Maagizo ya Waziri Mkuu kwa Dk Slaa, Mboweto

Muktasari:

Majaliwa aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na utalii na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na mabalozi wapya; Dk Willbrod Slaa na Muhidin Mboweto kisha akawaambia watumie mbinu za kidiplomasia kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali.

Majaliwa aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na utalii na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Pia aliwataka mabalozi hao wakaimarishe diplomasia kwa lengo la kuzifanya nchi wanazoenda ziendelee kushirikiana na Tanzania katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Dk Slaa anayeiwakilisha Tanzania nchini Sweden na Mboweto anayekwenda Nigeria walikutana na Waziri Mkuu jana katika makazi yake jijini Dar es Salaam.

Majaliwa aliwaambia kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwemo fukwe za bahari zinazoanzia Tanga hadi Mtwara, maziwa na mito na hifadhi za wanyama hivyo ni vyema wakajielekeza katika kuvutia wawekezaji kwenye sekta hiyo ili Taifa lipate watalii wengi.

Alisema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya madini, viwanda na masoko ili wafanyabiashara na wakulima waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Tumejiimarisha katika mazao ya chakula na biashara, hivyo tunatakiwa kuwa na uhakika wa masoko kwenye kilimo ili mkulima anapozalisha pamba, tumbaku, kahawa, chai, korosho, dengu pamoja na mazao mengine tuwe na mahali pa kuuza, kwa hiyo washawishini wafanyabiashara kuja kununua,” alisema.

Kwa upande wao, mabalozi hao waliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazokwenda.