Maalim Seif amtega Profesa Lipumba mahakamani

Maalim Seif.

Dar es Salaam. Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF), kambi ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba imemwandikia barua Jaji Wilfred Dyansobera ikimtaka ajiondoe kwenye kesi zote za chama hicho.

Jaji Dyansobera pekee anasikiliza kesi zipatazo 13 za chama hicho zilizofunguliwa na bodi ya wadhamini upande wa kambi ya katibu mkuu, Maalim Seif.

Kesi nyingi zimefunguliwa dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, msajili, Profesa Lipumba na baadhi ya wanachama wakiwamo viongozi wanaomuunga mkono Lipumba na nyingine dhidi ya mwenyekiti huyo na wenzake.

Hata hivyo, bodi ya kambi ya Maalim Seif ambayo ndiyo iliyofungua kesi hizo kupitia kwa wanasheria wake, Juma Nassoro na Daimu Halfani imeiwekea mtego bodi ya kambi ya Profesa Lipumba baada ya kuiwekea pingamizi, huku ikiipa masharti maalumu.

Awali bodi hiyo ya Profesa Lipumba iliandika barua moja ambayo inamtaka Jaji Dyansobera ajiondoe katika kesi zote.

Wakati mawakili wa pande zote walipoitwa mahakamani hapo ili mahakama isikilize hoja za bodi hiyo ya Profesa Lipumba, wale mawakili wa bodi ya Maalim Seif walipinga bodi ya Profesa Lipumba kutumia barua moja kumtaka Jaji Dyansobera ajiondoe kwenye kesi zote. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mawakili hao Nassoro na Halfani walidai kuwa waombaji hao katika barua yao hawajaainisha sababu za kumtaka jaji ajiondoe kwenye kesi hizo na kwamba barua hiyo imeandikwa kiujumlajumla.

Walisisitiza kuwa haiwezekani kutumia barua moja kumtaka jaji kujiondoa katika kesi zote hata ambazo hazijatajwa kwenye barua hiyo, badala yake walipendekeza waombaji hao waandike barua tofautitofauti kwa kila kesi na kuainisha sababu ili mahakama iweze kuzipima.

Wakili wa bodi ya Profesa Lipumba, Mashaka Ngole alipinga pamoja na mambo mengine akidai kuwa barua hiyo imeandikwa na wateja wake ambao si wanasheria, iko sawa huku akisisitiza kuwa inahusu kesi zote anazozisikiliza jaji huyo.

Hata hivyo, Jaji Dyansobera alikubaliana na hoja za mawakili wa bodi ya Maalim Seif na kuielekeza bodi ya Profesa Lipumba kufanya marekebisho kwenye barua yake hiyo kwa kuandika barua kwa kila kesi ili ziweze kuwekwa kwenye majalada ya kesi husika.

Kwa maana hiyo bodi ya Profesa Lipumba inapaswa kuandika jumla ya barua 13 huku wakitakiwa kubainisha sababu za kumtaka jaji huyo ajiondoe kwenye kesi hizo. Kwa mujibu wa Wakili Daimu, sababu zinazoweza kumfanya jaji akajiondoa kwenye kesi ni mwenendo wake mbaya katika uendeshaji kesi hizo, jambo ambalo bodi hiyo inapaswa kuainisha kwa kila kesi ni namna gani jaji amekuwa na mwenendo wa aina hiyo.

Hata hivyo, wakati bodi hiyo ya Profesa Lipumba ikimtaka Jaji Dyansobera kujiondoa kwenye kesi hizo, bado kuna utata wa bodi ipi ni halali kati ya hiyo ya Profesa Lipumba na ile ya awali ya Maalim Seif, ambao hadi sasa haujapatiwa ufumbuzi.

Utata huo wa bodi ipi ni halali inayopaswa kuendesha kesi hizo, uliibuka baada ya bodi hiyo mpya kuwasilisha mahakamani hapo barua kuwaondoa mawakili waliokuwa wakiendesha kesi hizo kwa niaba ya bodi ya awali na kuwatambulisha mawakili wapya na nia ya kuzifuta kesi hizo.

Mawakili wa bodi ya awali walipinga kujiondoa wakidai kuwa hawajapata maelekezo ya kuwaondoa katika kesi hizo kutoka kwa mteja wake waliyeingia naye mkataba na wakaiomba mahakama hiyo ifanye uchunguzi kwanza kujua ni bodi ipi halali.

Mbali na pingamizi hilo, pia mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh amefungua kesi akihoji uhalali wa bodi ya Profesa Lipumba iliyosajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), ambayo bado haijatolewa uamuzi.