Lissu kupelekwa Ulaya kwa matibabu Januari 6

Muktasari:

>>Mbowe amesema gharama zilizotumika kwa matibabu hadi sasa ni dola 300,000 za Marekani sawa na zaidi ya Sh600 milioni.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu atapelekwa Ulaya kwa matibabu ya mazoezi.

Mbowe akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Desemba 31,2017 amesema Lissu ameshamaliza matibabu na upasuaji katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na sasa anafanyiwa mazoezi.

"Tiba zote ameshamaliza kinachoendelea sasa ni mazoezi," amesema.

Mbowe amesema Januari 6,2018 Lissu atapelekwa katika moja ya nchi za Ulaya kwa ajili ya tiba ya mazoezi.

"Kwa sasa siwezi kuitaja nchi anakokwenda kwa ajili ya usalama," amesema.

Amesema gharama zilizotumika hadi sasa kumuuguza ni dola 300,000 za Marekani sawa na zaidi ya Sh600 milioni.

Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7,2017.

Alihamishiwa Nairobi siku hiyohiyo baada ya kupatiwa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Picha iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii Jumanne Desemba 26,2017 ilimuonyesha Lissu akiwa amesimama kwa msaada wa madaktari wa mazoezi ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipofikishwa hospitalini hapo.