Lugha ya kichina yashika kasi UDSM

Muktasari:

  • Ujio wa walimu hao ni mkakati wa kutimiza lengo la kuboresha ufundishaji wa lugha katika nchi za Tanzania na China zenye historia ya muda mrefu wa ushirikiano.

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimepokea walimu 24 kutoka Chuo cha Zhejiang Normal cha China  watakaosambazwa katika baadhi ya shule na vyuo nchini ili kujifunza Kiswahili na kufundisha lugha yao.

Ujio wa walimu hao ni mkakati wa kutimiza lengo la kuboresha ufundishaji wa lugha katika nchi za Tanzania na China zenye historia ya muda mrefu wa ushirikiano.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha walimu hao, Kaimu Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Profesa Florens Luoga amesema ili kuitumia fursa iliyopo ya kujifunza  Kichina na kukitangaza Kiswahili duniani, kuna kila sababu ya kufurahia ujio wa wanafunzi hao.

Profesa Luoga amesema katika kuhakikisha mafunzo hayo ya lugha yanakuwa endelevu, mwakani UDSM itaanza kutoa shahada ya lugha ya Kichina.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius ya UDSM inayofundisha lugha ya  Kichina, Profesa Zhang Xiaozhen amesema baadhi ya wanafunzi hao  watakaa Tanzania kwa miaka miwili na wengine mwaka mmoja.