Lukuvi awaonya maofisa ardhi
Iringa. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusema siku zao za kuwarubuni wananchi zinahesabika.
Amesema kwa kiasi kikubwa, ufisadi unaofanywa na maofisa ardhi ndio chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi nchini.
Ameyasema hayo wakati akizunguza Mpangomji wa manispaa ya Iringa katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Lugalo.
Amesema mchezo huo wa ufisadi ambao umekuwa ukitumiwa miaka yote na maofisa ardhi nchini ameubaini na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutokubaliana na ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalam hao bila ya wao kufika maeneo husika na kuoneshwa maeneo hayo ili kujiridhisha.
Waziri Lukuvi amefichua kuwa ufisadi unaofanywa na maafisa ardhi nchini kwa kupima viwanja hewa kwa ajili ya maslahi yao na kusema kuwa mbinu ambayo wamekuwa wakiitumia kuiibia serikali amekwisha ibaini na hatakubali kuona mbinu hiyo inapewa nafasi katika serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli.
Lukuvi amesema kuwa wathamini nao pia wamekuwa wakiwapunja wananchi wasio na uelewa kwa kuwafanyia tathimini kubwa zaidi ya uhalisia wake.
“Wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam nilibaini ujanja wa wathamini baada ya eneo ambalo nyumba zake zina thamani kati ya shilingi milioni 20 hadi 50 kwa maana nyumba hizo ni za udongo ila maofisa hao walimtafuta mtu na kutafuta nyumba nzuri zaidi na kumshikisha kibao kisha kumpiga picha na kuandika kuwa nyumba hiyo inathamani ya zaidi ya milioni 200,” amesema.