majukumu ya menejimenti na ilipewa miezi sita, pamoja na mambo mengine, kupendekeza meneja atakayesimamia shughuli za kila siku za kampuni hiyo mpya ya mawasiliano nchini ya Celtel.

Kama mkataba ulivyokuwa unasema; Serikali ilimteua Agnes Bukuku, Profesa Mathew Luhanga, George Mbowe na Amina Salum Ali huku MSI ikimteua Jaji Warioba kutetea masilahi yake ndani ya kampuni hiyo.

Hata hivyo, Serikali haijaridhishwa na namna umiliki ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL kwani ilipewa hisa chache tofauti na ilivyostahili jambo linalomaanisha mbia mwenza aliyepo hivi sasa, Bharti Airtel, ndiye anayenufaika zaidi na uwekezaji uliofanywa.

TTCL

Msimamo wa shirika hilo la mawasiliano Tanzania kwa mujibu wa Nundu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano katika Serikali ya Awamu ya Nne ni kwamba hivi sasa hawahitaji tena mgao, bali wanataka Airtel irudishwe katika kampuni ya Serikali.

Kwa kutambua hadhi na weledi wa baadhi ya wajumbe walioshiriki kufanya uamuzi unaoonekana ulikiuka taratibu pamoja na ukubwa wa mbia mwenza, mwenyekiti huyo wa TTCL anaona mchakato wa kuzirudisha hisa hizo ni sawa na vita.

Ni vita ambayo Waziri Mpango atatakiwa kuandaa mazingira ya kuishinda baada ya kupewa agizo la kufuatilia umiliki huo na Rais Magufuli na kuhakikisha Airtel inarudi mikononi mwa Serikali.

Ili kuhakikisha kwamba vita hiyo inafanikiwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema menejimenti na wafanyakazi wa kampuni hiyo watatoa ushirikiano na ushahidi unaohitajika kuhakikisha Airtel inarudi mikononi mwao.

Alifafanua kwamba, endapo kampuni hiyo ingekuwa mikononi mwa TTCL tangu mwanzo, mpaka leo ingekuwa imetoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania kwa kutoa gawio serikalini, ajira kwa wananchi na kukuza mchango wa sekta ya mawasiliano nchini.

Akitoa mfano alisema, katika robo mwaka iliyoishia Septemba, TTCL ilipata faida ya Sh2.6 bilioni kabla na Sh1.8 bilioni baada ya kodi na mwishoni mwa mwaka huu wa fedha, inatarajia kutoa gawio la Sh1 bilioni kwa Serikali.

“Faida hiyo ni ya TTCL, tungekuwa pamoja na Airtel tungekuwa mbali kiuchumi,” alisema.

Kutokana na ushahidi aliosema kampuni yake inao, Kindamba aliitaka menejimenti ya Airtel kuirudisha Airtel mikononi mwa TCCL kwa kuwa upatikanaji wake haukuwa halali.

“Kampuni yoyote iliyoanzishwa kwa njia haramu haiwezi kuendelea kuwa halali. Tunataka wairudishe bila kukwaruzana na kama wanataka hivyo tutapita huko.

“Ila hatutaki tufike huko, Watanzania wajue. Tunaitaka kwa njia bora kampuni hii irudishwe,” alisema.

Juzi, akizindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema kwa taarifa alizonazo, Airtel ni mali ya Serikali chini ya umiliki wa TTCL.

“Palifanyika mchezo wa ovyo, sasa sitaki kuzungumza mengi, fuatilia hilo (Waziri wa Fedha, Dk Mpango). Nchi hii ilikuwa ya maajabu sana, unachukua share (hisa) leo, kesho inauzwa kwa Dola moja, maajabu,” alisema.

Elias Msuya, Raymond Kaminyoge na Bakari Kiango