Lulu alivyogeuka kuwa malaika

Muktasari:

Unamkumbuka vizuri Elizabeth Michael ‘Lulu’? Vuta picha kamili ya kiumbe huyu pendwa miaka kadhaa nyuma. Akiiendesha Dar es Salaam anavyotaka. Kumbi za starehe zikimnyenyekea. 

Sinza Mori karibu na kituo kimoja cha mafuta, kulia kama unaelekea Mwenge. Kulikuwa na Super Market moja maarufu sana. Katika jengo hilo hilo kulikuwa na Pub flan hivi ya watoto wenye nyota kadhaa za urembo.

Siyo kwamba ilikuwa na vinywaji vitamu na vya tofauti. Hapana, tena bei yao ilikuwa juu kuliko Pub zilizojaa pale Sinza Mori. Mimi nilipapenda hapo na nilikuwa mhudhuriaji bora kwa sababu tu ya urembo wa wamiliki wa Pub hiyo.

Ndoto ya kuwamiliki ilitoweka lakini mazoea ya kutazama tabasamu zao yaliniteka. Sikuwahi kuthubutu kuwasaliti na kwenda kunywa sehemu nyingine. Wale wadada wametafuna pesa yangu. Mungu yupo atanilipia.

Jioni moja nikiwa hapo glasi ikaniponyoka (Lulu mbele yangu). Wakati mhudumu anatoa chupa zilizovunjika mimi macho yalikuwa kwa Lulu aliyeshuka kwenye gari peke yake akiingia Super Market. Siku ile ningekuwa bilionea ningemnunulia Super Market yote iwe yake milele.

Unamkumbuka vizuri Elizabeth Michael ‘Lulu’? Vuta picha kamili ya kiumbe huyu pendwa miaka kadhaa nyuma. Akiiendesha Dar es Salaam anavyotaka. Kumbi za starehe zikimnyenyekea. Pombe zikimtii na wanaume kapuku wakimuogopa. Achana na Lulu huyu unayemuona leo hii.

Mtoto mdogo mbichi mzuri. Tabasamu lake ni kama tiketi ya kwenda mbinguni. Hakika ukimtazama akicheka ni kama anakupa ‘trip’ ya peponi. Alikuwa mzuri kuliko uzuri wenyewe hata waliomrubuni hapo kabla wasamehewe, maana wengi tungetenda hilo kama tungepata ukaribu naye.

Ni aina ya wasichana ambao kama miaka yote ulizingirwa na ibilisi na kukana uwepo wa Mungu. Pindi ukutanapo na kiumbe wa aina yake kwa muda mfupi ungetambua uwepo wa Mungu. Kisha ungeokoka. Na hapo hapo ungekuwa mtumishi mwenye ‘mastazi’ ya unyenyekevu kwa Mungu baba. Acha. Katazame mpangilio wa meno ya Lulu, ni Mungu pekee anayeweza kuyapanga vile. Mchunguze tabasamu lake zaidi ya Yehova hakuna awezaye. Ni pamoja wa uchanganyaji rangi mpaka ikapatikana aliyonayo Lulu, ilifanywa na yule yule Baba wa Majeshi aliyemuumba Isaka na Yakobo kama siyo Herode na Sauli.

Kwa umaarufu wake mkubwa aliokuwa nao akiwa bado na umri mdogo vile, kazi hiyo ya kutoa nyota kali kama ya Lulu karakana na spana zake zipo kwa Mungu siyo shetani. Ogopa sana kupendwa toka utotoni mpaka ukubwani. Wapo waliopendwa ukubwani kabla hata ya ndoa nyota zimetoweka kama kifadulo.

Lulu? Labda Lulu mwingine ila siyo Elizabeth Michael huyu. Mtoto mdogo aliyebeba urembo wote anaostahili kuwa nao mwanamke. Kama haitoshi mtoto mdogo maarufu sana. Wasichojua wengi leo wajue ni kwamba pamoja na yote hayo kalikuwa kabinti kadogo kalikobarikiwa akili nyingi sana. Hata uwe mrembo vipi mwanaume mwenye akili zake hawezi kukwama au kuweka makazi ya kudumu kwenye mwili wa msichana mwemye akili chakavu. Walioweka kambi kwa Lulu hawakuwa maboya wala mabwege. Lulu ni aina ya wasichana ambao wanaweza kuiteka Dreamliner yetu kwa urembo unaochagizwa na akili nyingi.

Alipopata umaarufu ikaenda sambamba na kupata sifa ya mfano mbaya kwa watoto. Ingawa ilikuwa kwa muda mfupi, lakini Lulu alikuwa hafai mbele za wazazi, waandishi, jamii yote na serikali. Alipinda sana huku akiendekeza starehe na pombe. Kuna starehe na pombe. Yeye alibeba vyote ndani ya umri mdogo sana.

Matatizo ya sanaa kwa waigizaji, alikuwa mfano wa karibu sana kama mmoja wa wasanii wasiofaa. Taswira yake ilichafuka kwa kiwango kikubwa sana. Tukio la kifo cha Kanumba likazidi kumchafua zaidi kama mmoja wa binadamu uzao wa Eva asiyestahili msamaha. Hakuna aliyemuonea huruma zaidi ya wazazi wake na Dk Cheni. Ili ujue kuwa yupo duniani kwa makusudi ya Mungu baada ya dhamana yake kukubalika, ghafla akapindua meza na kugeuka shujaa wa sanaa na wasanii ambao walikuwa wamekata ringi wakati huo. Akazoa na tuzo katika vibaraza vya mama zake Van Vicker huko Lagos. Hata kesi yake ikasahaulika kabisa kwenye akili za watu.

Leo hii Lulu bado siku kadhaa awe huru kabisa akitumikia kifungo cha nje. Tayari amevikwa pete ya uchumba na mumewe mtarajiwa Majizzo. Mchizi ambaye amekuwa nyuma ya Lulu kwenye shida na raha kwa kipindi chote. Zawadi ya Lulu kwa Majizzo ni ndoa na faraja ya Majizzo kwa Lulu ni ndoa. Huu mtihani umewashinda dada zake wengi tena ambao hawajapitia hata nusu ya maswahibu yake. Lulu baada ya matatizo yote akatuliza akili kisha akajibrand na kujiengua na ngozi ovu ya awali na kuzaliwa upya. Leo kila mtoto wa kike hapa mjini anataka kuwa Lulu.

Kutoka mfano mbaya kwa wasichana, kageuka mfano bora kwa wasichana wote. Kuolewa ni jambo moja, kuolewa na mwanaume sahihi ni jambo la lingine. Hakuna mjingamjinga mwenye pesa zake wa kuvumilia mfungwa wa kike hapa mjini. Kwa lipi na madem wapo wengi kama wote?

Mjingamjinga mwenye pesa zake angempuuzia mbali kwenye nondo za jela huku akila bata na totoz amazing za mjini. Mchizi Majizzo akakomaa na mtoto mzuri, mpaka leo hii bado siku chache mtoto awe huru jumla. Waache waoane kwani shingapi?

Wakati Lulu akielekea kwenye dunia nyingine kabisa kwenye taratibu za kibinadamu, dada zake bado wanaishi maisha ya kufanya sherehe kubwa ya kuzaliwa. Anatumia mamilioni ya pesa akiwa hana mchongo wowote kwa sherehe za usiku mmoja. Wacha Lulu awe mfano bora kwa sasa. Siyo jambo dogo kwa binti aliyechukiwa kama muuaji wa kipenzi cha watu Steven Kanumba, leo hii akiwa bado ndani ya kifungo anaonekana mfano bora kwa wasichana wenzake. Pita popote uliza msichana yeyote anatakuambia anatamani awe kama Lulu.

Azam hawakuwa mabwege kumpa ubalozi wa shughuli zao za sinema. Wangempa nani na wengine wote kazi kubwa ni kugombea mabwana mjini? Wahindi pamoja na kukwama kibiashara lakini ukiwaonyesha sinema yenye sura ya Lulu wanaweza kulia. Lulu ni pesa. Kuwa Lulu ni majaaliwa siyo nguvu ya uchawi wala baraka za wachungaji. Kaumbwa hivyo na Mungu wake. Fuatilia tangu zamani, hajawahi kuwa na njaa njaa za kisanii. Na kama ni madanga ni wale wenye ‘aleji’ ya kutokosekana mkwanja mfukoni. Urembo ni moja na akili ni kitu kingine. Ogopa dem mwenye vyote hivyo.

Dada zake wanafanya biashara za kufanana. Wanaishi maisha ya kufanana. Na wana madanga yanayofanana. Ngwair, Sharomilionea na Kanumba wakifufuka leo kitu cha kushangaza kwao ni maisha ya Lulu wa sasa, lakini hayo mengine yote ni yale yale.

USHAURI

Kila unayemuoa au kuolewa ana udhaifu wake. Mungu pekee ndiye hana udhaifu. Hakuna mtu ambaye ni malaika, epuka kuchunguza mambo ya mtu ya nyuma samehe, sahau na songa mbele.

Ndoa haikosi changamoto

Ndoa sio kitanda cha maua yanayomeremeta kila muda, ndoa zote zenye mafanikio zimepitia misukosuko mingi.

Hatuwezi kuwa sawa, kuna watakaokuwa mbele kidogo na watakaokuwa nyuma kidogo.

Ukishaoa au kuolewa ni kuingia katika uwanja wa mapambano. Kuwa tayari kupambana kuulinda ukanda wa ndoa yako. Hakuna ndoa ambayo imetimilika. Ndoa ni kazi ngumu, jitolee mwenyewe na ufanye kazi ya kuijenga ndoa yako iwe kamilifu.

Mungu atakupa mtu ili wewe umtengeneze jinsi wewe unavyohitaji yeye awe. Huwezi jua nini kitatokea baada ya ndoa, hali inaweza badilika, hivyo achia nafasi ya marekebisho.

Hakuna mapenzi rahisi katika ndoa, huwezi kupenda au kupendwa bila kujitoa nafsi yako kwa dhati. Kama mtihani mikubwa ya dunia tena akiwa katika umri mdogo ameivuka ndoa hawezi kumshinda. Lulu ni kama kibaka aliyegeuka Malaika.