Kujipiga picha za ‘selfie’ mara kwa mara ni maradhi mapya

Muktasari:

  • Utafiti huo umebaini kwamba matumizi ya mara kwa mara ya selfie yanafanywa na watu wasiojiamini na ugonjwa huo wa akili unaitwa selfitis.

 Je, unapenda kujipiga picha mnato au selfie mara kwa mara? Watafiti wa Chuo Kikuu cha Nottingham Trent, Uingereza na kile cha Thiagarajar cha India wamebaini kwamba kama unapiga picha zaidi ya tatu kwa siku na kuziweka katika mitandao ya kijamii, basi una dalili za ugonjwa wa akili.

Utafiti huo umebaini kwamba matumizi ya mara kwa mara ya selfie yanafanywa na watu wasiojiamini na ugonjwa huo wa akili unaitwa selfitis.

Picha za selfie zimepata umaarufu baada ya kupanuka kwa mitandao ya kijamii kama vile Facebook, WhatsApp, Instagram na twitter.

Kuanzia nyota wa Hollywood mpaka kwa watoa maamuzi duniani na viongozi wa dini, hakuna mwenye kinga dhidi ya selfie.

Hata Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama alijulikana kwa kujipiga picha akiwa na wanasiasa wenzake.

Donald Trump wa Marekani, Vladmir Putin wa Urusi na Uhuru Kenyata wa Kenya, wote hujipiga selfie.

Lakini, wasomi waliofanya tafiti juu ya kujipiga picha mnato mara kwa mara na kuziweka katika mitandao ya kijamii wamesema ni maradhi mapya ya kiakili.

Imebainika kuwa picha zao zisipopendwa mitandaoni au wakikosolewa huathirika hata baadhi yao wanaweza kujiua.

Utafiti huo umefanyika kwa kuwashirikisha watu 400 kutoka India kwa sababu nchi hiyo ina watumiaji wengi wa mtandao wa Facebook na Instagram.

Pia, nchi hiyo inaongoza kwa vifo vya watu wanaojipiga picha za selfie kwenye maeneo ya hatari.

Si India tu, imekuwa ni jambo la kawaida kwa Watanzania, wakiwamo wasanii na wanasiasa kujipiga picha na kuziweka katika mitandao ya kijamii.

Mara nyingi picha zao ni za kuonyesha sura au mavazi yao.

Hatua za maradhi ya selfitis

Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa kwenye jarida la kimataifa la Afya ya Akili na limethibitisha kwamba kuna hatua za ugonjwa huo wa selfitis.

Hatua ya kwanza ni wale wanaojipiga picha tatu kwa siku lakini hawaziweki kwenye mitandao ya kijamii.

Hatua ya pili ya selfitis ni wale wanaojipiga picha mara tatu kwa siku na kila picha wanaiweka kwenye kurasa za mitandao.

Kwa mujibu wa utafiti huo, hatua ya tatu ni wale wanaojipiga picha kila saa na wanaweza kuweka picha zaidi ya sita kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Watafiti hao wamebainisha kwamba kuna sababu sita zinazowafanya watu kupata maradhi ya selfitis.

“Sababu hizo ni pamoja na kutokujiamini, kutaka kutambulika uwepo wao na kufurahisha hisia zao,” ulisema utafiti huo

Ugonjwa huo ukifikia hatua ya tatu, basi mtu huyo huweza kupiga picha na kuzituma mitandaoni na zisipopendwa au ‘kupata likes’ mtu huathirika kisaikolojia hata kufikia kujiua. Au akikejeliwa basi huathirikia.

Sababu nyingine ni kujiunganisha na mazingira yanayowazunguka(kuweka kumbukumbu za matukio), kujiweka karibu na jamii zinazowazunguka na kutaka kushindana na watu wengine katika jamii zao.

Profesa wa Masuala ya Uraibu na Tabia kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham Trent, Idara ya Saikolojia, Mark Griffiths anasema, “Miaka michache iliyopita taarifa kwenye vyombo vya habari zilidai kwamba selfitis ni tatizo la akili. Baadaye taarifa hizo zilielezwa kwamba ni za uongo, lakini haikumaanisha kwamba hali ya selfitis haikuwepo, sasa tunathibitisha uwepo wake.”

Mtafiti mwenzake, Dk Janarthanan Balakrishna anasema; “Watu wenye hali hiyo hawajiamini na wanataka kuendana na wale wanaowazunguka na wanaweza kuonyesha dalili za uraibu (addiction) wa tabia zao.”

“Uwepo wa hali hiyo sasa umethibitishwa na cha muhimu ni nini cha kufanya kuwasaidia walioathirika zaidi,”alisema.

Msanii wa Tanzania, Zuwena Mohammed maarufu kama Shilole alieleza kwa nini anapenda kupiga picha na idadi ya picha kwa siku.

“Napiga picha zaidi ya tano kwa siku, kukiwa na kitu maalumu ninaweza kupiga zaidi ya 10 na zote nikazituma mtandaoni. “Siwezi kukaa mbali na simu yenye kamera, hata nikitaka kubadili sinunui kabla sijajiridhisha kuwa ina uwezo wa hali ya juu wa kupiga picha, ”alisema Shilole.

Msanii mwingine wa Bongo Movie, Shamsa Ford anasema anapenda kupiga picha kwa sababu ni kumbukumbu, lakini ndiyo kitu kilichopo kwa wakati huu.

“Napenda picha ninaweza kupiga sita au saba kwa siku kulingana na jinsi nilivyoamka na shughuli ninayofanya kwa siku hiyo, ”alisema Ford.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka taasisi ya Christom Solution, Charles Nduku anasema hali hiyo huanza kama mzaha baadaye hukua na kuwa tabia.

Alisema wakati mwingine mtu anakosa uwezo wa kuchagua wapi panafaa kupiga picha au kutopiga picha na mwisho wa siku inakuwa kero na usumbufu kwa watu alio karibu nao.

“Anaweza kupiga picha hizo bila kuwa na matumizi nazo bali kwa mapenzi yake tu anakuwa ameshaathirika na tabia hiyo,” alisema Nduku.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Hassan Mwinuka alisema kujiangalia sura na kujipiga picha mara kwa mara kunasababisha matatizo.

Alisema mtu anapoiona sura yake mara kwa mara kupitia picha yake, asipoifurahia anaweza kupata matatizo ya kisaikolojia.

Alisema watu wa aina hiyo kwenye nchi zilizoendelea huwa wanafanya upasuaji (plastic surgery)wa kubadili muonekano ili kutengeneza sura wanazozitaka.

“Tatizo linakua kwa mtu ambaye hana uwezo wa kufanya upasuaji wa kubadili sura ya uso wakati ana sura ambayo haridhishwi nayo,” alisema na kuongeza:

“Badala yake atakuwa anajipiga picha mara kwa mara kwa kubadilisha staili angalau apate sura inayovutia.”