Lissu aenda rumande na tisheti ya Ukuta

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akiongozwa na polisi sehemu ya kwenda kukaa baada ya kuingizwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya  kusomewa mashtaka ya kudaiwa kutoa lugha ya uchochezi, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

  • Asomewa shtaka jingine la uchochezi, lakini adai kusema ukweli hakujawahi kuwa kosa la jinai, ‘kwa hiyo si kweli.’

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alienda mahakamani na baadaye rumande akiwa amevaa fulana iliyoandikwa “Ukuta” na kusomewa shtaka la kutoa lugha ya uchochezi, lakini hakupewa dhamana kutokana na ubishi wa kisheria.

Hakimu Mkazi MKuu wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri alisema atatoa uamuzi kuhusu dhamana ya Lissu keshokutwa Alhamisi, baada ya upande wa mashtaka kuipinga.

Lissu alifika mahakamani hapo akiwa amevalia suti ya gwanda ya rangi ya bluu na aliposhuka kutoka kwenye gari, alifungua vifungo vya jaketi na kufanya fulana hiyo nyekundu iliyoandikwa maneno “Ukuta” kuonekana.

Alipelekwa mahabusu ya mahakama na alipotoka alikuwa amevua jaketi na kubakia na fulana hiyo, akiwa anapunga mkono juu huku akinyoosha vidole viwili kuashiria alama ya Chadema.

Baada ya kunyimwa dhamana, Lissu alirudi mahabusu akiwa amevalia jaketi hilo.

Katika kesi hiyo, Lissu anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 17 akiwa Ufipa wilayani Kinondoni. Anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni ya ubaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa alidai wakati akisoma mashtaka hayo kuwa Lissu pia alisema vibali vya kazi vinatolewa kwa wamishenari wa kikatoliki tu, huku madhehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji.

Mutalemwa alidai kuwa siku hiyo Lissu alisema “viongozi wakuu wa Serikali huchaguliwa kutoka kwenye familia, kabila na ukanda. Acheni woga pazeni sauti, kila mmoja wetu. Tukawaambie wanaompa msaada wa fedha Magufuli na Serikali yake, kama tulivyowaambia wakati wa serikali ya makaburu. Hii Serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe na jumuiya ya kimataifa isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi. Yeye ni dikteta uchwara”.

Kishenyi alidai kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kujenga chuki ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mashauri alimtaka Lissu aeleze kama analikubali kufanya kosa hilo ama anakataa.

Na Lissu alijibu: “Kusema ukweli hakujawahi kuwa kosa la jinai. Kwa hiyo si kweli.”

Wakili Kishenyi aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kueleza kuwa wana hoja wanataka kuiwasilisha mahakamani hapo.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Simon Wankyo alisema wakati akipinga dhamana kuwa Lissu ana kesi kadhaa zinazomkabili ambazo alizitaja kuwa ni kesi namba 233 ya 2016, kesi namba 123 ya 2017, kesi namba 2270 ya 2016 na kesi namba 208 ya 2016.

Wankyo alidai kuwa kesi hizo zote ni za uchochezi na kwamba ni dhahiri makosa ya mshtakiwa huyo yanajirudia kwa kujumlisha kosa la jana.

Alidai kuwa kutokana na kujirudia kwa makosa hayo na kujenga chuki, wanaomba mshtakiwa asipewe dhamana kwa madai kuwa anaweza kusababisha madhara makubwa.

Wankyo alidai kuwa matamshi hayo si ya kawaida kwa sababu yanajenga chuki kwa wananchi, matabaka na madhara yake si madogo kama akiachiwa na kunyamaziwa kwa kuwa yamegusa udini, ukabila, familia na ukanda.

“Hivyo ni dhahiri si ya kawaida upande wa mashtaka tunaomba mahakama iangalie kwa jicho la ukali na kumnyima dhamana mshtakiwa kwa kuwa tunaamini amekuwa akiyatoa matamshi hayo baada ya kupewa dhamana. Asipopewa dhamana hayo hayatajirudia,” alisema Wankyo.

Naye wakili wa serikali, Tulumanywa Majigo aliiomba mahakama itumie mamlaka yake kutotoa dhamana kwa mshtakiwa kwa sababu ya ulinzi na usalama wake, akisema shauri dhidi yake linalenga kujenga chuki na kwamba chuki hiyo imejikita kwenye ukabila, ukanda na dini.

Alidai matamshi hayo yanalenga kubomoa misingi ya umoja, mshikamano na upendo ambao umejengeka miongoni mwa Watanzania na kwamba mahakama hiyo inatekeleza majukumu yake kwa sababu kuna umoja na amani.

Lakini wakili wa Lissu, Fatma Karume, akiwakilisha jopo la mawakili 18, aliiambia mahakama kuwa dhamana ni haki ya mshtakiwa kwa misingi ya sheria na si mawakili.

Karume aliwakumbusha mawakili wa upande wa mashtaka kuwa Lissu hajahukumiwa zaidi ya kutuhumiwa tu na kwamba uchunguzi haujakamilika na hivyo si sahihi kumnyima dhamana.

“Maana wanataka mahakama imfunge Lissu kwa kuwa ni upinzani, na Serikali ya CCM inataka kumfunga Lissu kwa sababu wameamua wao kuna maneno kayasema ya uchochezi,” alisema Karume.

Alieleza kuwa kesi za upande wa mashtaka dhidi ya Lissu zimeanzishwa 2015 na kwamba hiyo ni muhimu wote wajue ni baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani.

Karume alidai kuwa katika kesi nne zilizotajwa na upande wa mashtaka 2016, hakuna hata moja ambayo upelelezi umekamilika.

Alidai kila akipaza sauti wanafungua kesi lakini kumalizia wanashindwa.

“Kama wanataka mahakama hii imfunge Lissu, waendeshe kesi zao hadi mwisho,” alisema Karume.

“Serikali wanasema wananchi wanataka kumdhuru Lissu. Serikali inataka kumdhuru Lissu, wamemshtaki hii kesi ya tano. Hawana upendo.”

Alisema kama Serikali haipendi anachosema Lissu, basi ijirekebishe na si kumpeleka mahakamani na kutaka akae ndani.

“Wakijirekebisha, ataacha kusema. Hatakuwa na cha kusema,” alisema.

Alibainisha kuwa Lissu ni Mkatoliki, kama Rais Magufuli, hivyo kuna mambo kayaona ambayo hayapendi na hivyo kuamua kupaza sauti.

“Sasa wanataka kumuweka mahali kwa ridhaa yako, ili sauti yake isisikie waizime kabisa,” alisema Karume.

Wakili mwingine wa Lissu, Peter Kibatala aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka ulikuwa na wajibu wa kuwasilisha hati ya kiapo yenye hoja za kuzuia dhamana na jukumu la kumlinda Lissu ni la Serikali kupitia Jeshi la Polisi na akaiomba mahakama impatie dhamana.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu Mashauri alisema atatoa uamuzi wa dhamana hiyo Alhamisi wiki hii.