Lissu, Wasonga nusura wazichape mahakamani

Mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu (Kushoto) akimweleza jambo wakili Godwin Ngwilima katika Mahakama Kuu ya Dodoma jana. Picha na Ben Patrick

Muktasari:

  • Katika mahakama hiyo, ambayo ilifurika umati mkubwa wa mawakili na wasikilizaji, wawili hao waliibua mzozo wakiwa kwenye ushoroba (korido) walipokuwa wakisubiri kuingia kwenye chumba cha mahakama kuanza kusikilizwa kwa kesi mbili, ya kwanza namba 12/2017 ya kupinga uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambayo ilifunguliwa na Wasonga, na nyingine ni namba 13 na 14/2017 ambazo Lissu na wenzake walipeleka maombi ya kuunganishwa katika kesi hiyo ya Wasonga.

Dodoma. Mawakili maarufu nchini Tundu Lissu na Godfrey Wasonga jana nusura wazipige kavukavu na kama si busara za mawakili wengine waliokuwa wamefurika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na hasa Deus Nyabiri, huenda hali ingekuwa tofauti.

Katika mahakama hiyo, ambayo ilifurika umati mkubwa wa mawakili na wasikilizaji, wawili hao waliibua mzozo wakiwa kwenye ushoroba (korido) walipokuwa wakisubiri kuingia kwenye chumba cha mahakama kuanza kusikilizwa kwa kesi mbili, ya kwanza namba 12/2017 ya kupinga uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambayo ilifunguliwa na Wasonga, na nyingine ni namba 13 na 14/2017 ambazo Lissu na wenzake walipeleka maombi ya kuunganishwa katika kesi hiyo ya Wasonga.

Sakata lilianzia kwa Lissu, ambaye aliwashawishi wenzake kumuunga mkono kabla ya kuanza kesi hiyo kuwa wamuombe Jaji Awadh Muhamed abadilishe chumba cha kusikilizia kesi hizo kutokana na umati uliokuwa umefurika akisema eneo alilopanga lilikuwa ni dogo.

Hoja hiyo ilipingwa na Wasonga ambaye alimtaka Lissu kunyamaza kwa kuwa si mhusika ndipo wakaanza kurushiana maneno makali na kutaka kupigana huku kila mmoja akiwa ameshikiliwa na watu.

“Nitakufanya kama nilivyokufanya kule Singida na sijui kama umesahau... nitakushughulikia mimi si wa mchezo mchezo ,” alisema Wasonga huku akiwa ameshikwa na mawakili wanne.

Wakati huo, Lissu aliyekuwa ameshikwa mkono na Nyabiri alikuwa akirusha maneno kwa Wasonga akimweleza kuwa hawezi kumfanya kitu.

Kelele hizo zilimfanya Jaji Muhamed aliyekuwa akiendelea na kesi nyingine kuhoji sababu za kuwapo kelele nje hivyo kumtuma askari magereza ambaye aliwaambia jaji anahoji sababu ya kelele hizo.

Baada ya angalizo hilo, Nyabiri aliwasihi wanyamaze lakini Wasonga alionekana bado ana hasira hivyo mawakili wenzake kumtoa.

Nje ya mzozo huo, katika kesi mbili ambazo ziliwafikisha mahakamani hapo jana, Lissu ambaye ni mgombea urais wa TLS na mgombea umakamu wa rais, Godwin Ngwilimi walisema wanamwakilisha mgombea mwingine wa urais, Lawrence Masha kutaka mahakama ikubali ombi lao la kuingizwa katika kesi namba 12/2017 ambayo ilifunguliwa na Wasonga.

Katika kesi namba 12, Jaji Muhamed alianza kusoma barua ya Wasonga ya kutaka aiondoe mahakamani kwa kuwa ilifunguliwa kimakosa lakini akasema anayo hati ya kufungua upya baada ya marekebisho.

Alipomaliza kusoma barua hiyo, jaji akaomba muda wa kuitafakari huku akiwaomba mawakili wakubali kuhamisha chumba cha mahakama kutokana na idadi kubwa ya watu.

“Hii barua ya kuondoa kesi ndiyo nimeipata muda huu, naomba mnipe muda ili nitafakari, baada ya dakika 15 tukutane mahakama ya wazi maana hapa naona hapatoshi, lakini siyo lazima mje na majoho kwani mnajulikana,” alisema.

Baada ya dakika 20 wakiwa katika mahakama ya wazi, Jaji Muhamed aliwaita mawakili wa pande zote na kuzungumza nao kwa dakika 22 ndipo wakarejea saa 5:40 asubuhi. Kesi hiyo iliendelea tena huku kila upande ukipewa dakika sita ukianza na upande wa waliopeleka maombi ya kutaka waunganishwe katika kesi hiyo.

Mawakili hao; Lissu, Fred Kalonga, Paul Kaunda na Ngwilimi waliamua kumpa dakika zao Lissu na akazitumia kuwasilisha kile walichokiita hati ya haki.

Lissu alisema waliamua kuomba nafasi ya kuunganishwa katika kesi hiyo kwani wanajua kuwa kama hawataunganishwa, kwa vyovyote haki yao inaweza kupotea na hasa kwa wagombea.

“Mheshimiwa jaji, mimi Tundu Lissu na Lawrence Masha ni wagombea wa nafasi ya rais wa TLS, lakini pia yupo mwenzetu Godwin Ngwilimi ambaye anagombea nafasi ya makamu wa rais, kwa pamoja tunaomba kuunganishwa katika kesi hii kwa kuwa tuna masilahi na tunaweza kupoteza,” alisema Lissu na kuongeza:

“Kanuni ya 14 ya Mwenendo wa Mashtaka inaruhusu mtu mwenye masilahi kuomba aingizwe. Katika kanuni hiyo kifungu cha 1 na 2 vinaruhusu mheshimiwa Jaji, na hati ya maombi inajieleza yenyewe.”

Baada ya kueleza hayo ilikuja zamu ya Wasonga ambaye alisema, “Mheshimiwa Jaji, hakuna mahali ambapo mawakili hawa wanaweza kuingia na sheria inawaondolea uhalali hata wa kuleta maombi ya aina hii.”

Wasonga alihoji kati ya wagombea wote ni kwanini hao watatu ndiyo waliamua kwenda mahakamani Dodoma kutaka waunganishwe wakati wako wengi na akahoji kama ni gharama mbona wote walikuwa wameziingia.

Kuhusu ombi lake la kupinga uchaguzi, alisema kanuni za uendeshaji ni mbovu na haziwezi kuwafanya viongozi wake kuwa halali.

Mawakili wa TLS

Mawakili Deus Nyabiri na Elias Machibya ambao walisimama kwa niaba ya TLS, walikubaliana na hoja za waleta maombi Lissu na wenzake kwamba wanazo sababu za msingi za kuomba kuingizwa katika kesi hiyo huku wakisema Wasonga alifanya uamuzi kwa kukurupuka na kwamba ana lengo la kuivuruga TLS.

Machibya alisema hoja zote za Wasonga hazikuwa na mashiko, akaiomba mahakama kutupilia mbali utetezi wa wakili huyo na waombaji waingizwe na ili waje kumdai gharama.

Machibya alisema kanuni alizozipinga Wasonga ni nzuri kwani zilianza kutumika Januari Mosi, 2016 na kwamba viongozi wa sasa waliingia kwa kutumia kanuni hizo.

Mvutano uliendelea huku Jaji akisisitiza wapeane nafasi ya kueleza bila kurushiana maswali ndipo Ngwilimi alipohitimisha kwa kumuomba Jaji awaruhusu waingizwe kwenye kesi na bila ya kufanya hivyo, watakuwa wamepoteza haki zao zote kwani walishatumia gharama kuwashawishi watu wawachague.

Baada ya hoja hizo, Jaji Muhamed aliahirisha kesi hiyo kwa muda na ilipotimu saa 8:00 mchana alisema akirejea atatoa uamuzi wa kama waombaji wanastahili kuingizwa kwenye madai hayo au hawana sifa.

Aliporejea saa 8:13 mchana, Jaji hakutoa uamuzi huo kama alivyokuwa ameahidi kwani malumbano yaliendelea kwa kiasi kikubwa baada ya Wasonga kukiri kuwa alikuwa amekosea katika shtaka la awali, lakini akasema anayo hati nyingine ya kuwasilisha kwa kuifungua upya.

Ilichukua zaidi ya saa mbili kwa mawakili kuwasilisha hoja za kumpinga huku wakimpiga vijembe Wasonga ambaye hata hivyo alionekana kuwa imara kwa kujibu mashambulizi kila alipopewa nafasi.

Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo aliungana na hoja za upande wa Lissu na TLS kuwa Wasonga alikuwa amekosea na kumtaka akubali kuondoa kesi yake mahakamani na kulipa gharama.

Hata hivyo, Wasonga alipinga hoja ya kulipa gharama akisema atawasilisha ombi jingine lililo sahihi alimradi ahakikishe uchaguzi wa TLS haufanyiki.

Kesi zote mbili zitatolewa uamuzi leo mchana na Wakili Wasonga alisema baada ya uamuzi huo atafungua kesi nyingine hapohapo ambayo tayari alishafanya marekebisho ya vipengele vyake.

Nje ya mahakama

Lissu alidai kuwa anazo taarifa za njama za kumkamata na kumweka mahabusu ili asiwepo kwenye uchaguzi huo, lakini akasema hata akiwa gerezani lazima atashinda uchaguzi huo bila ya kizuizi.

Wakati Lissu akisema hivyo, Wasonga alisema kwa vyovyote atapinga uchaguzi huo na hatakuwa tayari kuona ukifanyika huko Arusha, Jumamosi.

Kesi nyingine Dar

Wakati hayo yakitokea Dodoma, jijini Dar es Salaam jana mahakama ilieleza kuwa hatima ya kesi dhidi ya TLS itajulikana leo wakati itakapotoa uamuzi wa pingamizi lililowekwa na Serikali pamoja na TLS.

Kesi hiyo ya kikatiba imefunguliwa na wakili wa kujitegemea, Onesmo Mpinzile katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika kesi hiyo, Mpinzile anapinga kanuni za uchaguzi za TLS za mwaka 2016, akiiomba mahakama itamke kuwa ni batili kwa madai kuwa zilisainiwa na kupitishwa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka katika TLS.

Hata hivyo, juzi AG na TLS waliwasilisha pingamizi la awali wakiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi hiyo, wakidai kuwa mdai hana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo na kwamba hati ya kiapo inayounga mkono maombi yake ina dosari za kisheria.

Hoja hizo za pingamizi la Serikali na TLS zilisikilizwa na jana mdai kupitia kwa wakili wake, Emmanuel Makene, alimalizia kujibu hoja hizo za pingamizi huku naye akiiomba mahakama itupilie mbali mapingamizi hayo ya Serikali na TLS.

Baada ya kukamilisha usikilizwaji wa hoja za pande zote jana, kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Rose Teemba aliiahirisha hadi leo kwa ajili ya uamuzi. Mbali na Jaji Teemba, majaji wengine katika kesi hiyo ni Beatrice Mutungi na Ignas Kitusi.

Uamuzi wa mapingamizi hayo leo ndiyo utakaoamua uhai wa kesi hiyo, kwani ikiwa Mahakama itakubaliana nayo, kesi hiyo itatupiliwa mbali na huo ndiyo utakuwa mwisho wake.

Hata hivyo kama itayatupilia mbali, kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya usikilizwaji wa maombi ya wanasheria wengine wanaoomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo upande wa wadaiwa, kama wadaiwa wenye masilahi nayo, kabla ya usikilizwaji wa kesi ya msingi.

Wanasheria hao walioomba kuunganishwa ni Tundu Lissu, Lawrence Masha na Jamhuri Johnson.