Prime
Makada Chadema walivyohojiwa Polisi kuhusu maandamano
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, tangu Kihongosi kudai Chadema inafanya vikao vya siri kupanga maandamano, imewaweka viongozi wa chama hicho mikoa mbalimbali kwenye kipindi kigumu kwa kuwa, wamekuwa wakiitwa kuhojiwa na Jeshi la Polisi
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kadhia ambayo viongozi wake wanakutana nayo ikiwamo kukamatwa au kuitwa polisi kuhojiwa ni matokeo ya tuhuma zilizotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi kuwatuhumu kupanga maandamano.
Chadema imelitaka Jeshi la Polisi kumwita kiongozi huyo wa CCM kumhoji na kuthibitisha madai hayo aliyoyatoa.
Chama hicho kimebainisha hayo wakati baadhi ya wanachama na viongozi wake wa maeneo mbalimbali nchini wakikamatwa au kuitwa polisi kuhojiwa akiwamo Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai na Katibu wa Kanda ya Serengeti Jackson Mnyawami.
Juni 13, 2026, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kihongosi aliituhumu Chadema kuacha ajenda za kisiasa na kujihusisha na uhamasishaji wa vurugu na maandamano.
Katika kauli hizo zilizozua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, Kihongosi alidai kuwa taarifa alizosema ni za uhakika, Chadema inafadhiliwa na watu kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuvuruga amani ya Taifa inayoweza kuvurugika kwa muda mfupi lakini kuijenga ni jambo linalohitaji juhudi kubwa.
Mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema, Gervas Lyenda amesema chama hicho bado kinaendelea kukusanya taarifa za makada na viongozi waliohojiwa, kushikiliwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana, kwa lengo la kupata takwimu kamili za matukio hayo.
“… tumepokea taarifa za kukamatwa kwa Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Songea pamoja na makada sita wa mkoa huo.
“Pia, makada wanne na kiongozi mmoja wa vijana wamekamatwa Mwanza na Dar es Salaam, aliyeitwa polisi ni Boni Yai,” amesema Lyenda.
Amesema chama kinaendelea kukusanya taarifa kutoka maeneo mengine nchini ili kubaini idadi kamili ya waliokamatwa, waliopata dhamana na kuachiwa, pamoja na wale wanaoendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
Taarifa fupi aliyoitoa usiku wa jana Jumatatu, Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amesema watu waliojitambulisha kuwa ni polisi wamefika nyumbani kwa Mnyawami, wamemchukua na kuondoka naye, wakisema walikuwa wanamhitaji kituo cha polisi Shinyanga.
“Wamemchukua akiwa nje anataka kuingiza gari lake ndani ,nilikuwa naongea naye akiwa ananipa mrejesho wa uchaguzi wa Mkoa wa Shinyanga na ratiba ya chama ya kesho (leo) ya Mkoa wa Simiyu,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, kuhusu suala la kuitwa kuhojiwa kwa Boni Yai, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kiongozi huyo aliitwa katika Ofisi za Polisi Kinondoni kwa ajili ya mahojiano kuhusu tuhuma zilizowasilishwa dhidi yake.
Muliro amesema hatua hiyo ililenga kumpatia Boni Yai nafasi ya kujitetea kabla ya hatua yoyote, jambo ambalo ni haki ya msingi kwa mujibu wa sheria.
“Ni kweli tulimuita kuhojiwa, na amehojiwa kuhusu tuhuma tulizozipokea ili kumpatia nafasi ya kujitetea kabla ya kumtuhumu, ambayo ni haki ya msingi ya kisheria. Baada ya mahojiano, alipewa dhamana na kuondoka,” amesema Muliro.
Amesema jukumu la kisheria la Jeshi la Polisi ni kuzuia vurugu kabla hazijatokea, na si kusubiri zitokee ndipo lichukue hatua.
Jitihada za kuwapata makamanda wa polisi wa maeneo ambayo kuna taarifa za makanda na viongozi kukamatwa au kuitwa kuhojiwa zinaendelea.
Kilichotokea Dar
Leo Jumanne, Juni 16, 2026, Boni Yai baada ya kutoka kuitikia wito wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni amesema Kihongosi, ni sababu viongozi mbalimbali wa Chadema kuendelea kupata usumbufu, ikiwamo kuitwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuhojiwa.
Amesema hata yeye kitendo cha kuitwa kwake na kuhojiwa kwa takribani saa tatu ni kutokana na madai hayo ya Kihongosi huku akitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuzipuuza na kumuita Kihongosi kuthibitisha ukweli wa madai hayo ambayo yamekuwa mtihani kwao.
Boni Yai ambaye amewahi kuwa Meya wa Kinondoni na Ubungo Dar es Salaam amesema licha ya kukanusha tuhuma hizo, ameliomba Jeshi la Polisi limuite Kihongosi ili athibitishe madai yake.
“Nimefika kuitikia wito wa Jeshi la Polisi nikiwa na viongozi, wanachama na mawakili wangu. Nimehojiwa kwa saa tatu kuhusu tuhuma za kufadhili na kutoa fedha kwa ajili ya kuratibu maandamano ya Julai 7, 2026. Nimeeleza kuwa tuhuma hizo ni uzushi na propaganda za watu wenye nia ovu,” amesema.
Boni Yai amesema tuhuma hizo ambazo Kihongosi alizisema ndizo zilizomfanya aitwe na Jeshi la Polisi kuhojiwa, huku akidai ametuhumiwa kuwagawia watu fedha ili wasambaze vipeperushi vya kuhamasisha maandamano katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nimetuhumiwa kuwagawia watu fedha kwa ajili ya kusambaza vipeperushi vya kuhamasisha maandamano katika Mkoa wa Dar es Salaam, jambo ambalo si la kweli kabisa,” amedai Boni Yai.
Amelitaka Jeshi la Polisi kuzipuuza taarifa hizo kwa kuwa hazina udhibitisho huku viongozi wengine wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikamatwa na kuhojiwa kutokana na madai hayo.
“Kwa siku tatu zilizopita viongozi wa Chadema tumekuwa tukiishi kwa mashaka. Tumekuwa tukiitwa kuhojiwa kwa tuhuma hizi, lakini hakuna ukweli wowote. Tunaliomba Jeshi la Polisi kuzipuuza kwa kuwa hakuna ushahidi wa kuzithibitisha; ni kusumbuana na kupotezeana muda tu,” amesema.
Amesema CCM kupitia Kihongosi wanadai Chadema inafanya vikao vya siri kupanga maandamano.
Boni Yai kutokana na madai hayo, alilitaka Jeshi la Polisi kumuita Kihongosi ili aeleze ni wapi na lini vikao hivyo vinadaiwa kufanyika.
“Baada ya kauli za Kihongosi kutolewa Dodoma, viongozi wa chama chetu wamekuwa wakipata usumbufu, kukamatwa na hata kuvamiwa majumbani kwa jambo ambalo hatulijui wala kulifahamu. Mimi binafsi leo nilitakiwa kuwa Ifakara, Morogoro, kwa mkutano wa hadhara, lakini nimeshindwa kutokana na hali hii,” amesema.
Amesema mahojiano yaliyofanyika yalidumu kwa saa tatu, yakijikita katika tuhuma ambazo anazieleza kuwa hazina msingi, huku akidai kuwa kauli za mtu mmoja zinawafanya viongozi wa chama hicho kusumbuliwa, kushikiliwa mahabusu na kuathiri shughuli za chama.
Boni Yai amedai viongozi wa Chadema wanaendelea kukumbana na changamoto hizo kote nchini.
Amesema kwa kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama vikubwa vya upinzani nchini, kila panapotokea taarifa za maandamano mara nyingi huanza kuhusishwa nacho.
“Nimeitwa kwa sababu Jeshi la Polisi linaniona kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi ndani ya Chadema. Tunafahamu kuwa Songea kuna kiongozi wetu amekamatwa na bado hajaachiwa. Vijana sita pamoja na Katibu wetu wa Kanda ya Serengeti nao wamekamatwa,” amesema.
Boni Yai amesema, baada ya kufuatilia matukio ya kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho, wamebaini yanahusishwa na tuhuma zilizotolewa na Kihongosi kuhusu madai ya kuwepo kwa vikao vya siri vya kuratibu maandamano, jambo ambalo amesema si la kweli.
"Kama kweli madai ya Kihongosi yana ukweli, basi atoe ushahidi wa kuthibitisha anachokisema, ikiwamo madai ya kugawa fedha kwa ajili ya kusambaza vipeperushi vya kuhamasisha maandamano,” amesema.
Mwananchi imemtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ambaye amesema: “Jeshi la Polisi hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi ili kulinda maisha ya watu na mali zao sambamba na kuendelea kushirikiana na wananchi kulinda na kuimarisha usalama wa nchi.”
“Hivyo Jeshi la Polisi halimkamati mtu yeyote yule bila kuzingatia sheria za nchi na ushahidi unaonesha mtu huyo ametenda au amekaribia kutenda kosa la jinai kwa vitendo na matamshi yake,” amesema.