Lusinde: Kusalimiana na Malecela ni kama mbingu zimefunguka

Mbunge wa Mtera Livingston Lusinde (kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, John Malecela wakati wa sherehe za uzinduzi wa majengo  ya Taasisi ya Elimu ya Afya Mvumi mkoani Dodoma juzi. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

  • Lusinde ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kukutana na kupeana mkono na Malecela mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya, Mvumi. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Chamwino. Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde amesema kitendo cha kusalimiana na kupeana mkono na waziri mkuu wa zamani, John Malecela baada ya miaka minane ni kama mbingu zimefunguka kwake.

Lusinde ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kukutana na kupeana mkono na Malecela mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa majengo ya Taasisi ya Elimu ya Afya, Mvumi. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akiwa katika hafla hiyo, Lusinde (CCM) maarufu kama Kibajaji, alimweleza Waziri Mkuu kuwa anajisikia mwenye furaha zaidi baada ya kuishi kwa miaka minane bila ya kusalimiana na Malecela ambaye pia alikuwa mbunge wa Jimbo la Mtera kabla ya kuchukuliwa na Lusinde mwaka 2010.

Malecela na Lusinde walikutana katika siasa za kugombea Jimbo la Mtera kwa mara ya kwanza mwaka 2005 wakati huo Lusinde akigombea kupitia Chadema lakini katika hatua za mwisho Lusinde alijitoa na Malecela akashinda.

Mara ya pili ilikuwa ni mwaka 2010 safari hii Lusinde akiwa Katibu wa CCM wilaya ya Tarime mkoani Mara na alimshinda Malecela katika kura za maoni na baadaye wakati wa uchaguzi alishinda na kuwa mbunge wa Mtera.

Mwaka 2015, Lusinde alichuana na mtoto wa Malecela, Samuel Malecela katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM na Lusinde akashinda na hatimaye kuwa mbunge kwa awamu ya pili.

“Nakushukuru sana Waziri Mkuu kwani ujio wako leo nimeweza kusalimiana na Mzee Malecela kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane, sisi ni Wakristo na lazima tuwe wa kweli,” alisema Lusinde mbele ya hadhara hiyo.

Baadaye akizungumzia tukio hilo katika mahojiano na Mwananchi, Lusinde alisema tangu siku walipopeana mkono na Malecela amekuwa ni mtu mwenye furaha kubwa na ameahidi kuchukua hekima kutoka kwa mzee huyo.

“Lakini juzi kwa kweli alikuwa mwenye furaha, naamini hata yeye ameyafuta moyoni mwake, ndiyo maana nasema kuwa ni muhimu kwangu mimi kumtumia hasa kuchota busara na kuomba ushauri katika mambo ya kimaendeleo,” alisema Lusinde.

Alisema kuwa Malecela alimlea vyema katika hatua zote, lakini kipindi chote hicho wamekuwa watu wasiokuwa na salamu wala mazungumzo ya aina yoyote kuhusu maendeleo ya jimbo lao.

Vuguvugu na mzozo wao ulianza kabla ya uchaguzi wa 2010 kwani Lusinde alikuwa wa kwanza kuzungumza na vyombo vya habari akidai kuwa Mzee Malecela alipanga kumuachia jimbo hilo.

Hata hivyo kauli hiyo ilikanushwa na wasaidizi wa Malecela wakieleza kuwa hakukuwa na maafikiano ya aina hiyo.

Lusinde alisema mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, alikutana na Malecela zaidi ya mara mbili katika ofisi za chama na kila alipojaribu kumsalimia aliona mwenzake hakuwa na mpango naye hivyo na yeye akaamua kuacha.

Kuhusu mtoto wa Malecela ambaye aligombea naye mwaka 2015, alisema hakuwa na shida naye kwani walifanya kampeni za kibabe kwa pamoja ukizingatia wote ni vijana.

“Hata baada ya uchaguzi tulikuwa kitu kimoja na tutaendelea kuwa wamoja katika kuwaungaisha wananchi wa Mtera,” alisema.

Kuhusu hofu ya Malecela kurudi jimboni, alisema hana shaka kwani mzee huyo sasa amekuwa ni mtu wa kutoa ushauri zaidi katika mambo mengi ya taifa na kimataifa hivyo kurudi kugombea ubunge huenda haitakuwa ndoto yake ingawa alisema mtoto wake, Samule Malecela anaweza kugombea.

“Hata hivyo nitamshinda tena.” alisema.