Lipumba akerwa Lissu kupigwa risasi

Muktasari:

  • Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi na vihakikishe wahusika wanapatikana.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kusikitishwa na tukio la kupigwa risasi mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki alipigwa risasi jana Alhamisi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma akiwa ndani ya gari lake na watu wasiofahamika.

Profesa Lipumba amesema tukio hilo linaleta taswira mbaya kwa Taifa la Tanzania.

Amesema tukio hilo linajenga hofu kwa wanasiasa hasa walio maarufu.

"Nimeshtushwa sana... Sijui hata nisemeje, najaribu kufikiria familia yake ambayo itakuwa katika mtikisiko mkubwa, hasa wale watoto wake. Namuomba Mungu awape wepesi katika kipindi hiki na Watanzania waendelea kumuombea hasa wapiga kura wake," amesema Profesa Lipumba.

Amesema tukio hilo halileti picha nzuri kwa Taifa na kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kuhusu wahusika na wachukuliwe hatua za kisheria.