Maalim Seif: Niko tayari kukutana na Rais Magufuli

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

Mwanza. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema ufunguo wa utatuzi wa mgogoro na kukwama kisiasa Zanzibar uko mikononi mwa Rais John Magufuli.

Amesema kutokana na nafasi ya Rais katika utatuzi wa mgogoro huo, yuko tayari muda wowote kukutana naye kujadili na kutafuta muafaka kwa kuwa hali iliyopo inachangia uhasama wa kijamii na kuharibu uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, wakati wa kipindi cha Tujadiliane kinachoandaliwa na Umoja wa Klabu ya Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Maalim Seif alisema msimamo wao wa kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein unatokana na alichodai uchaguzi uliomweka madarakani haukuwa halali.

Alisema hayuko tayari kujadiliana na Dk Shein akidai hana uwezo wa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

“Mwenye ufunguo wa mgogoro huu ni Rais Magufuli. Kutokana na kutambua hilo, nimeomba mara kadhaa kukutana na Rais bila mafanikio,” alisema.

Maalim Seif alisema hata barua alizomwandikia Rais hazijawahi kujibiwa.

Katibu huyo aliyekuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari alisema hajawahi kukaa vikao vya siri na Dk Shein.

“Hayo ni maneno ya mitaani, si kweli na wala siwezi kukutana na Dk Shein ambaye hata mkono wenyewe sikumpa,” alisema.

Kuhusu iwapo atawania urais wa Zanzibar uchaguzi wa 2020, Maalim Seif hakuweka wazi msimamo wake huku akisema kwa mujibu wa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, nafasi hiyo inatakiwa kuwaniwa na mtu mwenye umri wa kati ya miaka 45 hadi 70, umri ambao tayari ameuvuka.

Mgogoro na Profesa Lipumba

“Siwezi kukutana wala kukaa meza ya majadiliano na msaliti, dhambi ya usaliti haivumiliki,” alisema Maalim Seif akijibu swali kuhusu uwezekano wa kumaliza mgogoro ndani ya CUF kwa njia ya majadiliano.

Alisema mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa kupandikiza mgogoro ndani ya chama hicho.