Lori lalalia Noah, watano wafariki dunia

Muktasari:

Lori hilo liliparamia magari mengine matatu kabla ya kupinduka na kulalia gari dogo aina ya Noah na kusababisha vifo hivyo.


Mbeya. Siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutangaza uamuzi wa kulivunja Baraza la Usalama Barabarani kwa tuhuma za kushindwa kudhibiti ajali, ajali nyingine imetokea jijini Mbeya na kusababisha vifo vya watu watano papo hapo, huku mmoja akijeruhiwa.

Kama ilivyokuwa kwenye ajali ya awali iliyotokea katika Mteremko wa Mlima Mbalizi na kusababisha vifo vya watu 20, ajali ya juzi usiku pia imehusisha lori la mizigo lililofeli breki likiwa kwenye mteremko mkali wa Igawilo, Barabara Kuu ya Tanzania-Malawi.

Lori hilo liliparamia magari mengine matatu kabla ya kupinduka na kulalia gari dogo aina ya Noah na kusababisha vifo hivyo.

 

Akizungumza leo Julai 6, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mbeya, Leopold Fungu alisema chanzo cha ajali hiyo ni lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya sukari likitokea Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi kwenda nchini Rwanda.

Amesema lori hilo lilipofika kwenye mteremko mkali wa Igawilo, lilipoteza mwelekeo na kuanza kuyagonga magari mengine kabla ya kupinduka.

Kamanda Fungu amesema lori hilo lililokuwa limebeba zaidi ya tani 28 za sukari liliangukia gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba watu watatu na kusababisha wawili kati yao kupoteza maisha papo hapo.

“Pia dereva wa lori hili pamoja na msaidizi wake nao wamepoteza maisha kwenye ajali hii na mtu mwingine waliyekuwa naye hivyo kusababisha vifo vilivyotokea kwenye ajali hii kufikia watu watano,” amesema Kamanda Fungu.

Amesema mtu mmoja aliyekuwa ndani ya Noah alitolewa akiwa hai lakini amejeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa matibabu.

Kwa mujibu wa Kamanda Fungu, waliokuwa kwenye magari mengine yaliyohusika kwenye ajali hiyo walifanikiwa kutoka salama.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema ajali ambazo zimetokea mfululizo mkoani Mbeya zinaliingizia taifa hasara kwa kupoteza mali na rasilimali watu hivyo ipo haja ya kubuni mbinu zaidi za kukabiliana na ajali hizo.

“Licha ya Serikali mkoa kuendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola juzi, kwa hali hii inatupasa kufikiria mbinu zaidi za kukabiliana na ajali, hii ni pamoja na kushirikisha viongozi wa dini na viongozi wa mila katika kumuomba Mungu atuepushe na ajali za aina hii,” alisema Makalla.