Maaskofu KKKT watoa waraka mzito

Muktasari:

  • Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

 Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limetoa waraka mzito wa ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka ambao mbali ya kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini wake “ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.”

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

“Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya salamu za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake,” inasema sehemu ya waraka huo.

Salamu hizo za Pasaka zimetokana na kikao cha maaskofu hao kilichofanyika Machi 15 na waraka huo umepangwa kusomwa leo katika makanisa yote ya KKKT nchini.

Huo ni waraka wa pili kutoka kwa viongozi wa dini baada ya Februari mwaka huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kutoa ujumbe wa Kwaresma uliosaniwa na maaskofu 35 uliozungumzia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Alipotafutwa kutoa maoni kwa niaba ya Serikali kuhusu waraka huo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alijibu kwa kifupi; “Ujumbe huu unahusu Pasaka. Tunawatakia Pasaka njema.”

Mkuu wa KKKT, Dk Frederick Shoo alipoulizwa jana juu ya waraka huo alisema asingependa kuuzungumzia kabla haujasomwa akidokeza kwamba anachofahamu ni kuwa leo katika sharika zote za kanisa hilo nchini kutasomwa waraka wa maaskofu wa kanisa hilo.

“Nijuavyo Jumapili kesho (leo) kwenye nyumba za ibada zote kutasomwa Waraka wa Pasaka kutoka Maaskofu wa KKKT. Sitaki kuuzungumzia kwa sasa mpaka usomwe,” alisema Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.

Siasa na Jamii

Maaskofu hao wameipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi wakisema wameshuhudia nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima.

“Tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii,” unasema waraka huo na kuitaka Serikali kutambua kwamba sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo na si washindani wa Serikali katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya Serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Pia ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu, jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za biashara,” unasema waraka huo.

Maaskofu hao wamesema mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza makusanyo na kujenga ushawishi wa rushwa.

Kuhusu hali ya uchumi wa viwanda, maaskofu hao wameshauri uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini na kwamba kilimo na ufugaji vihusishwe katika viwanda.

Maisha ya Siasa

Waraka wa maaskofu hao pia ulichambua hali ya kisiasa nchini na kusema; “Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu.

“Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii, bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.

“Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na Bunge huru lililo sauti ya wananchi.

Wamesema wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya Bunge na kwamba chombo hicho hakisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yeyote.

Wameeleza kwamba kwa umoja wao na kwa nyakati za hivi sasa kuna matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea Taifa inayoshuhudiwa; “Baadhi ya matukio hayo ni hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.”

Pia wanasema kumekuwa na kupungua kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari na kuelezea hofu yao kuwa hali ikiendelea hivyo hata uhuru wa kuabudu unaweza kuwa shakani.

Pia wameelezea kuwapo kwa dalili za kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama na Tume ya Uchaguzi na kile walichodai kuwa ni kudhoofishwa kwa Serikali za Mitaa wakisema kumekuwa na mazingira kukosekana kwa haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali wakisema zipo ambazo zimegubikwa na ubabe, vurugu, hila na vitisho.

Wametaja pia kuwapo kwa dalili za utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi na kuonya kuwa hatua hiyo itaimarisha ubaguzi wa kiitikadi na kukuza migawanyiko.

“Udhalilishaji wa kauli njema isemayo “Maendeleo hayana chama”. Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzulu chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali,” unasema waraka huo na kusisitiza kuwa mambo hayo ni tishio kwa umoja na amani ya nchi.

Masuala Mtambuka

Katika masuala mtambuka maaskofu hao wanasema, “Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini.”

Wametaja baadhi ya masuala hayo waliyoeleza kuwa yanagusa maisha ya watu kwa njia nyingi kuwa ni pamoja na mfumo wa elimu na kusema, “Elimu ni kitovu cha ustawi wa Taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.

“Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na ubaguzi kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa Serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za Serikali.”

Mbali ya elimu waligusia suala la usimamizi wa sheria na utoaji haki na kuvitaka vyombo husika vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana.

“Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo,” unaeleza waraka huo.

Waraka huo haukuacha kuzungumzia suala la Katiba Mpya. Unasema mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano yatadumu iwapo kutakuwa na Katiba Mpya.

“Kiongozi mzalendo si mbadala wa Katiba Mpya na Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote za dini, makabila na makundi yote chini ya Katiba Mpya.”