Maabara ya Lancet yakabidhiwa cheti cha ubora

Mkurugenzi Mtendaji wa Maabara ya Lancet (Afrika Mashariki) Dk Ahmed Kalebi (Kushoto) akisoma maneno yaliyoandikwa kwenye cheti ya kimataifa cha ubora wa maabara walichotunikiwa baada ya kukaguliwa na kuthibitishwa kuwa wanazingatia viwango vya kimataifa.

Muktasari:

Maabara zenye kukidhi vigezo na viwango zinasaidia kupunguza uwepo wa makosa kwenye vipimo na kusababisha utata.

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Afya imeahidi kuendelea kuzifanyia ukaguzi maabara zote nchini kuhakikisha zinatoa huduma kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa.

Kaimu Msajili wa Maabara, Ednanth Gareba ameyasema hayo leo  Jumatano, Julai 26 wakati akikabidhi cheti cha kimataifa cha ubora kwa maabara ya Lancet.

Maabara hiyo imetunikiwa cheti cha ubora cha ISO15189:2012 kilichotolewa na mkaguzi wa maabara katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADCS).

Amesema uwepo wa maabara zenye kukidhi vigezo na viwango kunasaidia kupunguza uwepo wa makosa kwenye vipimo na kuleta utata.

Amesema kwa hatua waliyofikia Lancet ni muhimu maabara nyingine kuiga mfano huo kwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa.

"Wenzetu wamefanya vizuri kiasi cha kuwavutia wakaguzi wa kimataifa, cheti walichopata si cha mchezo, wengine tunapaswa kujifunza ili tufikie hatua hiyo,"amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lancet Afrika Mashariki, Dk Ahmed Kalebi amesema ni heshima kubwa kwa maabara hiyo kuwa ya kwanza binafsi kuthibitishwa kwa cheti hicho cha ubora.

"Tunajivunia huduma zetu zimetufanya kuwa maabara ya kwanza binafsi Tanzania kupata tuzo hii, tunaahidi kuendelea kufanya kazi nzuri na kuzingatia viwango ili heshima hiyo iendelee kuwepo," amesema

Mtaalam kutoka maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Martha Edward amesema mara kadhaa Lancet imekuwa ikitoa msaada pindi baadhi ya vipimo na vitendanishi vinapokosekana hospitalini hapo.

"Tunatambua ubora wa huduma zao ndio sababu tunashirikiana nao, tunapokosa vipimo au mashine kuharibika wanakuwa tayari kutusaidia na majibu yao ni ya uhakika,”amesema.