Boni Yai aripoti Polisi Oysterbay, aambatana na mawakili wawili
Muktasari:
- Polisi wamruhusu Boni Yai, mawakili wawili na wanachama wanne kuingia ndani ya ofisi hizo, huku wengine wakitakiwa kusubiri nje kutokana na idadi ya watu waliofika kuwa kubwa.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob maarufu Boni Yai, amewasili katika Ofisi za Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kwa ajili ya kuitikia wito wa Jeshi la Polisi uliomtaka kuripoti katika ofisi hizo.
Boni Yai amewasili katika ofisi hizo zilizopo Oysterbay leo Jumanne, Juni 16, 2026 saa 10:09 asubuhi, akiwa ameambatana na mawakili wake, akiwemo Hekima Mwasipu, pamoja na viongozi na wanachama wa Chadema waliofika kumuunga mkono wakati wa kuitikia wito huo.
Hata hivyo, baada ya kuwasili katika kituo hicho, ni Boni Yai, mawakili wawili na wanachama wanne pekee walioruhusiwa kuingia ndani ya ofisi hizo kwa hoja iliyojengwa na Polisi walikuwa wanachama wengi hivyo kutakiwa kukaa nje kuwasubiri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa jana Jumatatu Juni 15, 2026 na Katibu wa Kanda ya Pwani wa Chadema, Ntele Benjamin, alisema Boni Yai alipokea taarifa za wito huo akiwa safarini kuelekea Ifakara mkoani Morogoro kushiriki mikutano ya hadhara ya Chadema Kanda ya Kati.
Benjamin alisema Boni Yai alipigiwa simu na Jeshi la Polisi kutoka Wilaya ya Kimara na kufahamishwa kuwa kulikuwa na maelekezo rasmi yaliyomtaka kufika katika Ofisi za RCO wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam, leo.
“Jeshi la Polisi limemtaka afike katika ofisi hizo akiwa ameambatana na mawakili wake au watu wake wa karibu,” alisema Benjamin.
Kufuatia wito huo, Benjamin aliwataka mawakili, viongozi wa chama, wanachama na wadau wa haki za binadamu kujitokeza kumuunga mkono Mwenyekiti huyo wa Kanda ya Pwani katika safari yake ya kuelekea ofisi za polisi kwa ajili ya kuitikia wito huo.
Viongozi wa Chadema walifika katika ofisi hizo ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Pamela Maasay, ambaye hajaruhusiwa kuingia katika kituo hicho.
Endelea kufuatilia Mwananchi