Wanne mbaroni tuhuma mauaji raia wa China, fedha zanunua ng'ombe
Muktasari:
- Jeshi la Polisi limewakamata watu wanne wanaotuhumiwa kumuua mfanyabiashara raia wa China, huku wawili wakidaiwa kimbilikua mpakani. Sehemu fedha zilitumika kununulia mifugo.
Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewakamata watu wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Bhaozang Ge, mfanyabiashara raia wa China na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL Li, kilichopo eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam.
Mfanyabiashara huyo aliuawa na walinzi wa kiwanda hicho usiku wa kuamkia Mei 16, 2026.
Mwili wa Bhaozang ulichomwa moto Mei 24, 2026 katika eneo maalumu Makumbusho jijini Dar es Salaam na majivu yake kusafirishwa kwenda China, Mei 27 kwa taratibu za mazishi.
Watuhumiwa wa mauaji ya mmiliki namfanyabiashara wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI kilichopo Mabibo, Dar es Salaam wakiwasili katika Kituo cha Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.
Leo Jumatano, Juni 10, 2026 Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari, amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa kufuatia tukio hilo lililosababisha taharuki miongoni mwa ndugu, jamaa wa marehemu na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Amesema watuhumiwa wawili walinaswa Namanga wakiwa wamekimbilia eneo la mpakani huku wengine wawili wakikamatwa Mabibo, jijini Dar es Salaam walikokuwa wakijificha baada ya kutoroka.
"Tukio hilo la mauaji lilisababisha taharuki miongoni mwa ndugu, jamaa na watu waliomfahamu marehemu, hali iliyolifanya Jeshi la Polisi kuanzisha uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi," amesema Muliro.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, watuhumiwa hao walipohojiwa walikiri kupanga njama kwa pamoja za kumvamia marehemu usiku, kumshambulia na baadaye kumuua, kisha kuiba fedha Sh9 milioni zilizokuwa ndani ya kiwanda hicho.
“Baada ya kutenda tukio hilo, walichukua fedha hizo na kutorokea maeneo mbalimbali nchini wakidhani wataepuka mkono wa sheria, lakini uchunguzi wetu uliwafikia na kufanikisha kukamatwa kwao,” amesema.
Watuhumiwa wa mauaji ya mmiliki namfanyabiashara wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki cha XIL LI kilichopo Mabibo, Dar es Salaam wakiwasili katika Kituo cha Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.
Waliokamatwa ni Godson Simon maarufu Laizer (25), mkazi wa Olkolili, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Elisha Saitoti maarufu Luqmay (24), mkazi wa Mkonde, Handeni mkoani Tanga, Godfrey Laban maarufu Mollel (30), mkazi wa Makongo, Kinondoni na Godson Pineli maarufu Lisika (24), mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema baadhi ya watuhumiwa hao wamekiri kutenda uhalifu huo na kueleza namna walivyotumia sehemu ya fedha walizoiba, ikiwamo kununua ng’ombe ambao tayari wamekamatwa na kuchukuliwa kama vielelezo vya kesi.
“Taratibu zote za kisheria za kuhifadhi na kurekodi vielelezo hivyo zinaendelea. Watuhumiwa hawa watafikishwa katika vyombo vya sheria ikiwamo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani,” amesema.
Amesema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za uchunguzi na mashauri kukamilika.
Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani.
Pia, Muliro amesema Polisi halitakuwa na huruma kwa wahalifu na litaendelea kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria, akionya kuwa vitendo vya uhalifu huwasukuma wahusika katika migogoro mikubwa ya kisheria na kuathiri maisha yao pamoja na familia zao.
Kamanda huyo pia amewashukuru wananchi waliotoa ushirikiano kwa vyombo vya dola katika kufanikisha uchunguzi na ukamataji wa watuhumiwa hao.
“Ushirikiano wa wananchi umekuwa muhimu sana katika kufanikisha uchunguzi huu. Tunawaomba waendelee kutoa taarifa za uhalifu ili tuendelee kulinda usalama wa jiji letu,” amesema.