Lindo lilivyomuokoa na mauti Jonathan Kalambwia

Jonathan Kalambwia akiwa na watoto wake walionusurika katika tukio la mti kuangukia nyumba yake na kuua watoto wake watano. Kutoka kulia ni Charles, Zakayo na Josephat Jonathan. Picha na Moses Mashalla

Arusha, Mei 10 ni siku ambayo Jonathan Kalambwia, mkazi wa kijiji cha Ngiresi, kata ya Sokon 11 wilayani Arumeru mkoani hapa hataisahau kamwe katika maisha yake baada ya kupoteza watoto wake watano ambao ni marehemu Glory Jonathan (11), Miriam Jonathan (16), Best Jonathan (20) Jofrey Jonathan (31) pamoja na Lazaro Lamyamki (26).

Tukio hilo lilitokea baada ya mti mkubwa wa asili kuserereka takriban umbali wa mita 200 ukiwa umesimama kabla ya kuangukia nyumba ambayo familia yake ilikuwa imelala ndani yake.

Hata hivyo katika tukio hilo watoto wake wawili ambao ni Josephat na Zakayo walinusurika kifo baada ya kufanikiwa kutoka wakiwa salama katika mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na gazeti hili, Kalambwia alisimulia ya kwamba siku ya tukio alikuwa kazini katika Hospitali ya Dk Mohammed ambako hufanya kazi ya kuimarisha ulinzi kama askari mlinzi.

Kalambwia anasema kwamba siku hiyo ndio alikuwa amemaliza likizo yake na alikuwa anaripoti kwa mara ya kwanza ofisini baada ya likizo ya mwezi mzima.

“Siku ya lindo ndio nilikuwa naripoti kazini baada ya likizo ya mwezi mmoja kwisha kwa maana ya kwamba laiti nisingeripoti jioni na mvua ilikuwa ikinyesha kubwa sana leo ningekuwa na mimi marehemu,” anasimulia Kalambwia

Hatahivyo, anasema kwamba ilipofika majira ya saa moja asubuhi wakati akiwa kazini mama mmoja ambaye hakumtambua alifika na kumpa taarifa kwamba amepokea taarifa kuwa kuna mti mkubwa umeangukia nyumba yake na hakuna aliyebaki salama.

Anasimulia kwamba pamoja na kupewa taarifa hiyo hakuitilia maanani na kudhani kwamba mama aliyempa taarifa ana matatizo ya akili, lakini wakati akiwa ofisini alipokea simu zaidi ya tatu na ndipo alipoamua kupanda gari kuelekea eneo la tukio.

Kalambwia anasimulia kuwa wakati akiwa njiani alipigiwa simu na mjomba wake ambaye alimwambia kuwa amsubiri katika kituo cha abiria cha Kimandolu na ndipo aliposhuka pale na kutafuta maji ya kunywa wakati huo mvua kubwa ikinyesha.

“Nilipofika pale Kimandolu nilishuka na kutafuta maji ya kunywa, nilijikuta nimekaa kwenye jiwe huku mvua ikinyesha lakini nilikuwa sijitambui,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwamba akiwa pale kituoni alishuhudia gari la polisi likiwa limebeba miili ya marehemu na ndipo aliposhtuka na kubaini kwamba taarifa alizokuwa akizipokea zina ukweli na kuangua kilio.

Kalambwia anasema kwamba pamoja na kumaliza taratibu za mazishi jambo kubwa ambalo limekuwa likimsumbua kichwani ni baada ya kuona tukio hilo lilivyomwacha akiwa maskini wa kutupwa, kwani mbali na watoto wake kupoteza maisha pia mali zake zote zilichukuliwa na mafuriko.

Mkewe azungumza

Mama mzazi wa watoto hao, Rahel Jonathan anasimulia kwamba alinusurika katika  tukio hilo kwa kuwa siku yenyewe alikuwa amelala katika nyumba ya kijana wake akimhudumia mwali ambaye alikuwa amejifungua.

Rahel anasema kwamba siku ya tukio majira ya saa nane usiku alisikia kishindo kikubwa na kushtuka usingizini ambapo muda mfupi alisikia mlango wake ukigongwa na alipokwenda kufungua alimkuta kijana wake Zakayo akilia kwamba nyumba imefunikwa na mti.

“Tuliondoka na mwanangu mpaka kwenye eneo la tukio ili kuona nyumba na ilikuwa imefunikwa yote na mti ndipo nikaanza kupiga kelele kwa majirani kuomba msaada,” anasimulia mama huyo

Rahel anasema kwamba kitanda ambacho watoto wake ambao ni marehemu kwa sasa walikuwa wamelalia usiku huo ndicho hukitumia kulala na laiti kama asingekuwa amelala kwa mwali, leo angekuwa ametangulia mbele za haki.

Anasimulia kwamba ana siku ya 15 akimhudumia mwali wake na siku ya tukio ilikuwa ni siku ya kumi tangu ajifungue ambapo kila akikiangalia kichanga chake anasikia uchungu kwa kuwa baba yake ni miongoni mwa waliofariki dunia.

“Kwa kweli mimi namwachia Mungu tu kwa kuwa kitanda ambacho watoto wangu wamefia ndicho na mimi huwa nakilalia isingekuwa nimelala kwa mwali wangu namhudumia na mimi ningekuwa marehemu,” anasimulia Rahel.

Tukio la mtoto kumuokoa mdogo wake,

Katika tukio hilo kuna tukio la ujasiri lililofanywa na mtoto wake Zakayo wakati nyumba yao ilipofunikwa na mti ambapo alifanikiwa kumwokoa mdogo wake, Josephat aliyekuwa usingizini.

Tukio hilo lililofanywa na kijana huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Ngiresi limeibua mshangao katika familia yake kwa jinsi alivyoonyesha ujasiri  wa kumwokoa ndugu yake.

Akizungumzia tukio hilo, Zakayo anasema kwamba anakumbuka siku ya tukio usiku akiwa usingizini alishtuka baada ya jiwe kumgonga mgongoni na ndipo alipowasha tochi kumulika kinachoendelea na kuamua kuvaa viatu vya mvua na kisha kuruka upande wa dirisha la chumba alichokuwa amelala kukimbilia nje.

Anasema kwamba alipotoka nje ya nyumba hiyo alishuhudia mti mkubwa ukiwa umefunika nyumba na ndipo alipoanza kupiga kelele kuwaita ndugu zake wakiwamo kaka  na dada zake ambao walifariki dunia.

Hata hivyo, anasema kabla ya kuanza kupiga kelele kuomba msaada aliamua kukimbilia katika nyumba ya jirani kumwamsha mama yake ambaye waliongozana mpaka eneo la tukio na ndipo alipofanikiwa kumwona mdogo wake kupitia usawa wa dirisha na kisha kumvuta jambo lililofanikisha kumwokoa akiwa usingizini.

“Nilipokwenda kumwita mama yangu tulikuja naye, mama alianza kulia na kupiga yowe ndipo mimi nilipomwona mdogo wangu kupitia usawa wa dirisha na nikamvuta wakati akiwa usingizini na kufanikiwa kumwokoa,” anasema kijana huyo.