Lugola amtaka IGP Sirro kupunguza vituo vya ukaguzi wa magari

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya leo kabla ya kuanza ziara yake mkoani hapa. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesikitishwa na utitiri wa vituo vingi vya ukaguzi wa magari vinavyochelewesha wananchi kwenda katika shughuli zao

 


Mbeya. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro kuangalia uwezekano wa kupunguza vituo vya ukaguzi wa magari barabarani visivyokuwa na ulazima wa kuwepo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Oktoba 3, 2018 ofisini kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya, Lugola amesema kuwepo vituo vingi vya ukaguzi wa magari linageuka kero kwa abiria na watumiaji wa barabara.

“Utakuta kila baada ya hatua 20 unawakuta askari tena zaidi ya watano, wamesimamisha magari mengi wanayakagua, lakini ukiangalia hakuna umuhimu wa kufanya hivyo,” amesema Lugola.

“Sasa hii ni kero, hivyo nimtake Inspekta Jenerali wa Polisi (Sirro), kuangalia uwezekano wa kuanza kupunguza vituo hivyo kwani kusimamisha magari mengi eneo moja halafu mtu anakaa nusu saa au saa zima hajakaguliwa anapoteza muda mwingi wa kwenda kufanya shughuli nyingine.”

Pamoja na hilo, Lugola amesema ametua jijini Mbeya kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya kukabiliana na matukio ya ajali aliyoyatoa Julai 2, 2018 jijini hapa alipofika yeye na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe.

Lugola amejipambanua kwamba ni muumini ya kufuatilia utekelezaji wa mambo anayoyatoa kwa watumishi wake.

"Ziara yangu ya kwanza nilipoteuliwa nilikuja Mbeya na nikatoa maagizo ya Kitaifa, hivyo nimekuja Mbeya kufuatilia utekelezaji wa yale niliyoagiza," amesema Lugola.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amemuomba Lugola kuwaongezea askari magari kwani kuna changamoto ya magari ya doria na ya washa washa.

“Lakini mheshimiwa waziri, (Lugola) mkoa wetu ni mkubwa na una changamoto nyingi na askari wetu licha ya kufanya kazi usiku na mchana, tunaomba utufikirie kutuletea vitendea kazi kama vile magari,” amesema.

“Kwa mfano, katika uchaguzi mdogo kule Kyela kulitokea vurugu lakini tukawa na changamoto ya magari. Mfano tunalo gari moja tu la washa washa, lakini pia kwa hapa Mbeya mjini pekee tuna kata 36 hivyo ukiangalia utaona changamoto ya magari iliyopo.”

Mkuu huyo wa mkoa amesema, “Na katika hili, tunaomba yale magari ambayo yapo bandarini na wenye nayo wameshindwa kulipa kodi basi watufikirie hata kutuletea Mbeya ili yaweze kutusaidia ili askari wetu waweze kufanya kazi ya kuzunguka kwa ufasaha zaidi tofauti na sasa askari anakaa sehemu moja, hii si nzuri kwanza si nzuri kwa usalama wake mwenyewe.”

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema  wamekuwa wakiendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ajali za barabarani na matukio mengine ya kiuhalifu.

Amesema katika utekelezaji huo, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari na kwa madereva kupimwa kiwango cha ulevi na leseni zao.

“Lakini changamoto tuliyonayo ni vifaa vya kupimia kiwango cha ulevi kwa dereva. Kwani utaratibu ni kwamba, kifaa kimoja kinapaswa kutumika kwa dereva mmoja tu, hivyo tumeishiwa, tunaomba ukatuombee,” amesema Matei.

Kamanda Matei amesema wameanzisha utaratibu wa askari kufanya kazi saa 24 barabarani na wamekuwa wakiweka doria na kusimamisha magari maeneo ya miteremko na magari yamekuwa yakipishana kwa zamu.

“Kwenye milima ya Mlima Nyoka, Igawilo, Lwambi- Mbalizi na ile ya Chunya, tunasimamisha magari, yanapita kwa zamu, gari ndogo za abiria na malori. Na hii tumeona faida yake kwani juzi tu hapa malori matatu yamegongana pale Mlima Igawilo na bahati nzuri yalikuwa yenyewe tu, hivyo tunaamini yangekuwapo na magari ya abiria kungekuwa na maafa,” amesema.