Prime
Kilio cha upinzani DRC Mwendelezo wa ukandamizaji Afrika, wadau wataja mwarobaini
Barani Afrika, siasa za vyama vingi zimekuwa zikisukuma simulizi mbili zinazogongana; ndoto ya demokrasia shirikishi na uhalisia wa mamlaka zinazotegemea nguvu za dola.
Katika mataifa mengi, upinzani umekuwa si chombo cha kushindana kisiasa kwenye uchaguzi, bali taasisi inayopitia misukosuko mingi ya kidemokrasia na mivutano na mifumo ya dola.
Tukio la hivi karibuni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako kiongozi wa upinzani, Martin Fayulu alijeruhiwa wakati wa maandamano ya kupinga mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaodaiwa kufungua njia ya kuongeza muda wa Rais Félix Tshisekedi kubaki madarakani, limefufua tena mjadala wa bara zima kuhusu matumizi ya nguvu katika siasa za Afrika.
Ingawa Serikali ya DRC imesisitiza kuwa hatua zake zinalenga kudhibiti vurugu na kulinda utulivu wa taifa, upinzani unaona kilichotokea kama mwendelezo wa kuinyamazisha sauti mbadala za kisiasa kwa nguvu za dola.
Lakini simulizi hii si ya DRC pekee. Ni picha inayojirudia katika nchi nyingi za Afrika, mifano ipo karibu kila mahali, ikiwamo Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Rwanda na Ethiopia, ambako migogoro kati ya upinzani na dola imeendelea kuwa sehemu ya maisha ya kisiasa ya bara hili.
Kiongozi wa upinzani wa Congo DR, Martin Fayulu, anaendelea kupitia kipindi kigumu cha kisiasa kinachochangiwa na mivutano ya muda mrefu kati yake na Serikali ya Rais Félix Tshisekedi.
Moja ya maumivu makubwa anayobeba ni madai yake ya kuporwa ushindi wa urais wa mwaka 2018, ambapo amekuwa akisisitiza kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi lakini hakutangazwa mshindi.
Pia, amekuwa akilalamikia kuwekewa vikwazo mbalimbali ikiwamo kuzuiwa kwa baadhi ya shughuli za kisiasa za chama chake kutokana na mvutano wake na Serikali ya Tshisekedi.
Amekuwa akidai kuwa upinzani nchini humo unakabiliwa na ukandamizaji unaolenga kunyamazisha sauti zinazopinga Serikali.
Ni vilio kila kona
Nchini Tanzania, simulizi ya maumivu ya viongozi wa upinzani imeendelea kuzungumziwa kupitia tukio la Septemba 7, 2017, pale Mwenyekiti (wakati huo Makamu Mwenyekiti) wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akiwa mbunge, aliposhambuliwa kwa risasi nyumbani kwake mjini Dodoma.
Tukio hilo lilimuacha katika hali mbaya kiafya na kulazimika kupata matibabu ya muda mrefu nchini Kenya na baadaye Ubelgiji.
Japo waliohusika na tukio hilo hawajawahi kufahamika, hadi leo shambulio hilo limeendelea kuwa moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya siasa za Tanzania na limeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa na mazingira ya ushindani wa kisiasa nchini.
Baada ya hapo, Tanzania imeendelea kushuhudia msururu wa kukamatwa kwa viongozi wa upinzani ambapo hadi sasa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anashikiliwa gerezani akikabiliwa na mashitaka ya uhaini mahakamani.
Aidha, mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Freeman Mbowe alikamatwa Julai 2021 na kushtakiwa kwa ugaidi katika kesi iliyodumu kwa miezi kadhaa kabla ya kuondolewa.
Nchini Uganda, kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye amekamatwa mara nyingi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili, hasa wakati wa uchaguzi au maandamano ya kisiasa.
Hadi sasa kiongozi huyo anaendelea kushikiliwa gerezani nchini humo akikabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kijeshi nchini humo.
Naye mwanamuziki na mwanasiasa, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, mpinzani wa sasa wa Rais Museveni, amekamatwa mara kadhaa, kupigwa wakati wa maandamano na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali ya kisiasa.
Katika hali inayoonyesha kuwa tatizo hili ni la bara zima, huko Zambia, Rais wa sasa Hakainde Hichilema, kabla ya kuingia madarakani, alikamatwa mwaka 2017 na kushtakiwa kwa uhaini baada ya msafara wake kushindwa kumpisha Rais wa wakati huo, Edgar Lungu.
Alikaa gerezani kwa siku 127 kabla ya kuachiwa na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo. Hata hivyo, Rais wa zamani, Lungu alijikuta mpinzani wa aliyekuwa mpinzani wake, mwili wake umeendelea kuibua utata ukikaa zaidi ya miezi 10 bila kuzikwa baada ya kifo chake mwaka jana.
Zimbabwe pia imeendelea kuwa na simulizi ya migongano kati ya dola na upinzani. Chama cha Citizens Coalition for Change (CCC) kimekuwa kikilalamikia kukamatwa kwa wanachama wake, kuzuiwa kwa mikutano na kile kinachodai ni matumizi ya dola kudhibiti ushindani wa kisiasa.
Rwanda nayo imekuwa ikitajwa mara kwa mara katika mijadala ya kisiasa barani Afrika baada ya mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire kukamatwa mwaka 2010 na baadaye kufungwa kabla ya kupewa msamaha wa Rais mwaka 2018 na kuendelea na misukosuko kila msimu wa uchaguzi wa Rais nchini humo.
Kwanini Afrika ni tofauti?
Migogoro ya kisiasa ipo katika mabara yote duniani. Hata hivyo, Afrika imeendelea kujitokeza kwa kiwango kikubwa cha malalamiko kutoka kwa upinzani kuhusu kukamatwa, majeraha, kufunguliwa kesi au kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa.
Katika historia za Ulaya imepitia maandamano makubwa ya kisiasa. Ufaransa ilishuhudia maandamano ya kupinga mageuzi ya pensheni, Uingereza imepitia migawanyiko ya Brexit na Hispania imepitia vuguvugu la kujitenga kwa Catalonia.
Lakini ni nadra kusikia viongozi wa upinzani kukamatwa mara kwa mara kila uchaguzi unapokaribia au kufunguliwa kesi zinazotafsiriwa kisiasa.
Huko Marekani, uchaguzi wa mwaka 2020 ulisababisha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na hata vurugu katika Bunge la Congress, lakini taasisi zake ziliendelea kufanya kazi na mabadiliko ya madaraka yalifanyika kupitia taratibu za kikatiba.
Katika nchi nyingi za Asia kama Japan na Iran, mivutano ya kisiasa ipo, lakini taasisi za uchaguzi, mahakama na mifumo ya kikatiba imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kusimamia ushindani wa kisiasa.
Mzizi wa tatizo upo hapa
Kwa mujibu wa wachambuzi, tofauti kubwa ya Afrika ipo katika uimara wa taasisi. Wanasema katika nchi nyingi za Afrika, taasisi bado zinapambana kujijenga ili zisimamie ushindani wa kisiasa bila kuonekana zinatumiwa na upande mmoja.
Mchambuzi wa siasa na utawala bora wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda anasema maumivu ya upinzani barani Afrika hayawezi kutenganishwa na kile anachokiita utamu wa madaraka.
Kwa mujibu wake, madaraka katika nchi nyingi za Afrika yameendelea kuwa chanzo kikubwa cha ushawishi wa kisiasa, kiuchumi na hata kijamii, hali inayowafanya walioko madarakani kuwa wagumu kuviachia au kukubali ushindani wa kisiasa unaoweza kuhatarisha nafasi zao.
“Tatizo kubwa zaidi ni kwamba taasisi nyingi za kisiasa na kikatiba katika bara hili bado hazijajengeka kwa kiwango cha kuweza kuzuia matumizi mabaya ya madaraka,” anasema.
Dk Mbunda anafafanua kuwa matokeo yake, kila upinzani unapokuwa na nguvu na kuonekana kuwa tishio la kisiasa, hujikuta ukiingia kwenye msuguano na dola kupitia kesi mahakamani, kukamatwa kwa viongozi wake, kuzuiwa kwa mikutano au wakati mwingine matumizi ya nguvu katika maandamano.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa za Afrika, Dk Azaveli Lwaitama anaona vilio vya upinzani kama kiashiria kikubwa cha matatizo ya utawala katika bara hili.
Kwa maoni yake, mara nyingi wapinzani hujikuta wakikumbana na misukosuko kwa sababu wamekuwa sauti za kukemea matatizo yanayowakabili wananchi.
Anasema pale serikali zinaposhindwa kushughulikia changamoto za kiuchumi, ukosefu wa ajira, gharama kubwa za maisha au malalamiko ya utawala, mara nyingi ni vyama vya upinzani vinavyojitokeza kuzungumzia matatizo hayo.
Hali hiyo huweka upinzani katika mgongano wa moja kwa moja na wenye mamlaka.
“Vilio vya upinzani kwa kiwango kikubwa ni vilio vya wananchi. Wapinzani wanapopaza sauti kuhusu matatizo ya wananchi, mara nyingi wao ndio huonekana kuwa tatizo badala ya matatizo wanayoyazungumzia,” anasema.
Dk Lwaitama anasema chanzo kingine kinachochochea migogoro ya kisiasa katika Afrika ni tabia ya baadhi ya viongozi kubadilisha katiba au misingi muhimu ya kisheria ili kutimiza malengo ya kisiasa ya muda mrefu.
Mwarobaini wake huu hapa
Wakati katika mataifa mengi, vilio vya upinzani vinaendelea kusikika, wachambuzi wanaamini mwarobaini wake haupo kwenye matumizi makubwa ya nguvu, bali katika kujenga taasisi imara, kuheshimu katiba, kuimarisha uchaguzi.
Wanasema, jamii na mamlaka za dola zinapaswa kukubali kuwa katika demokrasia, upinzani si adui wa taifa, bali ni sehemu muhimu ya uhai wa mfumo wa kisiasa wenyewe.
“Vilio vya upinzani vina mwisho. Lakini hakuna siku ambayo kiongozi atasema wapinzani chukueni nchi mjaribu kidogo. Haki hailetwi kwenye sahani. Ni lazima vyama vipambane kuelimisha wananchi, kudai katiba bora, mifumo bora ya uchaguzi na kupata uungwaji mkono wa wananchi,” anasema Dk Mbunda.
Kwa mujibu wake, historia ya Afrika imeonyesha kuwa mabadiliko ya kisiasa hayajawahi kupatikana kwa urahisi, bali kupitia mapambano ya muda mrefu ya kisiasa, kujenga taasisi imara na kupata ridhaa ya wananchi.
Anasema mifano ya Zambia na Malawi inaonyesha kuwa upinzani unaweza kufanikiwa kuingia madarakani pale unapojenga uungwaji mkono wa wananchi na taasisi za uchaguzi zinapokuwa na kiwango fulani cha kuaminika.
Kwa upande wake, Dk Lwaitama anasisitiza umuhimu wa ushirikishwaji kikamilifu wa wananchi pale Serikali zinapotaka kufanya mabadiliko ya kisheria kupitia bungeni ambayo yanaathiri Katiba ya nchi.
Anasema, bila ushirikishwaji kamili wa umma, kunaweza kuibua migogoro kwa kuwa wapinzani wa mkakati huo wanaweza kupata uungwaji mkono na jamii katika kutetea maslahi ya umma na kuingia mgogoro na mamlaka za dola zinazotumika kuzima upinzani huo.
“Katiba ni kama dira. Cha msingi ni wananchi wanashirikishwa kwa kiasi gani. Maana watu wamekubaliana baadaye anaibuka mtu anapeleka bungeni kifungu kibadilike. Hapo matatizo yanatokea," anasema.
Anasema viongozi wengi wanaobadilisha katiba kirahisi ili waendelee madarakani huingia katika mgogoro wa moja kwa moja na upinzani kwa sababu katiba ndiyo makubaliano ya msingi ya namna nchi inapaswa kuendeshwa.
Wakati wachambuzi wa siasa wakijadili udhaifu wa taasisi na changamoto za katiba, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza anatoa tahadhari tofauti.
Kwa mtazamo wake, matumizi ya nguvu kupita kiasi katika kushughulikia migogoro ya kisiasa ni miongoni mwa sababu za vilio hivyo.
Anasema matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa taasisi za dola dhidi ya upinzani yanaweza kuleta madhara ya muda mrefu kwa uongozi na taifa.
“Viongozi wenye madaraka wanapaswa kupunguza matumizi ya nguvu na kuongeza hekima, busara na maridhiano,” anasema.
Askofu Bagonza anasema matumizi ya nguvu katika kushughulikia changamoto za kisiasa yanaweza kuathiri nguvu na taswira ya kisiasa ya utawala wowote.
Pia, anamrejea Mwalimu Julius Nyerere, akisisitiza kwamba aliwahi kuonya kuwa baadhi ya uamuzi unaofanywa kwa hasira au kwa kutumia nguvu huacha majeraha ya muda mrefu katika historia ya taifa.
“Wenye madaraka punguzeni nguvu, ongezeni hekima,” anasema.
Kauli hiyo inaonekana kugusa kiini cha changamoto ya Afrika ya leo. Bara linaloendelea kutafuta namna ya kujenga demokrasia za ushindani wa kweli bila kugeuza tofauti za kisiasa kuwa vita kati ya dola na upinzani.