Lissu azinduka Nairobi

Muktasari:

  • Ni baada ya dawa za usingizi alizochomwa kuisha mwilini

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema kuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Tundu Lissu anaendelea vizuri na ameshazinduka.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa, Dk Mashinji amesema amezungumza na mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe ambaye aliongozana na Lissu kupata matibabu Nairobi nchini Kenya na amemueleza kuwa Lissu anaendelea vema na amezinduka baada ya dawa alizochomwa kwa ajili ya kupumzika na kusafiri kuisha.

Amesema damu ya Lissu imemwagika kabla ya wakati wake hivyo makamanda wa chama hicho nchi nzima waende kwenye hospitali na zahanati kutoa damu.

"Tuchangie damu kuhakikisha benki za damu zinakuwa na damu ya kutosha ili ziwasaidue wahitaji," amesema Dk Mashinji.

Dk Mashinji amesema tukio hilo halijawatisha badala yake limewaimarisha zaidi.

Alifafanua kuwa Lissu alimiminiwa risasi za kutosha kuashiria kulikuwa na lengo la kuua.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Profess Abdallah Safari amesema wao kama wanasheria likitokea jambo kama lililomtokea Lissu huangalia mambo mawili makubwa, ambayo ni imetumika silaha gani na amepigwa eneo gani, hivyo kwa Lissu alilengwa kupigwa kichwa na kifua kuonyesha wazi kulikuwa na nia ya kuua.

"Hali inatia simanzi watu wa usalama wafanye kazi yao kwa weledi kulibainisha hili,"alisema Profesa Safari.

Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema kazi kubwa ya Serikali ni kulinda usalama wa raia, kama imeshindwa kufanya hivyo inaonekana wazi kuna kasoro za uwajibikaji.

"Kwa sisi tuliofanya shughuli za uongozi siku nyingi uwajibikaji unaweza kukosekana kwa makusudi au kwa uwezo na kupanga," amesema Sumaye.