Lipumba awananga viongozi mbele ya marais watatu

Kutoka kushoto ni marais wastaafu Benjamin Mkapa, Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Armando Guebuza (Msumbiji) wakifuatilia mada wakati wa Kongamano la Uongozi la Afrika lililofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Akizungumza jana katika kongamano la uongozi wa Afrika la mwaka 2016 jana jijini Dar es Salaam, mbele ya marais wastaafu watatu, Benjamin Mkapa (Tanzania), Joachim Chissano (Msumbiji) na Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Profesa Lipumba alisema mipango mingi inayoanzishwa Tanzania huwa haitekelezwi kikamilifu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amekosoa viongozi wa Serikali waliopo na wastaafu nchini akisema wana tatizo la kutotekeleza mipango ya maendeleo wanayoiweka.

Akizungumza jana katika kongamano la uongozi wa Afrika la mwaka 2016 jana jijini Dar es Salaam, mbele ya marais wastaafu watatu, Benjamin Mkapa (Tanzania), Joachim Chissano (Msumbiji) na Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Profesa Lipumba alisema mipango mingi inayoanzishwa Tanzania huwa haitekelezwi kikamilifu.

“Mwaka 1999 wakati Rais Benjamin Mkapa akizindua Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2020/2025 alieleza tatizo mojawapo la kutotekelezwa kwa mipango ya maendeleo, hata katika mchango wa Rais mstaafu Thabo Mbeki amesema kuna tatizo la umeme, lakini yote hii ni kutotekeleza mipango tunayojiwekea,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Tatizo letu ni ‘lack of implementation syndrome’, mambo tunapanga lakini hakuna utekelezaji. Kwa mfano, katika mpango wa miaka mitano ilipangwa kuwa ifikapo mwaka 2016 tuwe na uzalishaji wa umeme wa megawati 3,000 lakini tuko kama 1,500/1,600.

“Utasikia Kinyerezi 1 mara Kinyerezi 2 itakuwa imetekelezwa, hatusimamii utekelezaji, sasa inapokuwa hatusimamii, hata sekta binafsi zinashindwa kuendelea… bado hatujapata ufumbuzi wake.”

Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyebobea, alisema Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla inahitaji uongozi unaohamasisha na unaoweza kusimamia mambo.

“Wakati mwingine tunakuwa na viongozi wanaohamasisha lakini hawajui kusimamia mipango ya maendeleo,” alisema.

Kuhusu kuinua biashara za Waafrika, Profesa Lipumba aliitaka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wawekezaji wa Afrika kama zinavyofanya nchi zilizoendelea.

“Kuna mikopo ya riba inayokaribia asilimia sifuri huko Japan na Marekani. Lakini Tanzania hapa riba zinafikia hadi asilimia 90 kwa nini Benki ya Maendeleo ya Afrika inashindwa kuwekeza kwa wafanyabiashara?” alihoji Profesa Lipumba.

Mbali na marais hao wastaafu, walikuwapo pia mawaziri wakuu wastaafu; John Malecela, Cleopa Msuya na Dk Salim Ahmed Salim.

Mwenyekiti wa chama cha UDP, John Cheyo alirejea kaulimbiu yake ya mwaka 1995 alipokuwa akigombea urais kuwa Waafrika wanapaswa kujazwa fedha.

“Naitwa John Momose Cheyo, au maarufu kama Bwana Mapesa,” alisema Cheyo na kusababisha watu kuangua kicheko katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency (Kilimanjaro).

“Mjadala huu hauna tofauti na miaka kadhaa iliyopita nilipompinga Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mimi pia niligombea, niliwaambia Watanzania nitawajaza fedha nyingi. Lakini hawakunichagua mimi bali walimchagua Mkapa.

“Ninachotaka kusema ni kwamba kuna dhana potofu kwa nchi zetu za Afrika. Kwanza tumekuwa tukiwajaza watu wetu na dhana ya umaskini. Hata watu wetu wanakuwa na fedha nyingi mfukoni lakini bado wanajiona kuwa maskini,” alisema Cheyo.

Hata hivyo, Cheyo alimsifu Mkapa akisema katika uongozi wake alifanikiwa kubinafsisha uchumi na kujenga barabara ikiwamo ya Dar es Salaam - Mtwara hivyo kurahisisha uwekezaji wa viwanda kikiwamo cha saruji cha Dangote.

“Rais wa sasa naye amejaribu kujenga reli ya ‘standard gauge’. Mradi huo utazalisha zaidi ya Dola 68 milioni za biashara kwa kubeba mizigo ya tani 14 milioni, tani 9 milioni kutoka Dangote na mizigo mingine kutoka mgodi wa nikeli wa Kabanga. Atatengeneza biashara nyingi za usafirishaji. Kwa hiyo tusahau umaskini.

Makamu Rais wa Benki AfDB, Frannie Leautier alisema lengo la mjadala huo ni kuinua sekta binafsi.

“Kuna mambo makubwa matatu tunayoyaangalia; kwanza upendo wa viongozui wa Afrika kwa wananchi wao, ili miradi ya maendeleo iendelezwe. Pili utekelezwaji wa miradi ya maendeleo na uwezo wa viongozi wa Afrika kuangalia mbele, kuhakikisha wananchi wanapewa kipaumbele,” alisema Leautier.

Akizungumzia tatizo la migogoro kwa nchi za Afrika, Mbeki alisema rushwa ni tatizo kubwa, huku akitoa mfano wa Sudan Kusini akisema baadhi ya viongozi wa chama cha SPLM wanamiliki makampuni na akaunti za benki nje ya nchi hiyo.

“Utakuta mpigania uhuru ana kampuni nje ya nchi na inaongeza matatizo ya kupatikana amani, kwa mfano Sudan Kusini. Viongozi wamekifanya chama cha SPLM kuwa mali yao binafsi,” alisema Mbeki.

Chissano alitoa mfano wa nchi yake akisema mtaji pekee wa kuwawezesha wananchi ni ardhi: “Ardhi ndiyo msingi wa maendeleo. Tulipopata uhuru tulitangaza kilimo kuwa biashara kuu, lakini watu hawakuwa na ardhi, tukasema ardhi haiuzwi, ni mali ya wananchi.”

Akitoa mada ya ufunguzi katika kongamano hilo, Mfanyabiashara maarufu wa Afrika Kusini, Sipho Nkosi aliwataka viongozi wa Afrika kuzipenda nchi zao na wananchi wao.

“Serikali inatakiwa kuwa mfano. Ili tufanikiwe tunatakiwa kuzipenda nchi zetu, kwanza tujipende wenyewe kwa sababu ukijipenda utajilinda. Kama nitawapenda watu wangu nitakufa kwa ajili yao, kama nitaipenda nchi yangu nitakufa kwaa jili yake,” alisema Nkosi.