Lema aonya matumizi ya siasa

Muktasari:

  • Aliyasema hayo Jana wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Kwa Mrombo wakati akiongea na wananchi mbalimbali waliohudhuria katika mkutano huo.

 Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema amewaasa viongozi wa dini kutoingilia siasa kwani kwa kufanya hivyo wanaondoa thamani halisi ya imani na mwisho wa siku watawagawa waumini wao.

Aliyasema hayo Jana wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Kwa Mrombo wakati akiongea na wananchi mbalimbali waliohudhuria katika mkutano huo.

Lema alisema kuwa, kumekuwepo na hali ya viongozi wengi wa dini kuingilia siasa badala ya kutekeleza wajibu wao hatua ambayo amewataka kuacha mara moja badala yake wafanye yale waliyoelekezwa kufanya na jamii na sio vinginevyo.

Alisema kuwa, hatua hiyo inapelekea kuondoa kabisa thamani ya imani na hata waumini kukosa imani nao kitendo ambacho Mwisho wa siku kinahatarisha Amani ,hivyo aliwataka kuachana na siasa na hivyo kutenda wajibu wao.

“Mimi nawashangaa viongozi wa dini wanaochanganya siasa na dini badala ya kufanya yale wanayotakiwa kufanya katika kuhakikisha kuwa wanahubiri amani na sio kuingilia siasa maana mwisho wa siku wanahatarisha maisha ya wananchi wao. “alisema Lema.

Aidha aliwataka wananchi kusimamia haki zao bila hofu yoyote na kuhakikisha wanatumia haki yao ya msingi kumchagua kiongozi wanayeona anafaa kuwatumikia.

Naye Mgombea udiwani wa Kata hiyo, Simon Mosses aliwataka wananchi kumchagua yeye ili aweze kupeperusha bendera ya chama hicho ndani ya Kata hiyo na kuweza kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi hao .

Simon aliwaahidi wananchi hao kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ya maji ambayo ndiyo imekuwa sugu katika Kata hiyo sambamba na kushughulikia swala la umeme ili kila mwananchi aweze kuwa na umeme.