Lukuvi aziagiza halmashauri zisimamishe mauzo ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Muktasari:

Ujenzi na mauzo hayo ni yanayofanyika katika maeneo yanayozunguka mji wa Serikali (eneo la Ihumwa) na Chamwino.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezielekeza halmashauri ya Manispaa Dodoma na ya Wilaya ya Chamwino kusimamisha ujenzi holela na mauzo yasiyo rasmi ya ardhi.

Ujenzi na mauzo hayo ni yanayofanyika katika maeneo yanayozunguka mji wa Serikali (eneo la Ihumwa) na Chamwino.

Katika tangazo alilolitoa Machi 28, Waziri Lukuvi alisema hatua hiyo inalenga kusubiri kukamilika kwa upangaji wa Mji wa Dodoma.

Alisema katika kutekeleza uhamishaji wa mji mkuu wa Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Serikali inafanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Dodoma (2010) ili kuendana na mahitaji halisi ya uhamishaji na fursa zingine za kiuchumi na kijamii.

Pamoja na mapitio ya Mpango Kabambe, alisema Serikali imeandaa mpango wa eneo la mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa.

“Kati ya eneo la Mji wa Serikali na Chamwino na eneo linalozunguka maeneo hayo kuna vijiji vya Msanga, Chahwa, Vikonje, Buigiri, Chamwino, Mahomanyika na Kikombo. Katika vijiji hivi kuna ujenzi holela na mauziano ya ardhi yasiyo rasmi unaoendelea,” alisema.

Waziri Lukuvi alisema kwa kuwa kazi ya kufanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Mji Mkuu Dodoma inaendelea, kuna umuhimu wa kusimamisha shughuli za uendelezaji ardhi katika maeneo hayo na maeneo yaliyo kwenye Tangazo la Serikali namba 912 la Juni 30 mwaka jana ili kupisha ukamilishaji wa kazi hiyo.

“Kama waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sekta ya ardhi, na katika kuzingatia kifungu cha 8 cha Sheria ya Ardhi Sura 113 na Kifungu cha 5 kikisomwa sambamba na kifungu cha 75 (a-c) cha Sheria ya Mipangomiji, Sura 355; nazielekeza Halmashauri ya Manispaa Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambazo ndiyo mamlaka za upangaji, kusimamisha ujenzi holela na mauziano yasiyo rasmi kusubiri kukamilika kwa upangaji wa Mji wa Dodoma,” aliagiza Lukuvi na kuwataka wananchi wa maeneo hayo kuzingatia maelekezo hayo.

Rais John Magufuli alitangaza Serikali kuhamia mjini Dodoma katika Sikukuu ya Mashujaa iliyofanyika kitaifa kwa mara ya kwanza mjini humo mwaka 2016 tangu nchi ipate uhuru.

Uamuzi huo uliitikiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetangaza ratiba ya Serikali kuhamia huko katika kipindi cha miaka mitano huku mwenyewe akionyesha mfano kwa kuhamia Septemba Mosi, 2016.

Pamoja na mawaziri wote, makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu wote na angalau idara moja au mbili ambao walianza kuhamia tangu Septemba hadi Februari mwaka jana.

Hata hivyo, Desemba mwaka jana, Majaliwa alisema Rais John Magufuli aliyekuwa ahamie Dodoma akiwa wa mwisho mwaka 2020 sasa atahamia wakati wowote mwaka huu.

Tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameshahamia mjini Dodoma.

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu alisema watumishi 2,346 kutoka wizara zote wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia Dodoma.