VIDEO: Lissu asimulia mwaka mmoja nje ya Bunge

Muktasari:

Mbunge wa Singida ,Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 nje ya nyumba yake mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka katika kikao cha Bunge na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na baadaye kuhamishiwa jijini Nairobi, Kenya alikotibiwa kwa takribani miezi miwili, kupelekwa nchini Ubelgiji 

Dar es Salaam. “Nimei-miss sana Tanzania na nimewa-miss Watanzania.” Hii ndiyo kauli ya Tundu Lissu leo anapotimiza mwaka mmoja tangu ashambuliwe kwa risasi mjini Dodoma.

Lissu, ambaye hadi sasa amefanyiwa upasuaji mara 21 katika mwili wake, amefanya mazungumzo maalumu na Mwananchi na kueleza masuala mbalimbali huku akisisitiza, “Nitarudi.”

Haya ndiyo mahojiano ya Lissu na Mwananchi

Swali. Mwaka mmoja umetimia bila kushiriki Bunge, siasa za jimboni wala kazi za uwakili, umemiss kitu gani?

Jibu: Ninachoweza kusema ni kwamba nimei-miss sana Tanzania na nimewa-miss Watanzania.

Nime-miss sana Bunge, licha ya matatizo yote ya Bunge la Spika (Job) Ndugai. Nimewa-miss sana watu wangu wa Jimbo la Singida Mashariki na mikutano ya hadhara.

Nime-miss sana kazi zangu za chama na nimewamiss viongozi wenzangu, wanachama wetu na wafuasi wetu katika mamilioni yao.

Nime-miss sana mapambano ya utetezi wa haki za watu wetu ndani na nje ya Mahakama. Nimewa-miss mawakili wa Tanzania Bara walionipa heshima ya kuwaongoza.

Miaka mingi iliyopita niliwahi kusoma shairi liitwalo ‘The Exile’, yaani ‘Uhamishoni’, la mshairi maarufu wa Soweto, marehemu Sipho Sepamla. Shairi hilo linaelezea machungu ya kuishi uhamishoni kwa kulazimishwa.

Katika huu mwaka mmoja wa kulazimishwa kuwa nje ya nchi; wa kutokuonana moja kwa moja na watu wetu, familia, ndugu, jamaa, sasa ninaelewa maana hasa ya kuwa ‘uhamishoni.’

Swali: Kuna mvutano juu ya matibabu yako, kati ya wewe, familia na Chadema dhidi ya Bunge, hili unalizungumziaje?

Jibu: Mvutano huu ni wa kutengenezwa na ni aibu kubwa kwa Bunge kama taasisi na kwa uongozi wake.

Spika Ndugai na Katibu wa Bunge wa wakati huo, Dk Thomas Kashililah walikutana na ndugu zangu kwenye ofisi ya Bunge Dar es Salaam na kuwashauri waandike barua ya maombi ili Bunge liweze kutoa fedha za matibabu yangu.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu naye alishauri hivyohivyo, tena hadharani kwenye mkutano na waandishi habari.

Barua zikaandikwa kama ilivyoelekezwa. Mara Kashililah akaondolewa madarakani na Stephen Kagaigai akateuliwa kushika nafasi hiyo.

Inaelekea kuna maelekezo Tundu Lissu asipewe pesa ya matibabu na Bunge.

Spika amethibitisha hivyo, tena ndani ya Bunge. Aliliambia Bunge mwezi Juni kwamba sitatibiwa na Bunge kwa sababu Rais hajatoa idhini hiyo.

Spika Ndugai amekubali kupokwa madaraka ya kuendesha Bunge kama mhimili. Hii haijawahi kutokea tangu Bunge lianzishwe wakati wa ukoloni.

Swali: Unafikiri tukio lako lilitokana na harakati za kisiasa au kiuwakili?

Jibu: Nilishambuliwa kwa sababu ya msimamo wangu wa kisiasa, hasa kwa kuipinga Serikali kwa kuikosoa hadharani.

Nimekuwa wakili kwa miaka 15 na sijawahi kutiwa msukosuko wowote kutokana na kazi yangu.

Lakini nimekuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu za Watanzania na harakati za kisiasa tangu kabla sijamaliza masomo.

Kwa sababu ya kuwa mwanaharakati wa aina hiyo, nimetiwa misukosuko mingi tangu enzi za marais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Nilikamatwa na Serikali ya Mkapa Desemba 2002 kwa sababu ya kutetea wachimbaji wadogowadogo waliouawa Bulyanhulu mwaka 1996. Nilikamatwa na Serikali ya Kikwete mara mbili; mara ya kwanza mwaka 2012 kufuatia mauaji ya wananchi wa Tarime katika Mgodi wa Nyamongo na mara ya pili kufuatia mauaji ya Soweto, Arusha, mwaka 2013.

Lakini ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, nimekamatwa mara nane na kufunguliwa kesi za jinai sita mahakamani. Walifikiri watanitisha na kuninyamazisha.

Moyo wangu haujavunjika. Nafsi yangu iko vilevile. Na msimamo wangu haujatetereka.

Ernest Hemingway, Mwanafasihi wa Kimarekani na Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi, aliandika - katika fasihi yake ya ‘The Old Man and the Sea’ - kwamba “mtu anaweza kuuawa lakini asishindwe”.

‘Kushindwa’ kwa maana ya Hemingway ni kukata tamaa na kubadili msimamo na kukubali kumtumikia kafiri ili upate mradi wako. Nimeumizwa vibaya kimwili, bado niko hai. Sijashindwa.

Swali: Je, ukirudi nchini utaendelea kufanya siasa za aina hiyo?

Jibu: Ndiyo. Nikinyamaza sasa maana yake nimeshindwa, nikibadili msimamo sasa maana yake ni kwamba maumivu yote ya mwaka huu mmoja hayakuwa na maana.

Nikitetereka sasa maana yake ni kwamba kazi ya maelfu kwa maelfu ya walioniombea, walionichangia kwa hali na mali na ambao wameweka matumaini yao kwangu, ilikuwa ya bure.

Ninaomba Mungu anisaidie ili kikombe cha usaliti wa aina hiyo kinipitie pembeni.

Swali: Mwaka mmoja umetimia kukiwa hakuna mtu yeyote aliyetiwa mbaroni, unazungumziaje?

Jibu: Si tu hakuna mtu aliyetiwa hatiani. Hakuna mtu yeyote anayeshukiwa kunishambulia. Hakuna yeyote anayetuhumiwa. Hakuna yeyote aliyehojiwa na polisi kama shahidi. Hata ‘mhanga’ wa shambulio lenyewe hajahojiwa.

Lakini ndugu zangu na viongozi wangu wa chama walisema tangu mwanzo: Jeshi la Polisi la Tanzania haliwezi kuchunguza shambulio hili.

Marehemu Sipho Sepamla aliandika katika shairi lingine: ‘watafute ushahidi kwa ajili gani wakati jua la mchana liliangaza macho yake kwenye kitendo chote kilichofanyika.’

Swali: Katika kipindi chote ukiwa nje ya nchini, mkeo Alice yupo kando yako akikuuguza, unamzungumzije?

Jibu: Mke wangu mpenzi amepitia mengi na makubwa sana katika mwaka huu mmoja. Ameacha kuangalia watoto wetu; ameacha mji wake na kazi yake ya uwakili. Ameacha kila kitu chake ili kuniuguza. Huyu ni mke mwema aliyetajwa katika maandiko matakatifu. Ninajihesabu mbarikiwa kuwa naye kama mke wangu.

Swali: Una kipi unachoweza kukielezea kuhusu mwaka mmoja baada ya kushambuliwa?

Jibu: Baada ya kushindwa na Wajapani kwenye Mapigano ya Ghuba ya Leyte, nchini Ufilipino, mwaka 1942 wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Kamanda wa majeshi ya Marekani, Jenerali Douglas MacArthur, alitamka: ‘Nitarudi.’ Na mimi nawatamkia Watanzania: ‘Nitarudi’.

Swali: Ukipona na kurejea nchini utagombea tena ubunge au utahamia kwenye urais?

Jibu: Mimi ni mwanachama na kiongozi mwaminifu wa Chadema. Nitapigania nafasi yoyote ambayo chama chetu kupitia vikao vyake halali kitaona inafaa kwa kuzingatia vigezo stahiki.

Itaendelea kesho....