Maajabu mengine matokeo kidato cha sita mwaka huu

Wanafunzi wa Shule ya Feza Boys’ wakiwa wamembeba mhitimu wa shule hiyo Amour Aly alieshika nafasi ya nne katika wanafunzi kumi waliofanya vizuri kiujumla, kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita wa mwaka 2018. Picha na Omar Fungo 

Muktasari:

Shule bora zilizofanya vizuri kitaifa kutoka Dar es Salaam ni Feza Boys, Feza Girls na Canossa.


Dar es Salaam. Kama ni kuvuta soksi, basi tunaweza kusema mikoa ya Simiyu na Manyara, imeivuta kwelikweli. Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yanaonyesha kuwa mikoa hiyo imepaa.

Katika orodha ya matokeo hayo kimikoa, Mtwara imeongoza kwa kufanya vizuri nchini, lakini Simiyu imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mikoa mingine kwani imepanda hadi nafasi ya 10 kutoka ya 26 mwaka jana.

Kadhalika, Mkoa wa Manyara umeshika nafasi ya tisa kitaifa kutoka nafasi ya 24 mwaka jana.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka hakuficha furaha yake kutokana na matokeo hayo, na katika ukurasa wake wa Facebook ameandika, “Kambi kitaifa kitaaluma Simiyu: Kama mkoa mwaka jana tulikuwa nafasi ya 26 kitaifa, mwaka huu tumekuwa nafasi ya 10, ufaulu kwa daraja la 1, 2, 3 umeongezeka, sifuri zimepungua.”

Aliwapongeza walimu kwa moyo wa kujitolea kuwasaidia wanafunzi na wanafunzi wenyewe kwa kuzingatia maarifa waliyopewa na hakuwaacha wazazi kwa kuwa kichocheo kwa watoto wao.

“Zaidi nawapongeza na kuwashukuru kwa dhati viongozi wenzangu wote wa Serikali, kisiasa na kidini, kuanzia ngazi ya ubalozi, kijiji, kata, wilaya na mkoa kwa kuibeba elimu kama ajenda kuu ya mapinduzi ya kiuchumi ndani ya mkoa wetu,” alisema Mtaka.

Mkoa mwingine ni Tabora ambao umeshika nafasi ya nane kutoka ya 18 mwaka jana. Arusha nao umepanda kutoka nafasi ya 21, hadi nafasi ya 12 mwaka huu na Mkoa wa Tanga ulioshika nafasi ya tano kutoka ya 13.

Mtwara, Lindi na Geita imeendelea kushika nafasi tatu za juu. Mtwara imebadilishana nafasi ya kwanza na ya tatu na Geita wakati Lindi imeendelea kushika nafasi ya pili.

Akizungumzia matokeo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,  Gelasius Byakanwa alisema yametokana na mkakati wa kumaliza silabasi mapema na kufanya mitihani mingi ya majaribio.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mkoa wetu kushika nafasi ya kwanza. Nawashukuru walimu na wanafunzi kwa kufanya vizuri. Tumekuwa na mkakati wa kumaliza silabasi mapema na kufanya mitihani mingi ya majaribio kwa ngazi za darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita,” alisema Byakanwa.

Hata hivyo, alisema matokeo hayo hayatakuwa na maana ikiwa yale ya kidato cha nne yatakuwa mabaya, hivyo aliwataka walimu na wanafunzi kuvuta soksi.

“Matokeo haya yatashajihishwa na matokeo mazuri ya darasa la saba na kidato cha nne. Wanafunzi wengi wa kidato cha sita wanatoka mikoa mingine, hivyo wanafunzi wanaotoka mikoa hii kwenye vidato vya chini lazima wajitahidi,” alisema na kuongeza:

“Tunazo shule za kidato cha tano na sita 11 tu na zote hazina daraja sifuri. Nimewaandikia walimu wangu wajitahidi kuimarisha nafasi hiyo ili tusiwe na sifuri kabisa.”

Mkoa wa Pwani ulioshika nafasi ya 19 kitaifa ndiyo unaoongoza kwa kutoa shule nne katika shule 10 bora zilizofanya vizuri kitaifa  huku Sekondari ya Kibaha ikiwa ya kwanza, ikifuatiwa na Marian Girls, Marian Boys na Ahmes.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa mikoa hiyo, katika mpangilio huo, Mkoa wa Dar es Salaam wenye shule mbili zilizoongoza kitaifa umeshika nafasi ya nne kutoka mwisho.

Shule bora zilizofanya vizuri kitaifa kutoka Dar es Salaam ni Feza Boys, Feza Girls na Canossa.

Sekondari kongwe ya Jangwani ni miongoni mwa shule zilizouangusha mkoa huo katika matokeo hayo kwani ilikuwa katika kundi la shule 10 zilizofanya vibaya kitaifa ikishika nafasi ya tatu kutoka mwisho.

Tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo ameitembelea na kumwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kufanya mabadiliko ya uongozi wa shule hiyo na kubadilisha walimu.

Mikoa mingine iliyofanya vibaya kulingana na  matokeo ya mwaka 2017 ni Mara uliotoka nafasi ya nne mwaka jana hadi nafasi ya 25 mwaka huu.

Hata hivyo, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mara, Emmanuel Kisongo alisema haukufanya vibaya bali inategemea na kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine (mobility) ya ufaulu.