LSF: Wengi hawajui namna ya kupata msaada wa kisheria

Muktasari:

LSF, imesema hatua hiyo imesababisha wananchi kuingia katika migogoro na vyombo vya Serikali.

Dar es Salaam. Mfuko wa Ruzuku wa Uwezeshaji Vituo vya Msaada wa Kisheria (LSF), umesema Watanzania wengi hawana uelewa wa haki zao pamoja na namna ya kupata msaada wa kisheria.

LSF, imesema hatua hiyo imesababisha wananchi kuingia katika migogoro na vyombo vya Serikali.

Imejata migogoro hiyo ni ile ya ardhi, kukandamizwa katika usawa na haki, uonevu na kufungwa bila makosa.

Hata hivyo LSF,  imesema Watanzania wana kila sababu ya kuhoji haki zao za msingi katika jamii bila vitisho.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Julai 26 na Mwezeshaji wa Mafunzo ya Msaada wa Kisheria, James Marenga wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari jiiini Dar es Salaam.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2015, LSF imefanikiwa kuwajengea uwezo na kuwasajili wasaidizi wa msaada wa kisheria 4500 katika mikoa 26 nchini.

"Watu hawajui wanachopaswa kujua kuhusu sheria, wengi wanaishi kiujanja ujanja, kwa wanaojua ni hatari sana kuingia mgogoro na sheria. Jamii inatakiwa kufahamu na kuzipata haki na sheria mbalimbali ili ziwasaidie katika maendeleo yao, mfano ni mtu kutumia Sh100milioni kujenga eneo lisiloruhusiwa kisheria," amesema Marenga.