Prime
Boni Yai aibua mapya CCM Dar kujimilikisha maeneo ya wazi, yenyewe yamjibu
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai amekinyooshea kidole Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, akidai kimejimilikisha maeneo mengi ya wazi kinyume cha utaratibu.
Kwa mujibu wa Boni Yai, maeneo ambayo miaka kadhaa iliyopita, wakiwa madiwani na mameya, waliogopa kuyagusa, hivi sasa yamenyakuliwa huku akikiinyooshea mkono chama hicho kwa kuyashikilia kwa ajili ya shughuli za kibiashara.
Boni Yai aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa za Kinondoni na Ubungo, ameeleza hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, akisimulia uzoefu wake kwa anayojajua na kile anachokiona kwenye maeneo hayo.
Wakati Boni Yai akitoa shutuma hizo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga amesema ikiwa Chadema wanaona chama hicho tawala kinamiliki maeneo hayo kinyume cha utaratibu waende mahakamani.
“Waendee mahakamani wakadai kuhusu viwanja kama ni mali yao au vinginevyo, lakini waende kwenye sheria. Tuna hati za maeneo yetu, tuna vielelezo vya muda mrefu, kama wanadhani wana hoja basi tusiongee kilevilevi wakati mahakama zipo, sheria zipo,” amesema Bananga.
Bananga amesisitiza maeneo kama Biafra ni mali ya CCM kwa miaka mingi na waliyatumia kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya chama hicho.
“CCM si chama cha kuombaomba, pale ndiyo mahali fedha zilipo, sisi siyo wa tonetone, tuna mali. Kama wanadhani kuna jambo halipo sawa mahakama zipo. Zile ni mali zetu tunazomiliki kihalali, tuna vielelezo vinavyotupa uhalali, ni mali yetu kwa maendeleo ya chama,” amesisitiza Bananga.
Anachokijua Boni Yai
Boni Yai amesema alipokuwa meya wa Kinondoni mwanzoni mwa mwaka 2020 akiwa pamoja na wajumbe wa kamati ya ardhi, walipita kata mbalimbali za halmashauri hiyo kwa lengo la kukagua na kujionea maeneo ya wazi yaliyohifadhiwa.
Amesema miongoni mwa maeneo waliyotembelea na kukagua ni pamoja na Mbezi Beach, Ununio, Bahari Beach, Masaki, Mabibo Sahara na Tegeta, lakini kwa sasa yote yamepimwa na watu wamejenga makazi.
Amejenga hoja yake akieleza umuhimu wa kuwepo kwa viongozi imara wa upinzani katika nafasi mbalimbali za uwakilishi wa wananchi, akisema wasipokuwapo kila kitu kinakuwa tofauti na zinakosekana sauti za kuwatetea Watanzania.
“Tunajaribu kuwaonyesha watu ukiondoa kuchagua mwakilishi wa upinzani ngazi ya mtaa, ukamkosa diwani au mbunge kwa kura yako na kubaki CCM wenyewe, hakuna litakalofanyika,” amesema diwani huyo wa zamani wa Ubungo.
Boni Yai ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amefafanua kwenye kata, mitaa, vijiji, vitongoji na majimbo, CCM kimeongoza kwa kutoa wawakilishi, hivyo ni vigumu kwa maeneo ya wazi kusalimika.
Amedai akiwa meya wa Manispaa ya Kinondoni alikuta ofisini kwake ripoti ya kamati ya kuchunguza maeneo ya wazi mkoani Dar es Salaam, iliyoundwa na aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa huo, William Lukuvi (marehemu sasa).
Boni Yai amesema ripoti hiyo ilibainisha kwamba eneo la Biafra lililopo Kinondoni ni mali ya umma. Amesema kamati hiyo ilipitia mpango mkakati wa Mkoa wa Dar es Salaam na ramani za mipango miji ya mkoa, inayoonyesha mipango ya maeneo ya wazi na kujua yanamilikiwa na nani.
“Ile ripoti ya Kamati ya Lukuvi ilionyesha maeneo mengi ya wazi yalivamiwa na CCM kwa asilimia 70 huku wananchi wa kawaida wakiwa wamevamia asilimia 30. CCM wakishavamia wanajenga vibanda au kulaza magari.
“Ndiyo maana tunawaambia wananchi, pamoja na mengi yote haya, ukikosa uwakilishi imara katika ngazi mbalimbali za uongozi, basi watarajie mambo kwenda tofauti, ikiwemo maeneo ya wazi kuhodhiwa na watu wachache,” amedai Boni Yai.
Katika mazungumzo hayo, Boni Yai amesema Sinza, pia, kuna eneo la wazi, lakini CCM wamelichukuwa na kulimiki.
“Nyuma ya Sinza Lion, pale kuna eneo kubwa kabisa la uwanja wa mpira ambalo hadi sasa linaitwa uwanja wa CCM, lakini linajulikana kama eneo la wazi, hivi sasa limejengwa fremu, ofisi na kuweka gereji. Ripoti ya Kamati ya Lukuvi inaonyesha ni eneo la wazi, lakini limevamiwa na CCM,” amebainisha mwanasiasa huyo.
Amesema kuna skendo iliibuka huko Mbezi Beach ya ‘Botanical Garden’ iliyosababisha Idara ya Ardhi Kinondoni kufumuliwa yote na wahusika walikamatwa wakafikishwa mahakamani, kisha kufungwa gerezani.
“Hawa si kwamba waliuza au kupima viwanja, bali eneo lilipimwa na mipango miji ya Dar es Salaam kwa ajili ya watu kupumzika kama vile Forodhani Zanzibar, kuwepo na bembea ili watoto wacheze, lakini leo watu wameuza viwanja, wakubwa wamegawana na maghorofa yamejengwa, sasa si eneo la wazi tena,” amesema.
Boni Yai ameongeza kuwa: “Sasa maeneo ya namna hii yalikuwa mengi sana, nimekuwa meya Kinondoni najua.”
Amesema zamani wakati wakiongoza halmashauri, waliyaheshimu maeneo ya wazi wakiamini ni mali za Serikali, likiwemo eneo la pembezoni mwa ubalozi wa Marekani, Msasani ambalo nalo amedai limechukuliwa.
Ametaja eneo jingine kuwa ni Mabibo Sahara ambalo amedai ni la umma tangu akiwa mdogo, wamecheza mpira hapo, lakini sasa wananchi wanaambiwa kuna mmiliki ambaye ni kijana wa umri wake.
“Hawa wote waliohodhi maeneo ya umma, mbona hatujasikia wakipelekwa mahakamani au kwenye vyombo vya dola, badala yake wamemkamata mwenyekiti wetu (Tundu Lissu) ambaye anatetea haki za wananchi” anasema Boni Yai.
Mapokezi makubwa
Kuhusu mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Kanda za Chadema za Kaskazini, Victoria na Serengeti, Boni Yai amesema kumekuwa na mwitikio mzuri hasa wananchi wanavyojitokeza kukisaidia chama hicho rasilimali fedha ili kiendelee kufanya mikutano hiyo.
“Chadema tupo vizuri, nchi imeamka, kama unavyojua chama hakina ruzuku lakini wanachama na wananchi wanakichangia chama. Tunafanya mkutano Katoro, fedha zilizopatikana zilikwenda kufanya mkutano Geita.
“Fedha ziliyopatikana Geita zikatuwezesha kufanya mkutano Kahama, fedha za Kahama zikaenda kufanya mkutano Arusha. Wananchi wana uhitaji, maana sisi hatubebi watu kwenye magari,” amesema Boni Yai.
Boni Yai ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika mikutano hiyo, amesema miaka ya nyuma iliwazimu kuweka bajeti ya uratibu wa bodaboda ili kupata mapokezi lakini hivi sasa hali imebadilika, badala yake waendesha pikipiki wenyewe wamekuwa wakijitolea kufanikisha suala hilo.
“Sasa hivi mambo yamebadilika, nimeshuhudia hivi Kahama na Arusha, bodaboda wamejiratibu wenyewe pasipo kuwekewa mafuta au kutaka posho kutoka Chadema. Yote hii maana yake wananchi wameamka na hali ya kisiasa nzuri na CCM isiwachukuliwe poa,” amesema Boni Yai.
Boni Yai amewasihi Watanzania kuendelea kukichangia chama hicho, akisema kwa sasa kinajiendesha bila ruzuku kwa sababu hakikushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.